Mwandishi chipukizi TSN afariki dunia

MWANDISHI wa habari chipukizi wa vyombo vya habari vya digital vinavyomilikiwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) maarufu kama Daily News Digital, Katuma Masamba (pichani) amefariki dunia.

Taarifa iliyotolewa na Naibu Mhariri Mtendaji wa TSN, Tuma Abdallah ilisema Katuma (24) alifariki dunia jana jioni katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam, alikokimbizwa ili kupatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla juzi akishiriki Jukwaa la Biashara la TSN mjini Zanzibar.

Mjomba wa marehemu, Shamte Ally alisema hospitalini hapo jana kuwa mipango ya mazishi ya Katuma ambaye awali alikuwa mwandishi wa habari wa gazeti hili, itafanyika baada ya kikao cha familia kukaa leo.

Dada wa Katuma, ambaye ni mfanyakazi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Nyambona Masamba alisema ndugu wamepokea kwa mshituko mkubwa taarifa za kifo hicho cha Katuma. Taarifa zaidi kuhusu mazishi ya Katuma, zitaendelea kutolewa kwa kadri mipango itakavyokuwa inakwenda. Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wa TSN, wanaungana na familia ya marehemu katika wakati huu mgumu wa maombolezo.