‘Mliotafuna fedha za maji jiandaeni kutapika’

NAIBU Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amesema, yeyote aliyetafuna fedha za miradi ya maji ajiandae kuzitapika. Aweso amesema, Serikali haina mzaha na yeyote kwa kuwa ni jukumu la Serikali kuwapatia wananchi maji.

Ametoa msimamo huo bungeni mjini Dodoma wakati anajibu swali la nyongeza Mbunge wa Serengeti, Marwa Chacha.

Aweso amesema, maji hayana mbadala, si kama wali kwamba ukiukosa utakula ugali au vyakula vingine.

Wakati anajibu swali la nyongeza Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda, Aweso alisema, mkandarasi yeyote atakayechelewesha wananchi kupata maji ataondolewa, atawekwa mwingine ili wananchi wapate huduma hiyo muhimu.

Wakati anajibu swali la msingi la Mbunge wa Vitu Maalum, Lucy Owenya, Aweso alisema, katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Prgramu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP 1), Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ilipanga kutekeleza miradi ya maji katika vijiji 12.

Kwa mujibu wa Aweso, kati ya hivyo, ujenzi wa miradi umekamilika katika vijini sita vya Korini Juu, Korini Kati, Korini Kusini, Kirima Juu, Kirima Kati na Boro.

“...na utekelezaji wa miradi iliyobaki unaendelea kufanyika katika Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP II)” amesema Aweso wakati wa kikao cha kwanza cha Mkutano wa 11 wa Bunge la Tanzania.