Mtoto wa Kova, wenzake 5 kortini

MTOTO wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, Masoud Kova na wenzake watano, wamefi kishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kuisababishia hasara Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ya Sh milioni 26.

Mbali ya Kova ambaye ni Mtaalamu wa Uhasibu wa TPA, wengine ni maofisa uendeshaji wa mamlaka hiyo, Lydia Kimaro (52) na Ally Mkango (54) pamoja na Mtaalamu wa uhasibu, Aron Luisinga (35), maofisa wa Benki ya CRDB, Grace Komba (41) na Juma Ng’oka (41) ambao walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba. Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono alidai kuwa washitakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka matano ya uhujumu uchumi.

Wakili Kombakono alidai kuwa mashitaka ya kwanza ya kughushi yanawakabili washitakiwa Kimaro na Kova, ambao wanadaiwa kati ya Agosti na Septemba 2014, katika Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa na nia ya kudanganya walighushi nyaraka za uongo ili kuonyesha TPA imehusika katika malipo ya kiasi cha Sh milioni 26 kutoka kwa Cargo Service Invoice (CSI) kitendo ambacho si kweli.

Pia Kimaro na Kova wanadaiwa kati ya Agosti na Septemba 2014 katika Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa na nia ya kudanganya walighushi nyaraka kuonesha kuwa TPA imehusika kufanya malipo ya Sh milioni 26 kutoka Kampuni ya Freight Forwarders (T) hali ya kuwa ni uongo. Wakili Kombakono alidai kuwa kati ya Septemba na Oktoba 2014, maeneo ya Dar es Salaam washitakiwa wote kwa pamoja walijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Pia inadaiwa kwa pamoja walijipatia kiasi cha Sh milioni 26 kutoka kwa Freight Forwarders na kudanganya kuwa fedha hiyo imelipwa katika akaunti ya TPA iliyopo Benki ya CRDB kitendo ambacho sio kweli. Washitakiwa Mkango na Lusingu wanadaiwa kati ya Septemba na Oktoba 2014, walishindwa kuzuia makosa kufanyika, ambapo wakiwa waajiriwa wa TPA walishindwa kuzuia kutendeka kwa kosa kwa kutokagua upande wa TPA na Cargo Service Invoice (CSI) hali iliyosababisha Freight Forwarders kutoa makontena 16 bila kulipiwa kodi ya Sh milioni 26 kwa TPA. Kombakono alidai kati ya Septemba na Oktoba 2014, maeneo ya Dar es Salaam, ka nia ovu walisababishia TPA kupata hasara ya Sh milioni 26. Washitakiwa hao walikana mashitaka hayo. Washtakiwa wako nje kwa dhamana.