Mishahara kuendana na gharama za maisha

OFISI ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeomba kuidhinishiwa bajeti ambayo pamoja na malengo mengine, itaandaa taarifa za gharama za maisha kama msingi wa kukadiria kima cha chini cha mshahara unaoendana na gharama halisi za maisha.

Aidha, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali Mitaa katika maoni yake, imeshauri serikali iongeze mshahara kwa watumishi wa umma kuwawezesha kumudu gharama za maisha ambazo zinaongezeka. Akiwasilisha bungeni makadirio ya matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2018/19, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti na Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika ameomba aidhinishiwe jumla ya Sh 669,094,556,009. Kulingana na taarifa ya Waziri, miongoni mwa malengo yaliyopangwa kutekelezwa na ofisi hiyo katika mwaka ujao wa fedha kwa upande wa Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma ni kuandaa taarifa nne za gharama za maisha kama msingi wa kukadiria kima cha chini.

“Taarifa hizi zinaweza kushauri kuhusu mshahara wa chini unaoendana na gharama halisi za maisha, “ alisema Mkuchika katika hotuba yake. Chini ya eneo hilo la mishahara na maslahi kwa utumishi wa umma, kupitia bajeti hiyo iliyoombwa, ofisi itafanya utafiti wa hali ya masilahi katika utumishi wa umma nchini na mifumo ya kupima utendaji kazi. Lengo ni kushauri namna bora ya kutoa motisha kwa kuzingatia utendaji ili kuongeza ufaisi katika kuhudumia wananchi. Vile vile itatekeleza mapendekezo yanayotokana na kazi ya tathimini kazi na uhuishaji wa madaraja katika utumishi wa umma.

Ili kutekeleza mpango wa bajeti ya mwaka ujao wa fedha, Mkuchika alisema Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma imeomba kutumia Sh 1,652,435,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Kamati ya Kudumu ya Bunge katika ushauri wake kwa serikali kuongeza mshahara, ilisema wote ni mashahidi kwamba serikali haijaongeza mshahara wa watumishi wa umma kwa mwaka wa tatu sasa.

Ofisi hiyo ya Rais pamoja na mafungu yake imepanga kutekeleza malengo 209, ikiwemo kutoa huduma kwa Rais na familia yake; kumshauri Rais katika maeneo ya uchumi, siasa, masuala ya jamii, sheria, mawasiliano na habari kwa umma, uhusiano wa kikanda, kimataifa na maeneo mengine. Malengo mengine ni kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa mkakati wa taifa dhidi ya rushwa awamu ya tatu (NACSAP III); Kuifanyia mapitio sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya 2007 ili kujumuisha makosa ya uhujumu uchumi na kutaifisha mali zilizopatikana kwa njia ya rushwa na ufisadi.

Imepanga pia kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo kwenye taasisi za umma zinazotolewa na serikali na wabia wa maendeleo ili kuhakikisha utekelezaji wake unazingatia thamani halisi ya fedha. Ofisi hiyo ya Rais pia itatumia njia za mawasiliano za kimkakati kufikia kundi la vijana ili washiriki katika shughuli zinazowajengea maadili na hivyo kujenga jamii inayochukia rushwa.

Vile vile itafanya utambuzi na uandikishaji wa kaya masikini zipatazo 355,000 katika vijiji 4,408, mitaa 1,189 na shehia 96 ambazo hazikufikiwa katika awamu ya kwanza. Aidha itaweka na kuhuisha mfumo wa utunzaji wa kumbukumbu za kiutendaji za watumishi katika taasisi za umma 58 ili kuboresha utoaji wa huduma. Hata hivyo kamati katika taarifa yake ilisema uchambuzi wake umebaini kiasi kilichoombwa na ofisi kuidhinishiwa kimepungua kwa Sh 152,227,791,665 sawa na asilimia 18.53 ikilinganishwa na bajeti iliyoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2017/18 ambayo ilikuwa Sh 821,322,347,674. Kwa mujibu wa kamati, kiasi kilichopungua ni kikubwa zaidi kwani ni takribani mara tatu ya kiasi kilichopungua katika mwaka wa fedha unaoisha ambacho kilikuwa asilimia 6.89.