Mpango, Jafo watoa hoja nzito ripoti ya CAG

WAZIRI wa Fedha na Mpango, Dk Philip Mpango ametoa majibu ya Serikali katika maeneo manane, yaliyoibuliwa katika taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka unaoishia Juni 30, mwaka jana, ambayo hayakutekelezwa vizuri.

Waziri mwingine ambaye naye ametoa maelezo ya serikali kuhusu ripoti hiyo ya CAG ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ambaye amesema wafanyakazi 434 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu na kisheria, baada ya kubainika kuwa wamezisababishia hasara halmashauri zao.

Walitoa ufafanuzi huo, walipozungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma jana. CAG aliwasilisha ripoti hiyo bungeni Aprili 11, mwaka huu, baada ya kuwa ameiwasilisha kwa Rais John Magufuli Machi 27, mwaka huu. Akijibu hoja ya Deni la Taifa (DLT), Dk Mpango alisema Tanzania ina uwezo wa kuendelea kukopa, kutokana na ukweli kwamba nchi ipo vizuri, hivyo itaendelea kukopa kwa ajili ya kuendeleza, kutekeleza na kukamilisha miradi ya maendeleo nchini. CAG alibainisha kuwa Deni la Taifa hadi kufikia Juni 30, mwaka jana, lilifikia Sh bilioni 46,081.43 na halikuunganisha na madeni ya Mifuko ya Pensheni ya Sh bilioni 4,588.39, kiwango alichosema serikali inatakiwa kuwa makini nacho.

Dk Mpango alisema katika viashiria vya deni baada ya kufanya tathimini Novemba mwaka jana, ilionesha kwamba Deni la Taifa lilikua kwa asilimia 34.4 wakati ukomo wa kimataifa ni asilimia 56, hivyo bado deni hilo halijafikia kiwango cha kutokuwa stahimilivu, hivyo nchi inaweza kuendelea kukopa. Alisema sababu nyingine za kuendelea kukopa ni kutokana na ukweli kwamba thamani ya sasa ya deni la nje, imefikia asilimia 19.7 wakati ukomo wa kimataifa ni asilimia 40.

Pia thamani ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 81.8 wakati ukomo wake ni kimataifa ni asilimia 150, huku thamani ya deni la nje kulinganisha na mapato ya ndani ni asilimia 117.1 wakati ukomo wa kimataifa ni asilimia 200. Mpango alisema kutokana na vigezo hivyo, Tanzania bado ina uwezo wa kuendelea kukopa kutokana na mapato yake na uwezo wa kuuza nje pamoja na kulipa deni hilo.

CAG alizungumzia pia ongezeko la deni la matibabu nje ya nchi la Sh bilioni 17.13, ambalo linakua kutokana na wagonjwa kurudi kutibu maradhi kwa muda mrefu yakiwamo ya saratani, figo za kupandikizwa, mishipa ya fahamu, upasuaji wa mifupa, moyo na aina ya magonjwa ya watoto. Akijibu hoja hiyo, Waziri Mpango alisema serikali imeweka mkakati wa kulipa deni kwa wakati, kuweka bajeti halisia, kuimarisha huduma za kibingwa kwa kuongeza mafunzo kwa madaktari bingwa, kununua vifaa vya kisasa na uchunguzi na kuendeleza huduma hizo katika hospitali nchini.

Kuhusu hoja ya upungufu katika kushughulikia pingamizi za kodi, ambapo Mamlaka ya Mapato (TRA) ilikuwa na pingamizi za kodi ambazo haijashughulikia za Sh bilioni 738.6, Mpango alisema serikali kupitia TRA imechukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha pingamizi hizi zinatatuliwa. “Hatua hizo ni pamoja na kuunda kikosi kazi cha kushughulikia kesi za kodi, zilizopangwa na kuongeza ufanisi katika kutoa ufafanuzi kwa wafanyabiashara katika masuala yanayohusiana na sheria na kanuni za kodi,” alisema.

Mpango alisema TRA imefanyia kazi hoja ya CAG na kufunga hoja zinazofikia Sh bilioni 223.6, kati ya Sh bilioni 296.09 na kazi bado inaendelea. Kuhusu kesi za muda mrefu katika Mamlaka za Rufaa za Kodi zinazosubiri hukumu, alisema CAG alibainisha kwamba TRA ilikuwa na kesi nyingi za kodi za muda mrefu zenye thamani ya Sh trilioni 4.44 zinazosubiri uamuzi taasisi hizo.

Dk Mpango alisema serikali imechukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha rufaa za kodi hizo, zinatatuliwa kwa wakati kwa kuteua wajumbe wa Bodi za Rufaa za Kodi pamoja na wenyeviti wao na kuongeza bajeti ya matumizi ili kuimarisha utendaji kazi wa bodi hizo. Kuhusu mafuta yaliyosamehewa kodi ya Sh bilioni 11.05, yaliyotumiwa na kampuni zisizostahili, Dk Mpango alisema mafuta hayo yalitumiwa na kampuni zilizopewa kazi na kampuni za madini midogoni. “Tayari serikali imechukua hatua ya kukusanya Sh bilioni 5.53 kwa kupunguza fedha za kampuni kutoka katika akaunti za uchimbaji na juhudi za kukusanya kasi cha Sh bilioni 5.47 zinaendelea,” alisema.

Kuhusu usimamizi na ufuatiliaji usioridhisha wa makusanyo ya madeni ya kodi, alisema TRA inadai kodi Sh bilioni 262.29 kutoka kwa wakopaji mbalimbali, tayari imefuatilia kodi ya Sh bilioni 3.6 ambayo imeshatolea ufafanuzi na kiasi kilichosalia cha Sh bilioni 5.7 kinafanyiwa kazi. Kuhusu upungufu katika ukaguzi wa manunuzi, Dk Mpango alisema taasisi nane za Serikali Kuu zilifanya manunuzi ya vifaa na huduma ya Sh bilioni 52.67, kiasi hicho kinajumuisha malipo ya Sh bilioni 51.8 ambazo serikali imelipia ndege aina ya Bombardier Q 400 iliyopokewa Aprili 2, mwaka huu ili kuimarisha usafiri wa ndege nchini.

Upungufu katika usimamizi wa fedha kwa mwaka 2016/17 katika ubalozi wa Maputo-Msumbiji, alisema serikali imechukua hatua za kinidhamu na kisheria kwa mtumishi aliyehusika na upotevu wa fedha kiasi cha Sh milioni 332.86 kwa kumrudisha nyumbani kutoka ubalozini na kufikishwa mahakamani. Kuhusu upembuzi yakinifu kwa baadhi ya miradi ya Kampuni Hodhi ya Reli (Rahco) iliyopangwa kufanyika, alisema kutokana na ukubwa wa gharama, unaotokana na wingi wa ugumu au changamoto wa miradi.

Aidha pale upembuzi unapobainisha gharama za mradi ni kubwa kuliko kuwa na faida ya kiuchumi na kijamii, hakuna sababu ya kutekeleza. Kuhusu kiasi cha dawa kilichoisha muda wake katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD), alisema kwa mujibu wa Viwango vya Shirika la Afya la Dunia (WHO), kiwango cha dawa kupoteza muda ni kati ya asilimia tatu hadi tano ya bei ya mauzo, hivyo kiwango kilichoripotiwa na MSD ni asilimia 3.4 ambacho hakipo chini ukilinganisha na WHO. Aidha, asilimia 70 ya dawa zilizopatwa na muda nikutokana na mabadiliko ya teknolojia.

Katika hatua nyingine, wafanyakazi 434 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu na kisheria, baada ya kubainika kuwa wamezisababishia halmashauri zao hasara kwa mujibu wa ripoti ya CAG. Takwimu hizo zilitolewa na Waziri Jafo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa baadhi ya mapendekezo ya CAG. Jafo alisema uamuzi huo wa kusimamisha wafanyakazi hao, ulitokana na hoja zilizoibuliwa wakati wa ukaguzi uliofanywa na CAG kutokana na kutotekeleza ipasavyo wajibu wao au kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu.

Kati ya hao, watumishi (9) walifukuzwa kazi, watumishi 201 walipewa barua za onyo, watumishi 15 walifikishwa kwenye vyombo vya dola na watumishi 28 walisimamishwa kazi. Vile vile, watumishi 13 wametakiwa kufidia hasara kutoka kwenye mishahara yao, watumishi wanne wameshushwa vyeo, watumishi 10 wamebadilishiwa majukumu na watumishi 64 wapo katika mchakato wa hatua za kinidhamu unaoendelea.

Kuhusu fedha zilizopelekwa kwenye mamlaka za serikali za mitaa, zimeongezeka katika mwaka wa fedha wa 2016/17, ambapo zimefikia Sh bilioni 705.9 sawa na asilimia 57 ya bajeti iliyoidhinishwa ya Sh trilioni 1.24, wakati mwaka, fedha za maendeleo zilizopelekwa zilikuwa Sh bilioni 390.5 sawa na asilimia 39 ya bajeti ya Sh trilioni 1.01. Kuhusu vitabu 379 vya kukusanyia mapato kutoka katika halmashauri 21 ambavyo havikuwasilishwa kwa wakaguzi, Jafo alisema, licha ya idadi ya vitabu kuonekana vingi, lakini vimepungua kutoka vile 871 katika halmashauri 57 vilivyokuwapo mwaka 2015/16.

Alisema mkakati wa serikali ni kuhakikisha kwamba halmashauri zote zinakusanya mapato kwa kutumia mashine za kielektroniki badala ya kutumia mfumo wa kukusanya mapato kupitia stabadhi au vitabu vya kuandika kwa mkono. “Serikali imetenga Sh bilioni 1.7 katika bajeti ya mwaka huu 2018/19 kwa ajili ya kununua mashine za kukusanyia mapato ambazo zitasambazwa katika halmashauri zenye uwezo mdogo wa kununua mashine hizo,” alisema. Alisema, halmashauri zilizopata hati zenye mashaka zimepungua kutoka 32 yaani asilimia 19 mwaka wa fedha wa 2015/16, hadi halmashauri 16 sawa na asilimia tisa katika mwaka wa fedha 2016/17.