Magufuli awapandisha vyeo maofisa JWTZ

RAIS na Amiri Jeshi Mkuu, John Magufuli amewapandisha vyeo maofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika vyeo mbalimbali.

Taarifa iliyosomwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo, Ikulu Dar es Salaam jana, ilieleza kuwa Rais Magufuli amempandisha cheo Meja Jenerali Peter Massao kuwa Luteni Jenerali. Meja Jenerali Massao ni Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Maofisa Wanafunzi wa Jeshi Monduli (TMA). Kwa uteuzi huo, sasa JWTZ itakuwa na Luteni Jenerali wawili.

Alisema pia Rais Magufuli amempandisha cheo Brigedia Jenerali Henry Kamunde kuwa Meja Jenerali. Aidha, Rais Magufuli amewapandisha vyeo maofisa 27 wa JWTZ kutoka cheo cha Kanali na kuwa Brigedia Jenerali na Ofisa mmoja kutoka Luteni Kanali na kuwa Kanali. Waliopandishwa vyeo hivyo ni D.D.M Mullugu, J.J Mwaseba, A.S Mwamy, R.K Kapinda, C.D Katenga, Z.S Kiwenge, M.A Mgambo, A.M Alphonce, A.P Mutta, A.V Chakila, M.G Mhagama, V.M Kisiri, C.E Msolla na S.M Mzee.

Wengine ni C.J Ndiege, I.M Mhona, R.C Ng’umbi, S.J Mnkande, A.C Sibuti, M.M Mumanga, I.S Ismail, M.N Mkeremy, G.S Mhidze, M.A Machanga, S.B Gwaya, P.K Simuli na M.E Gaguti. Pia Rais Magufuli amempandisha cheo Luteni Kanali Bernard Mlunga kuwa Kanali na ameteuliwa kuwa mpambe wa Rais. Kanali Mlunga ameteuliwa kuwa mpambe wa Rais, akichukua nafasi ya Kanali Mbaraka Mkeremy, ambaye amepandishwa cheo kuwa Brigedia Jenerali.