Ujasiriamali kuchangia 40% pato la taifa

WIZARA ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imesema, mchango wa sekta ya ujasiriamali mdogo na wa kati katika pato la Taifa utafikia 40% mwaka 2025.

Taarifa ya CAG inaonesha kuwa, sekta hiyo inachangia 35% katika pato la Taifa, na matarajio yalikuwa 40%.

Waziri wa Wizara hiyo hiyo, Charles Mwijage amesema mjini Dodoma kuwa, mwaka 2012 sekta hiyo ilichangia asilimia 28 katika pato la Taifa na mwaka 2017 mchango umefikia 35%.

“Ni matarajio kuwa kiwango hiki kinaweza kufikiwa hata kabla ya mwaka 2025 kama tukiwekeza zaidi mtaji katika sekta hii tutaweza kufikia mchango wa asilimia 60. Kwa sasa Watanzania wengi hasa vijana wameshahamasika kuingia katika ujasiriamali…” amesema.

Amewaeleza waandishi wa habari kuwa, sekta hiyo inaendeshwa na kumilikiwa na wazalendo hivyo kuna fursa nzuri ya kujenga uchumi imara wa Tanzania.

“Kulingana na taarifa zilizopo, sekta nyingine zinazochangia zaidi ni ujenzi asilimia 13, habari na mawasiliano asilimia 13, usafirishaji na uhifadhi mizigo asilimia 11.8, uchimbaji wa madini na mawe asilimia 11 na shughuli za fedha na bima asilimia 10.7” amesema Waziri Mwijage mjini Dodoma.

Amesema, Wizara imeyakubali mapendekezo yote aliyotoa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Mwijage amesema, Wizara na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) tayari wametengeneza mpangokazi wa kutekeleza mapendekezo hayo.

Amesema, Wizara inampongeza na kumshukuru CAG kwa kufanya ukaguzi wa kina na ufanisi katika sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo.

Kwa mujibu wa Mwijage sekta hiyo inaongoza katika kushirikisha Watanzania wengi katika shughuli za kujiongezea kipato.

Amesema, sekta hiyo ni pili kwa kutoa ajira kwa Watanzania ikiifuatia sekta ya kilimo.