Manispaa yataja bei viwanja Dodoma

KUANZIA Aprili 20 mwaka huu Manispaa ya Dodoma itaanza kuuza viwanja 10,864 maeneo ya Mtumba na Iyumbu. Kwa mujibu wa Manispaa hiyo, watakaoomba kununua viwanja hivyo watatakiwa kulipa malipo yote ndani ya mwezi mmoja.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi amewaeleza waandishi wa habari kuwa, wananchi watakaofanya ujanja ujanja wa kupata viwanja vingi wamewekewa mfumo wa kuwadhibiti.

“Viwanja 10,864 vilivyopo eneo la Mtumba na Iyumbu vimekamilika na uuzaji wa viwanja hivyo utaanza Aprili 20 mwaka huu, viwanja 2,600 vipo kwenye hatua za ukamilishwaji na vitaingia sokoni kabla ya Aprili 28 mwaka huu,” amesema.

Viwanja vinavyotarajia kuuza ni miongoni mwa viwanja 19,467 vilivyopimwa kuanzia Januari mwaka huu.

Hadi sasa idadi ya viwanja vilivyopimwa ni Iyumbu(967), Mtumba (9,897), Michese (1,500) na Nala (7,000). Kunambi amesema, mradi huo unagharimu zaidi ya Sh bilioni 44.

Akitoa mchanganuo wa bei ya viwanja kwa mita ya mraba moja, Kunambi amesema, eneo la Mtumba viwanja vimegawanywa katika kanda tatu na kwamba, ukanda ya barabarani kiwanja cha makazi kitauzwa Sh 8,000, makazi na biashara Sh 8,500, biashara 10,000, taasisi 7,000 na viwanda vidogo Sh 20,000.

Amesema ukanda ya kati katika eneo la Mtumba, kiwanja cha makazi ni Sh 6,000, makazi na biashara Sh 7, 500, biashara Sh 8,000, taasisi 5,000 na viwanda vidogo ni Sh 15,000 huku ukanda wa barabara ya Kikombo, kiwanja cha makazi ni Sh 3,000, makazi na biashara 5,500, biashara Sh 6,000 na viwanda vidogo Sh 10,000.

Kunambi amesema eneo la Iyumbu viwanja vya makazi vitauzwa Sh 6,000, makazi na biashara Sh 8,000, biashara Sh 15,000, taasisi Sh 7,000 na viwanda vidogo Sh 20,000.

“Wananchi waliokwishaandika barua za kuomba viwanja manispaa wanatakiwa kufika ofisi za zamani za Halmashauri na kuhakiki majina yao. Ni lazima afike na kitambulisho. Kabla ya kuchagua kiwanja mwananchi anatakiwa kulipa Sh 20,000 kama ada ya maombi.

“Baada ya kuchagua kiwanja atapewa hati ya madai ya kiwanja na kutakiwa kulipa fedha zote ndani ya simu 30 tangu tarehe uliyopokea hati ya madai, atakayeshindwa kiwanja hicho kitauzwa kwa mwingine” amesema Kunambi.

Kuhusu watumishi wa umma wanaohamia Dodoma, Kunambi amesema watapelekewa hati ya madai kupitia makatibu wakuu wa Wizara zao na watatakiwa kufanya malipo ndani ya siku 30.

Amesema lengo la manispaa ni kuhakikisha kila mwananchi anamiliki kiwanja na kuonya kuwa manispaa imeweka mifumo ya kudhibiti wale wanaotaka kujilimbikizia viwanja.