Mvua yaua wanne ikiwemo mwanafunzi baada ya kunyesha siku mbili mfululizo

WATU watatu wameripotiwa kufa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Jiji la Dar es Salaam.

Katika tukio jingine; mwanafunzi wa darasa la sita wa Shule ya Msingi Mwanalugali, Hadija Juma (15) amekufa baada ya kuzama kwenye dimbwi la maji jirani na mto Mpiji wilayani Kibaha mkoani Pwani. Kutoka Dar es Salaam, taarifa ya kufa kwa watu hao ilitolewa jana jijini hapa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu matukio yaliyotokea tangu kuanza kuonyesha kwa mvua hizo. Mambosasa alisema watu hao wamekufa katika maeneo mawili tofauti katika wilaya ya Ilala.

Alisema katika eneo la Tabata Kisiwani watu wawilim mama na mtoto waliripotiwa kufa baada ya nyumba yao kuangukiwa na ukuta wa nyumba ya jirani na kusababisha wote kufa. “Hatujapata majina yao lakini nimeambiwa wameangukiwa na ukuta wa jirani na kusababisha mama na mtoto kufa, tunaendelea kufuatilia zaidi,”alisema Mambosasa. Pia alisema tukio jingine la kifo liliripotiwa eneo la Bonyokwa Kinyerezi ambako umeokotwa mwili wa kijana wa kiume ukiwa umesombwa na maji na umekutwa na majeraha ya kujigonga sehemu mbalimbali za mwili.

Aidha, Mambosasa alisema mbali na mvua hizo kuleta madhara kwa binadamu zimesababisha uharibifu wa barabara katika maeneo mbalimbali ya Jiji na kusababisha barabara hizo kushindwa kupitika. Gazeti hili pia lilimtafuta Ofisa Habari wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA), Monica Mutoni ili kujua kama mvua hizi zitaendelea baada ya taarifa iliyotolewa na TMA kudai kuwa mvua zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa kuisha jana. Alisema kwa sasa hakuna taarifa rasmi ya kuendelea au kutoendelea kwa mvua hizo hadi hapo wataalamu watakapofuatilia ili kubaini kama zitaendelea au la.

Kutoka mkoani Pwani imeripotiwa kuwa mwanafunzi wa darasa la Sita wa Shule ya Msingi Mwanalugali, Hadija Juma (15) amekufa baada ya kuzama kwenye dimbwi la maji jirani na mto Mpiji wilayani Kibaha mkoani Pwani. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwanalugali, Deo Rwekaza alisema kuwa tukio hilo limetokea ambapo mwanafunzi huyo akiwa na wenzake walikwenda shamba kupeleka mbolea na walipokuwa wakirudi walianza kuogelea kwenye dimbwi hilo. Rwekaza alisema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 13, saa 12 jioni baada ya watoto wenzake kutoa taarifa kuwa mwenzao kazama na ndipo majira ya saa moja jioni alikwenda kuopolewa.

Wakati huo huo, kijana mmoja ambaye ametambuliwa kwa jina moja la Karimu (15), mkazi wa Kibwegere amenusurika kuliwa na mamba ambapo amejeruhiwa kwa kung’atwa mkono wake wa kushoto alipokuwa akijaribu kuvuka mto Mpiji akitokea mtaa wa Lumumba wilaya ya Kibaha kwenda Kibwegere wilaya ya Ubungo. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa Mtaa wa Lumumba, Gidion Tairo alisema kuwa kijana huyo alikumbwa na tukio hilo saa 2 usiku alipokuwa akivuka mto akiwa na watu wengine ambao ndiyo waliomwokoa.

Gidion alisema kuwa kijana huyo alikuwa akivuka kwenye mto huo ambapo maji yalikuwa ni mengi yakiwa yamefika kwenye kifuani ndipo mamba alimnasa mkono wa kushoto na kuanza kumvuta kabla ya kuokolewa. “Kijana huyo anaendelea vizuri baada ya kukimbizwa kwenye zahanati ya Kibwegere ambako alipelekwa kwa ajili ya matibabu. Nawataka wananchi kuwa makini wakati wanavuka mto huo katika kipindi hichi cha mvua,” alisema Tairo.