Rais Magufuli ateua majaji 10

RAIS John Magufuli amefanya uteuzi wa Majaji 10 wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka, Wakili Mkuu wa Serikali na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu Dar es Salaam jana, ilisema Rais Magufuli amefanya uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu kwa lengo la kujaza nafasi za majaji waliostaafu. Aidha, ilisema amefanya uteuzi wa Wakili Mkuu wa Serikali na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali kwa lengo la kuhakikisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Mashitaka na Wakili Mkuu wa Serikali zinafanya kazi vizuri zaidi katika kushughulikia masuala ya mahakama.

Majaji wa Mahakama Kuu walioteuliwa na Rais Magufuli jana ni Elvin Mugeta, Elinaza Luvanda, Yose Mlyambina, Immaculata Banzi na Mustafa Sioyani. Wengine ni Paul Ngwembe, Agnes Mgeyekwa, Stephen Magoiga, Thadeo Mwenempanzi na Butamo Philip.

Kabla ya uteuzi huo Butamo alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais. Taarifa hiyo ilisema pia kuwa Rais Magufuli amemteua Evaristo Longopa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Longopa anachukua nafasi ya Ngwembe ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Aidha, Rais amemteua Edson Makallo kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka na amemteua pia Julius Mashamba kuwa Wakili Mkuu wa Serikali huku akimteua Dk Ally Possi kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.