Mahamaka na mkakati wa kutorundika kesi

MAHAKAMA ya Tanzania ambayo imeshughulikia kesi za uchaguzi uliopita kwa haraka kulinganisha na siku za nyuma, imejipanga kuhakikisha inaendelea kuondoa kesi za muda mrefu, ikiwa ni sehemu ya maboresho yanayofanywa na mahakama hiyo.

Ikiwa ni takribani mwezi kupita tangu mahakama hiyo kuadhimisha Siku ya Sheria, Msajili Mkuu wa mahakama hiyo, Katarina Revocati, anasema mahakama imethibitisha kwamba hilo linawezekana kwani takwimu zinaonesha kwamba mwaka jana ulimalizika huku mlundikano wa kesi katika ngazi za mahakama za mwanzo na za wilaya ukiwa sifuri.

Msajili Mkuu huyo anasema katika ngazi ya mahakama za mwanzo mkazo uliopo ni kuhakikisha kesi zinakamilika ndani ya kipindi cha miezi sita.

“Kwa mahakama za wilaya na za hakimu mkazi, kesi inatakiwa kuwa imekamilika ndani ya mwaka mmoja na kwa upande wa mahakama Kuu na mahakama ya rufani kesi zinatakiwa zinamalizike ndani ya miaka miwili,” anasema na kuongeza kwamba moja ya nguzo za mahakama ni kuboresha suala zima la utoaji haki.

Uwezo wa asilimia 100 Wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria mwanzoni mwa mwezi uliopita, Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, alisema pamoja na changamoto ya uwiano usio sawa wa idadi ya majaji, mahakimu na watumishi wengine kama Wasaidizi wa kumbukumbu, wastani wa umalizaji wa kesi katika mahakama hiyo umefikia asilimia 101.

Hiyo ilimaanisha kwamba katika kila mashauri 100 yanayosajiliwa, mahakama ina uwezo wa kuyamaliza kwa asilimia 101. Alisema katika mwaka wa mahakama ulioisha Desemba 2016, jumla ya mashauri 276,147 yalisajiliwa na yaliyokuwa bado yako mahakamani hadi muda huo ni 56,531 tu.

Alifafanua kwamba kati ya hayo, yenye sifa ya kuitwa ya zamani (backlogs) yalikuwa mashauri 3,618 sawa na asilimia sita. Kesi za uchaguzi Profesa Jaji Juma aliongeza kuwa kati ya mashauri 249 yaliyosajiliwa mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi, yaani 53 yakiwa ya ubunge na 196 ya udiwani, hadi kufikia Desemba 30, 2016 mashauri 52 yaliyohusu ubunge yalikuwa yameshaamuliwa, hivyo kubaki na shauri moja.

Shauri hilo pia liliamliwa Feburuari 23. Kwa mujibu wa Profesa Juma, mashauri ya udiwani yalisikilizwa na kuamuliwa yote na kwamba mashauri ya ubunge yalisikilizwa mfululizo kuanzia mwezi Juni mwaka jana mpaka Oktoba 2016 na kwamba yale ya ubunge yalifanywa na majaji 29.

Magufuli aipa agizo mahakama Katika sherehe hizo, Rais John Magufuli ambaye alikuwa mgeni rasmi alipongeza kasi ya usikilizwaji wa mashauri mbalimbali unaofanywa na mahakama. Hata hivyo, aliitaka mahakama kuhakikisha mashauri ya kodi na fedha zilizokwama kutokana na wadaiwa ‘kucheza’ na mahakama kuhakikisha kesi hizo zinamalizika ili serikali ipate fedha hizo zinazofikia sh trilioni 7.5.

Alisema wadaiwa hao hufanya mchezo unaoitwa ‘parking kuzuia mashauri yasimalizike na hivyo kuikosesha serikali mapato ambayo yanategemewa pia na mahakama katika kufanikisha changamoto mbalimbali zinazoikabili.

Nakala za hukumu Katika hatua nyingine, Kaimu Jaji Mkuu katika hotuba yake ya siku hiyo ya sheria alisema mahakama imedhamiria kutimiza ahadi yake ya kuhakikisha watu wanapata nakala za hukumu ndani ya siku 21 na mwenendo wa shauri ndani ya siku 30 tangu hukumu iliposomwa.

“Wananchi wanastahili kupata nakala za hukumu kwa wakati. Sheria inataka kila Jaji au Hakimu asome hukumu ndani ya siku 90 tangu kesi ilipomalizika kusikilizwa,” alisisitiza Kaimu Jaji Mkuu. Matumizi ya Tehama Kaimu Jaji Mkuu pia alitilia mkazo mahakama kujielekeza katika matumizi ya Teknolojia ya Mawasiliano (Tehama) ili kurahisisha kazi zake.

“Ifikapo Desemba 2018, kulingana na ramani (Road map) ya matumizi ya Tehama, kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (E-Govt Agency), tumedhamiria tuweze kuanza matumizi kamili ya Tehama kwenye kazi za kimahakama na kiutawala,” alisema Jaji Juma.

Aliongeza kuwa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kisasa ya mahakama pia unaenda sanjari na matumizi ya hatua kwa hatua ya Tehama na kwamba wanahakikisha taratibu za masuala ya fedha yanaendeshwa kwa kutumia Tehama kwa ngazi zote, makao makuu hadi wilayani.

Alisema mfumo wa ukusanyaji wa Takwimu za Mashauri (JSDS) kwa kuitumia Tehama utaboreshwa na kwamba mahakama itaangalia hadi inavyoweza kurahisisha mawasiliano kwa kutumia simu za mkononi ili kuleta mabadiliko ya utendaji kazi wenye tija.

Naye, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria aliitaka mahakama kukamilisha mapema mashauri ya jinai, rushwa na uhujumu uchumi.

Umuhimu siku ya sheria Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini hutumika kama njia mojawapo ya kukutana na wadau ili kupata maoni mbalimbali katika kuboresha shughuli ya mahakama huku na yenyewe ikitumia siku hiyo kujitathmini na kuona wapi imepwaya na kufanya maboresho katika suala zima la utoaji haki nchini.

Siku hiyo huadhimishwa ndani ya wiki ya kwanza ya mwezi Februari kila mwaka. Siku hii huashiria mwanzo wa shughuli za mahakama kwa mwaka husika ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Umuhimu wa Utoaji Haki kwa wakati kuwezesha Ukuaji wa Uchumi.’

Kaulimbiu hii ina maana ya kuwa kukamilishwa mapema kwa mashauri ya jinai, rushwa na uhujumu uchumi ni kuendeleza amani na usalama katika jamii na hivyo kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi. Kwa mara ya kwanza, siku hii iliadhimisha mwaka 1997.

Mapema kabla ya hapo, yaani Machi 1, 1996 kulifanyika ibada maalum ya kuwaombea majaji na mahakimu ili wasikilize vyema mashauri yote na hasa ya uchaguzi mkuu wa vyama vingi uliofanyika kwa mara ya kwanza mwaka1995. Ilikuwa ni mwaka 2007 pale sherehe za Siku ya Sheria nchini zilipohudhuriwa kwa mara ya kwanza na Rais ambapo alipata nafasi ya kutoa hotuba na huu ndio ulikuwa mwanzo wa mgeni rasmi kutoa hotuba.

Kwa mwaka huu, siku ya sheria iliadhimishwa rasmi tarehe 2, Februari ambapo kila mkoa uliadhimisha kivyake. Sherehe za kilele cha Siku ya Sheria nchini zilitanguliwa na Maonesho ya Wiki ya Sheria yaliyoanza rasmi Januari, 28 hadi Februari 1. Maonesho ya Wiki ya Sheria yalifanyika nchi nzima lengo kuu likiwa ni kutoa elimu ya Sheria kwa wananchi juu ya huduma na taratibu mbalimbali za kisheria na mahakama.

Kwa upande wa Dar es Salaam, maonesho haya yalifanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja na kushirikisha wadau mbalimbali huku mahakama ikiwa mwenyeji.

Wadau hao ni Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mahakama Kuu Zanzibar, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Mahakama (AGC), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Mkemia Mkuu wa Serikali, Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Mkuu wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu Huria na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Wengine ni Tume ya Kurekebisha Sheria, Taasisi zinazotoa msaada wa Kisheria (Legal Aid), Taasisi ya Kuzuia, kupambana na kudhibiti tushwa (Takukuru), Polisi, Magereza, Msajili, Mabaraza ya Ardhi na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Maonesho hayo pia yalishirikisha Tume ya Kurekebisha Sheria, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Sekretarieti ya Msaada wa Sheria, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), ‘Tanzania Network of Legal Aid Provider (Tanlaps),’ Chama cha Msada wa Kisheria (LAHC) na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).

Katika maonesho hayo kulikuwa na uwakilishi wa ngazi zote za mahakama kuanzia mahakama za mwanzo hadi mahakama ya Rufaa ambapo taratibu na huduma mbalimbali za kimahakama zilitolewa kwa wananchi waliopata fursa ya kutembelea mabanda ya maonesho hayo.