Kuwa gerezani hakuondoi haki ya mtoto

UDHALILISHAJI au unyanyasaji wa mtoto ni aina yoyote ya matendo mabaya au kutotoa matunzo, kunakosababisha madhara ya mwili, maadili au hisia kwa mtoto.

Chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Mtoto, udhalilishaji/ unyanyasaji wa mtoto unatafsiriwa kuwa ni kukiuka haki za mtoto kunakosababisha madhara ya kimwili, kimaadili, kihisia ikiwemo kumpiga, kumtukana, kumbagua, kumtelekeza, kumnajisi kingono na kumnyonya kwa kumtumikisha.

Watoto wanaokinzana na sheria ni mtu yeyote aliye chini ya miaka 18 ambaye atatenda kosa la jinai na hivyo kukumbana na mkono wa sheria. Watoto waliofungwa ni watoto walionyimwa uhuru ikiwa ni aina ya kizuizi au kifungo au mtoto kuwekwa katika sehemu ya umma au binafsi kwa amri ya mahakama, utawala au mamlaka nyingine ambapo hataruhusiwa kuondoka apendavyo.

Hiyo ni tafsiri kwa mujibu wa Ibara ya 11 ya Kanuni za Umoja wa Mataifa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Walionyimwa Uhuru. Jeshi la Magereza sasa linatekeleza Sera ya Ulinzi wa Mtoto ambayo inaonesha taratibu za kufuata kukidhi matakwa ya kuwalinda watoto walioko chini ya kizuizi.

Maandalizi ya sera hii yalianza katika utawala wa Kamishna Jenerali wa jeshi hilo, John Minja ambaye sasa amestaafu. Kamishina aliyepo sasa ni Juma Malewa. Malewa anasema sera hii itasaidia wafanyakazi wote wa jeshi hilo kujenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu na zaidi kuhakikisha masuala ya ulinzi wa watoto yanazingatiwa.

“Tuna imani kuwa sera hii na taratibu zake zimeweka mwongozo mzuri katika kulinda na kuimarisha ulinzi wa mtoto magerezani,” anasema Malewa. Madhumuni ya sera ni kuweka mazingira salama kwa watoto wanapokuwa chini ya uangalizi wa jeshi.

Sera hiyo inaeleza ni nini maana ya ulinzi wa mtoto na jinsi ambavyo askari na watumishi wengine wanapaswa kumtendea mtoto kuhakikisha ulinzi wa mtoto.

“Jeshi la magereza limedhamiria kuhakikisha kwamba maslahi bora ya mtoto katika magereza yanalindwa na kukuzwa ili kutoa ulinzi kwa mtoto dhidi ya madhara yoyote. “Ustawi wa watoto ni kipaumbele muhimu na ni jukumu la kila mtu katika jeshi letu kuhakikisha kuwa haki za mtoto zinalindwa na kuchukuliwa hatua za haraka na stahiki kwa mtu atakaezivunja,” anasema.

Jeshi hili ni taasisi mama ya urekebishaji wa wafungwa. Limeanzishwa chini ya Ibara ya 147 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.

Kwa kuwa kuna watoto ambao huwekwa chini ya uangalizi wa magereza, jeshi hilo lina wajibu sawa na ule wa Kamishna wa Ustawi wa Jamii kuhakikisha kuwa kunakuwa na sera ya ulinzi wa watoto na taratibu za kufuata endapo ukiukaji wa haki za mtoto unatokea magerezani.

Chini ya kanuni ya 53 ya Kanuni za Sheria ya Mtoto G.N Na. 151 ya mwaka 2012, kuna jukumu la kuweka sera ya ulinzi wa mtoto na taratibu zake. Kamishna Malewa anasema jukumu hili ni la Kamishna wa Ustawi wa Jamii kwa kuwa watoto wanaokuwa kizuizini wakisubiri kesi zao kumalizika wanakuwa katika makazi ya kizuizi yaliyoko chini yake.

Anasema mara mtoto anapopatikana na hatia katika kosa ambalo kama lingefanywa na mtu mzima adhabu yake ingekuwa ni kifungo, mahakama inapaswa kutoa amri kuwa mtoto huyo awekwe katika kifungo katika Shule za Maadilisho au Shule zilizoidhinishwa.

Suala hilo limeainishwa katika Sheria 3 ya Mtoto kifungu cha 20 ili kuhakikisha kuwa mtoto huyo anapata haki zake, ikiwa ni pamoja na kupata elimu na malezi.

“Kwa hiyo basi, jukumu la msingi la kutunza watoto waliokinzana na sheria limewekwa chini ya Shule za Maadilisho. Kwa kuwa kuna watoto ambao huwekwa chini ya uangalizi wa magereza,” anasema.

Madhumuni ya kuwa na sera ni kuimarisha na kukuza utendaji bora kwa kuweka viwango bora vya utendaji kazi katika ulinzi wa watoto na hivyo kuweka mazingira salama kwa watoto wanapokuwa chini ya uangalizi wa Jeshi.

Madhumuni mahususi ya sera ni kutoa ulinzi na kuhakikisha usalama unaohitajika kwa watoto walio chini ya magereza, kuchukua hatua stahiki ambazo zitawezesha kuchangia na kuimarisha jitihada ya kuboresha mazingira ya mtoto aliyepoteza uhuru wake kutokana na kuwekwa magereza.

“Nyingine ni kuzuia matukio yoyote ya udhalilishaji au unyanyasaji wa watoto yakiwemo yale yanayofanywa kati ya mtoto na mtoto au kati ya mtoto na mtu mzima katika magereza,” anasema Malewa.

Aidha, sera hiyo pia ina lengo la kutoa mwongozo kwa askari na watumishi wengine wa Jeshi katika kutoa uamuzi sahihi kuhusu jambo lolote linalohusu ulinzi wa mtoto, kuweka utaratibu wa uwazi, wa haki na wenye usalama wa namna ya kutoa taarifa inapotokea matukio ya aina yoyote ya udhalilishaji au unyanyasaji wa mtoto.

Malewa anasema sababu ny ingine ni kuweka utaratibu unaoonesha hatua kwa hatua jinsi malalamiko na matukio yanayoathiri ulinzi wa mtoto yanavyoweza kushughulikiwa. Kuna aina nne za udhalilishaji/unyanyasaji wa mtoto. Nazo ni udhalilishaji wa kimwili, kingono, kihisia na utelekezaji.

Udhalilishaji wa kimwili hufanywa kwa kusababisha madhara ya kimwili kwa mtoto kama vile kumpiga, kumtingisha, kumchoma, kumtilia sumu, kumfinya, kumzamisha katika maji, kumnyonga, kumpa mtoto kilevi au dawa ya kulevya au kumsababishia mtoto ugonjwa au aina yoyote ya madhara ya kimwili.

“Udhalilishaji wa kingono ni mtu anapotumia watoto katika kutimiza haja zake za ngono, inaweza kuwa kwa njia ya kukutana kimwili na mtoto mfano, kufanya ngono, kumtomasa, kutoa maneno yanayoashiria ngono au kumwonesha mtoto picha za ngono,” anasema Malewa.

Udhalilishaji wa kihisia anasema kuwa ni kitendo ambacho anafanyiwa mtoto kwa muda mrefu cha kuumiza hisia zake ambayo yaweza kusababisha madhara makubwa na ya kudumu kwa maendeleo ya mtoto kihisia au kumzuia mtoto asishiriki katika mahusiano ya kawaida ya kijamii.

“Haya yote yaweza kumsababishia mtoto kuwa mwoga au kujihisi kuwa wakati wowote anaweza kugombezwa, au kutishiwa na hivyo kuwa na woga na wasiwasi wakati wote,” anasema Malewa. Anasema hiyo ni pamoja na kumwita mtoto majina mabaya au kumzodoa kitendo kinachofanywa na mtu mzima au mtoto mwenzie.

Kutelekeza ni endapo watu wazima wanaacha kumtimizia mtoto mahitaji yake muhimu kiasi kwamba huweza kumsababishia mtoto madhara katika afya yake na makuzi yake. “Na hii ni mfano kushindwa kumpa chakula cha kumtosha, sehemu ya kuishi, au kushindwa kumlinda dhidi ya madhara ya kimwili au hatari nyingine, kushindwa kumpatia dawa au matibabu pindi anapohitaji,” anasema.

Kamishna Malewa anasema vitendo hivyo vyote hutokea mara nyingi katika mahusiano ya karibu kwa mtu aliyeaminiwa au mwenye jukumu la kumtunza mtoto na inapotokea huwa ni kosa la kutumia madaraka vibaya na kuvunja uaminifu.

Haki za watoto zinalindwa kikamilifu katika mikataba mbalimbali ya kimataifa, kikanda na sheria za nchi ambazo ni pamoja na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto wa mwaka 1990, Kanuni za Umoja wa Mataifa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Walionyimwa Uhuru za mwaka 1990 (Kanuni za Havana).

Kanuni za Umoja wa Mataifa za Maadili kwa Wasimamizi wa Sheria za mwaka 1979, Kanuni za Viwango vya Chini juu ya Adhabu zisizo za vifungo za Umoja wa Mataifa za mwaka 1990. Mwongozo wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Kuzuia Makosa kwa Vijana wa mwaka 1990 (Mwongozo wa Riyath), Orodha ya Kanuni kwa ajili ya Ulinzi ya Watu wote walioko katika vizuizi vya aina yoyote au kifungo ya mwaka 1988.

Kanuni za viwango vya chini kuhusu matunzo ya wafungwa za mwaka, 1955 (Kanuni za Mandela) na Kanuni za Umoja wa Mataifa za Matunzo ya wafungwa wa Kike na Adhabu zisizo za Vifungo kwa Wahalifu wa Kike za mwaka 2010 (Kanuni za Bangkok).

Zaidi ya nyaraka hizo za kisheria, askari wa magereza wanapaswa pia kuheshimu sheria za nchi kama vile Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na kanuni zake.

Ibara ya 3(2) ya Mkataba wa Haki za Mtoto inasema, “nchi wanachama zimedhamiria kuhakikisha ulinzi na matunzo kwa mtoto ikiwa ni jambo muhimu sana kwa makuzi yake, na kwa kuzingatia haki na wajibu wa wazazi wake, walezi wake au watu wengine ambao wanawajibika kisheria kwa mtoto huyo, na kwa kutimiza hili zitachukua hatua stahiki za kisheria na kiutawala.”

Ibara ya 19(1) ya mkataba huo pia inasema: “Nchi wanachama zitachukua hatua stahiki za kisheria, kiutawala, kijamii na kielimu ili kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vyovyote vya ukatili wa kimwili au kiakili, madhara, udhalilishaji, kutengwa au kutomjali au kumnyonya, ikiwa ni pamoja na udhalilishaji wa kingono, akiwa chini ya uangalizi wa wazazi, walezi au mtu yeyote ambaye anamtunza mtoto huyo.”