Matumizi dawa za maumivu kupindukia yanaua figo

FIGO ni kiungo katika mwili wa binadamu kilichoko ubavuni kwa upande wa nyuma, kushoto na kulia.

Kila binadamu ana figo mbili ingawa kwa mujibu wa Daktari bingwa wa magonjwa ya figo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Jonathan Mgumi, hutokea mtu akawa na moja au akawa na zaidi ya mbili.

“Tulivyojaaliwa na Mungu, kila figo inafanya kazi robo tu, yaani asilimia 25 kila figo inakutosheleza, asilimia nyingine 75 zimepumzika kama unazo mbili, lakini kama una figo moja ina maana itafanya kazi asilimia hamsini na asilimia hamsini iliyobaki haina kazi,” anasema Dk Mgumi.

Daktari huyu bingwa wa magonjwa ya figo anasema figo ikiwa moja, ina uwezo wa kufanya kazi sawa na zinapokuwa mbili. “Ndiyo maana tunahimiza watu kuchangia figo kwa sababu ukibaki na figo moja, ina uwezo wa kufanya kazi yake kama kawaida zikiwa mbili,” anasema Dk Mgumi.

Anasema kabla ya mtu kuchangia figo, hutakiwa kuwa amepita kwenye vipimo mbalimbali kuhakikisha kwamba atakayobaki nayo itakuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa muda mrefu labda itokee tatizo. Ukubwa wa figo ni sawa na ngumi ya mtu na ikitokea ni kubwa au ndogo kuliko ngumi, humaanisha lipo tatizo.

“Figo inaanza kufanya kazi tumboni kabla mtoto hajazaliwa. Mtoto anakojoa tumboni, ndio maana akizaliwa ndani ya saa 48 anatakiwa awe amekojoa, asipokojoa kuna tatizo, figo inatakiwa baada ya kuzaliwa iongezeke na mwisho kulingana na ngumi,” anasema.

Kazi za figo ni pamoja na kutoa taka sumu mwilini kwa njia ya mkojo, kutoa maji yaliyozidi mwilini, kuhakikisha uwiano wa shinikizo la damu mwilini, kutengeneza damu na kuweka madini mwilini katika uwiano mzuri, kutoa afya ya mifupa. Kwa kawaida, figo huchuja maji mwilini lita zaidi ya mililita 125 kwa dakika moja.

Lakini itakapokuwa na shida, itapungua uwezo wa kufanya kazi kwa zaidi ya asilimia 75 ya asilimia hizo. Inapobainika kwamba mtu ana tatizo la figo, ina maana uwezo wa kiungo hiki muhimu mwilini umepungua kwa asilimia 75. Hii hutokea katika hatua za mwisho za ugonjwa huo.

Kitaalamu, inaelezwa kwamba tatizo la figo inaweza kusababisha muathirika kupata tatizo la akili na kwa wanaume hupungua nguvu za kiume. Dk Mgumi anasema zipo hatua tano kabla ya figo kushindwa kufanya kazi. Katika hatua ya kwanza mpaka ya tatu, dalili haziwezi kuonekana hadi hapo anapokuwa hatua ya nne na tano.

Katika hatua ya kwanza hadi ya tatu, figo huwa bado ina uwezo wa kufanya kazi. “Katika hatua za mwanzo, ugonjwa unakuwa kimya kabisa, ndio maana tunashauri kuangalia afya ya figo angalau mara mbili kwa mwaka kwa kupima mkojo na vipimo vingine vya figo,” Dk Mgumi anasisitiza.

Anasema mgonjwa anakwenda hospitali akiwa katika hatua hizo mbili za mwisho, ataonesha dalili ambazo baadhi siyo maalumu. Dalili ambazo si maalumu ni kama vile kuchoka, kupungukiwa damu, kichefuchefu, kuwashwa mwili baada ya kujaa sumu, kuchanganyikiwa na mwili kujaa maji (mwili kuvimba).

Nyingine ni kupungua kwa kiwango cha mkojo na wengine kukosa kabisa, kuvunjika mifupa. “Unaweza kupata tatizo la kuvunjika mifupa na hiyo ni kwa sababu ya udhaifu,” anasema Dk Jonathan.

Aidha, figo inatumika katika kutengeneza vichocheo mbalimbali hivyo ni rahisi mtu mwenye matatizo ya figo kuwa na tatizo la kupungukiwa nguvu za kiume, kupata shinikizo la damu na kupungukiwa na madini hususani calcium.

Daktari huyo bingwa anasema mgonjwa mwenye tatizo la figo akifika hospitali lalamiko kubwa huwa ni la kuumwa mifupa au kuvunjika baada ya mifupa kuwa dhaifu kwa sababu madini yanayotengenezwa na figo hayatengenezwi vizuri. Figo husaidia pia kufanya sukari ya mwili isiwe sawa baada ya kutoa kiwango cha sukari kilichozidi mwilini.

“Kuna dawa ambazo figo inazitoa mwilini baada ya kutumika, ndio maana katika matumizi ya dawa mtu anatakiwa kupewa kwa kiwango kinachostahili,” anasema. Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo na Mkuu wa Kitengo cha Figo, Jacqueline Shoo anasema visababishi vya magonjwa sugu ya figo viko katika makundi mbalimbali kama vile vinayotokana na maambukizi.

Anasema mgonjwa anaweza kuwa na wadudu kwenye mwili wake ambao wanasababisha hitilafu kwenye mifumo mbalimbali ikiwemo utendaji kazi wa figo. Anatoa mfano wa virusi vya homa ya ini (Hepatitis B na C), Ukimwi, maambukizi ya athari za malaria na magonjwa ya ndani ya figo ambayo huharibu chujio la figo.

“Chujio la figo likiwa na hitilafu linasababisha protini kutoka nyingi kwenye mkojo hasa kwa watoto au anazaliwa nalo, linaendelea na kuonekana katika utu uzima, likikaa kwa muda mrefu na hasa chujio lisipopokea matibabu baada ya muda itasababisha ugonjwa sugu wa figo,” anasema Dk Shoo.

Anasema tatizo la chujio linaweza kumpata mtu yeyote na katika umri wowote bila kujali kuwa ni mtoto au mtu mzima. Hupata pia matatizo ya mfumo wa njia ya mkojo ambao husababisha mkojo kuziba kutokana na uvimbe, jiwe, tezi dume zilizozidi ukubwa au kujikunja mrija kwa sababu yoyote ile.

“Yaani mkojo unatakiwa utengenezwe, ushuke uje kwenye kibofu kisha utoke nje, ikitokea tatizo hapo figo linaathirika,” anasema Dk Shoo. Aidha anasema kundi jingine ni wale ambao wanapata tatizo la figo kutokana na matumizi ya dawa kama vile za maumivu kwa muda mrefu, dawa za jamii ya diclofenac na za kienyeji zisizo na vipimo maalumu.

“Tumepata wagonjwa wengi sana ambao wametumia dawa hizo za kienyeji baadaye figo zimeshindwa kufanya kazi yake, hujui amekunywa kiasi gani, hujui zimetengenezwa na miti gani,” anasema Dk Shoo. Anasema watu wengi ambao figo zao zimeathirika zimesababishwa na magonjwa ya sukari na shinikizo la damu.

“Hii ina maana kwamba wagonjwa wengi ambao wana tatizo la figo ni kutokana na magonjwa ya sukari, shinikizo la damu au vyote,” anasema Dk Shoo. Anasema sukari ambayo haiko chini ya uangalizi mzuri kwa kutotumia dawa au kutumia dawa tofauti na maelekezo ya wataalamu, haiwi katika uwiano mzuri inapanda na kushuka.

Dk Shoo anasema kuna magonjwa ya ghafla ya figo ambayo mgonjwa sasa anaweza kuwa hana tatizo la figo lakini baada ya siku moja akawa nalo. “Kwa mfano magonjwa ya kuharisha, mzazi amepoteza damu nyingi wakati wa kujifungua, damu inayoenda kwenye figo inapungua inashindwa kufanya kazi yake vizuri na sumu inashindwa kutolewa,” anasema.

Mgonjwa mwenye tatizo la figo la ghafla atatambulika kwa kulinganisha vipimo vya sumu mwilini kwa jana yake na siku moja baadaye. Magonjwa mengine yanayoweza kuchangia tatizo ni malaria kali, magonjwa ya mfumo wa mkojo na kuziba njia ya mkojo.

Daktari mwingine bingwa wa magonjwa ya figo, Muhidin Mahmoud anasema utafiti uliofanywa mwaka 2010 na Shirika la Kimataifa la Magonjwa ya Figo, asilimia 10 ya watu wana ugonjwa huo. Aidha taarifa ya mwaka 1990 inaonesha magonjwa ya figo yanashika nafasi ya 27 na kwa mwaka 2010 yamepanda na kushika nafasi ya 18 kwa kusababisha vifo.

Takwimu hizo za kidunia zinaonesha ni asilimia 10 pekee ambayo inapata huduma ya kusafisha damu kwa mashine na kupandikiza figo huku asilimia 90 hawapati huduma. Dk Mgumi ambaye yupo kwenye kitengo cha tiba ya figo, anasema hapa nchini kuna hospitali ambazo zinatoa huduma kwa magonjwa ya figo kwa kusafisha damu.

Nazo ni Muhimbili, KCMC, Hospitali ya Mbeya, Benjamin Mkapa UDOM pamoja na nyingine za taasisi binafsi zilizoko Dar es Salaam.

Wataalamu hawa wa afya wanasema njia pekee ya kuepuka magonjwa hayo ni kula mboga za majani na matunda kwa wingi, kufanya mazoezi angalau nusu saa kila siku, kupima afya mara kwa mara na hasa figo mara mbili kwa mwaka na pia kuepuka chakula na vinywaji vya viwandani.