LIGI KUU: Mwanzo mpya wa soka ya Wanawake

LIGI Kuu ya soka ya wanawake Tanzania Bara ilihitimishwa Machi 10 mwaka huu huku Mlandizi Queens ya Pwani ikitangazwa bingwa wa kwanza wa ligi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Ligi hiyo imefanyika kwa mara ya kwanza nchini, baada ya wadau wa soka la wanawake kulia kwa muda mrefu na hatimaye kilio chao kikasikika.

Mlandizi Queens ambayo haikupoteza mchezo wowote kwenye hatua ya sita bora na kupata pointi 15 ilizichapa timu za JKT Queens ambayo ilimaliza kwenye nafasi ya pili ikiwa na pointi 12 na Kigoma Sisterz iliyomaliza kwenye nafasi ya nne ikiwa na pointi saba lakini vikosi vyake vikiundwa na asilimia kubwa ya wachezaji wa timu ya Taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’.

Mlandizi Queens ilikuwa na wachezaji wa kawaida lakini ilitoa mfungaji bora ambaye ni Mwanahamisi Omar na golikipa bora ambaye ni Janeth Simba. Timu yenye nidhamu ilikwenda kwa Panama FC ya Iringa licha ya kufungwa michezo yote lakini ilionesha nidhamu ya hali ya juu kuanzia benchi la ufundi mpaka wachezaji wake.

Mlandizi Queens pamoja na kutangazwa bingwa wa kihistoria ilipatiwa Sh milioni tano, kombe na medali za dhahabu, huku mshindi wa pili na wa tatu wakipata medali za fedha na shaba. Kocha Mkuu wa Mlandizi, Hussein Kioma aliwapongeza wachezaji wake kwa kutwaa ubingwa mbele ya timu zilizosheheni wachezaji wazoefu na wakongwe kwenye ligi ya wanawake.

“Kuwa bingwa kwa kwanza wa Ligi Kuu ya wanawake ni zawadi kwa mkoa wa Pwani pamoja na viongozi wote kwani walitupa sapoti ya kutosha tangu mwanzo hadi mwisho,” alisema Kioma. Ligi hiyo haikuwa na mdhamini zaidi ya Azam walionunua haki za matangazo ambapo fedha yao ndiyo iliyotumika kuendesha ligi hiyo.

Mwenyekiti wa chama cha soka la wanawake Tanzania (TWFA), Amina Karuma anasema changamoto za kuendesha ligi hiyo zilikuwa kubwa lakini anashukuru na kamati yake kwa kumudu kuiendesha.

“Tunashukuru ligi imekwisha salama, changamoto zilikuwa nyingi mno, nawashukuru pia wanakamati wenzangu pamoja na viongozi wa mikoa kwa ushurikiano wao, kikubwa ni kuzidisha ushirikiano ili ligi yetu ijayo iwe bora zaidi,” anasema.

“Nafurahi ligi kufika tamati na bingwa kupatikana kwani ni moja ya malengo yangu niliyojiwekea kwa kipindi cha miaka miwili ambayo nimekaa madarakani,” anasema Karuma. Aidha Mwenyekiti huyo analipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuwapa ushirikiano wa bega kwa bega kufanikisha ligi hiyo.

“TFF haikutuacha imekuwa ikitupa mwongozo wa nini cha kufanya mwanzo mpaka mwisho wa ligi hiyo hasa kwa vile tumeandaa ligi ya wanawake kwa mara ya kwanza,” anasema. Ligi ya wanawake ilishirikisha timu 12 zilizogawanywa makundi mawili yenye timu sita kila moja ambapo timu tatu za juu kutoka kila kundi zilicheza ligi ya sita bora ambapo timu yenye pointi nyingi ndiyo iliyoibuka bingwa.

“Mwanzo siku zote huwa mgumu, naamini ligi yetu ya msimu ujao haitakuwa kama hivyi, itakuwa bora zaidi,” anasema Karuma.

Waamuzi na Makamisaa

Katika kudhihirisha kuwa ni Ligi Kuu ya wanawake hatua ya sita bora ilichezeshwa na waamuzi wanawake pamoja na makamisaa wanawake.

Kuchezeshwa kwa waamuzi wanawake ilidhihirisha kuwa wanawake katika soka wako mbele na ni mfano wa kuigwa kwani hakuna malalamiko wala timu iliyokata rufaa ikipinga maamuzi au kuonewa. Ni nadra kuona kwenye soka timu zikimaliza dakika 90 bila kulalamika kuonewa au timu fulani kubebwa, hivyo kwenye soka la wanawake inawezekana bila lawama.

Maandalizi ya timu

Asilimia kubwa ya timu hazikujiandaa vya kutosha kuingia kwenye ligi yenye ushindani na hii ilitokana na mikoa kutokuwa na uzoefu wa kuandaa ligi ya wanawake.

Nasema hivyo kwa sababu timu ya Victoria Women ya Kagera haikumudu kusafiri kucheza kwenye mikoa mingine kutokana na ukata, hivyo kufanya timu zingine kupata ushindi wa mezani na kuondoa ushindani halisi ambao unapatikana kwenye dakika 90.

Ukata kwenye timu pia ulitokana na ligi kukosa mdhamini kwani Azam Media ilinunua haki ya kurusha matangazo tu na fedha iliyopatikana ilinunua jezi jozi mbili kwa kila timu, kulipa waamuzi, makamisaa, ulinzi na huduma ya kwanza na wasimamizi wengine huku timu shiriki zikipata fedha kidogo ya kujikimu.

Kwa sababu ligi imeonekana na timu zimeonesha ushindani hasa kwenye hatua ya sita bora ni wakati sasa wa kampuni, mashirika na watu binafsi kutumia fursa hii kujitangaza kupitia soka la wanawake.

Ligi ya kwanza Afrika kuoneshwa mbashara Soka la wanawake linachezwa katika nchi nyingi za Afrika, lakini ligi ya wanawake ya Tanzania inasemekana ndio ligi ya kwanza kuoneshwa mbashara (live) katika nchi za Afrika.

Kuoneshwa kwa ligi kunaweza kuwa fursa ya ajira kwani wachezaji wanaweza kupata timu nje ya nchi kwani soka ni ajira kama zilivyo ajira nyingine. Sitashangaa kusikia wachezaji kadhaa wa Tanzania wanahitajika na timu za nje kwani wapo ambao walionesha vipaji pia itasaidia kuijenga Twiga Stars ambayo inashika nafasi ya nane kwa ubora Afrika.

Mwito

Kwa sababu soka ni ajira wachezaji watumie fursa hii kujitangaza kwa kucheza kandanda safi na kuwa na nidhamu uwanjani na nje ya uwanja.

Wachezaji wengi wa kike wanapenda kuvaa kama wanaume huku wakiiga hata mwendo wa kiume, jambo ambalo ni tofauti na maana ya mchezo huo kwani hata watalaamu wa soka la wanawake timu za Brazil, Ujerumani, Marekani na Nigeria wachezaji wao wanavaa kike.

Utu wa mwanamke ni wa thamani hivyo wachezaji wa kike wa Tanzania wanapaswa kujivunia kuwa mwanamke na kuheshimu kuwa mwanamke. Hili naamini wengi watakubaliana na mimi kwani wachezaji waliosajiliwa JKT Queens wamebadilika na sasa wapo kwenye mwonekano mzuri kama wanawake wengine tofauti na walivyokuwa miaka iliyopita.

Timu za U-20

Ili kuwe na ligi bora na endelevu Chama cha Soka la Wanawake kinatakiwa kuweka kwenye kanuni timu zote zitakazoshiriki ligi kuwa na timu B ili kuinua soka la wanawake. Kwa sababu ndio mwanzo basi msisitizo wa kanuni uanze sasa kusiwepo na visingizio vyovyote kwani itasaidia soka letu kukua na hii tabia ya kugombea wachezaji kufutika.