Upelekaji mawasiliano vijijini na changamoto ya umeme

NISHATI ya umeme ni muhimu kwa maendeleo kwani inahitajika katika masuala mbalimbali ikiwemo viwanda na ukuaji wa sekta mbalimbali.

Pamoja na juhudi zilizofanywa na serikali, bado wananchi wengi vijijini hawajapatiwa nishati hiyo kupitia mradi wa Umeme Vijijini (REA). Hata hivyo, siku hizi si ajabu kupita katika baadhi ya maeneo yasiyo na umeme vijijini na kukuta nyumba zimefungwa taa.

Katika muktadha huo huo, Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) nao aumejikuta unapolazimika kupeleka mawasiliano ya simu katika vijiji ambavyo havina umeme, kulazimika kupeleka pia nishati ya umeme. Mbali na changamoto ya nishati ya umeme, UCSAF pia hukumbana na changamoto ya barabara.

Katika mikoa ya kusini kwa kuanza na Lindi, UCSAF imefikisha mawasiliano katika kata za Barikiwa, Makata, Liwale mjini, wilaya ya Liwale, Mitole, Kiranjeranje, Mandawa wilaya ya Kilwa, Chiponda Lindi vijijini, Namapwia, Kiegei, Kilima Rondo, Mbondo wilaya ya Nachingwea, Matambarale na Namichiga wilaya ya Ruangwa.

Katika mkoa wa Mtwara, kata zilizopata neema hiyo ya mawasiliano kwa juhudi za UCSAF ni za Chiwata, Mkululu, Mpindimbi, Lipumburu na Namatutwe wilaya ya Masasi. Zingine ni Dihimba, Kiromba, Kitaya, Namtumbuka, Njengwa katika wialaya ya Mtwara vijijini na kata ya Sengenya na Mkonona katika wilaya ya Nanyumbu.

Mkoani Ruvuma, kata zilizopata mawasiliano ni Muhukuru, Mahanje, Songea Vijijini, Mbaha, wilaya ya Nyasa, Mpepai na Litumbandyosi katika Wilaya ya Mbinga. Kata zingine ni Magazini, Kitanda, Mchesi, Nalasi, Muhuwesi, Namwinyu, Kalulu, Misechela na Mindu katika wilaya ya Tunduru.

Katika takwimu hizo wananchi 59,886 wanapata mawasiliano katika mkoa wa Lindi wenye vijiji 48 huku mkoani Mtwara kukiwa na wananchi 49,109 waliopatiwa mawasiliano kutoka vijiji 102 na mkoa wa Ruvuma wananchi 121,006 kutoka vijiji 71.

Kati ya vijiji hivyo, vipo ambavyo havina umeme wa gridi ya taifa licha ya kwamba zimejigharimia umeme utokanao na nishati mbadala.

Katika vijiji hivyo ambavyo vimewekwa minara ya mawasiliano na UCSAF na havina umeme, mfuko huo umelazimika pia kutumia umeme jua unaoweza kutoa umeme wakati wote wa hali ya hewa hata kama hakuna jua ili wananchi wapate mawasiliano.

Mlinzi wa mnara wa kijiji cha Kihegehi, Isack Erio anasema minara hiyo mingi ina paneli 24 ikiwa na wati 250 kila moja inayowezesha mawasiliano huku juu ya minara kukiwa na taa kwa ajili ya kuonesha eneo hilo lina mnara kwa ndege zinazoruka.

Anasema vifaa vya umeme jua vilivyowekwa kwenye minara hiyo ni vya gharama kubwa hivyo kuhitaji ulinzi usiku na mchana kwa kupokezana walinzi watatu kwa kila mnara ili kuepuka wezi kuiba vifaa vya umeme jua.

Katika kijiji cha Mbombo, ukipita utakuta baadhi ya nyumba wameunganisha umeme huo wa jua kutoka nyumba moja hadi nyingine pamoja na maduka yao kwa lengo la kuhakikisha wanapata nishati hiyo.

Elias Mkuzi, anasema kutokana na mapato ya kilimo cha korosho wananchi wengi wamekuwa na mwamko wa kununua umeme jua ambao unasaidia kupata mwanga na hata kuchaji simu zao kwa kutumia umeme huo.

“Mimi nina mitambo ya umeme jua yenye uwezo mdogo lakini inanisaidia kujipatia fedha kwa kuchajisha simu za mkononi kwani baada ya kuanza kupata mawasiliano watu wengi wamenunua simu lakini hawana maeneo ya kuchaji simu zao za mkononi,” anasema Mkuzi.

Anasema hutoza Sh 200 hadi 500 kuchaji simu kutokana na hali ya hewa ya siku hiyo na kwamba kuna watu wengi katika kijiji hicho wanaofanya biashara hiyo. Anayahimiza makampuni yanayouza vifaa vya umeme jua kutoka mijini na kwenda vijijini ambako ndiko kuna uhitaji mkubwa.

“Katika mikoa ya Kusini inafahamika kuna mazao ya msimu na husimamiwa na vyama vya ushirika. Wanaweza kuja kuuza vifaa vya umeme jua kwa kuzungumza na wanaohitaji na kuandikisha majina na kupewa vifaa hivyo ili wakatwe wakati wa mauzo,” anasema.

Naye Mohamed Salum anasema umeme wa jua umekuwa mkombozi katika vijiji vyao kutokana na kutumika kwenye minara iliyofungwa pamoja na kuchaji simu. Anasema kwa sasa giza hakuna katika vijiji vyao hivyo kusaidia katika kuimarisha usalama na kuwasiliana kutokana na kuwekwa kwa minara katika kila eneo ambalo awali kulikuwa hakuna mnara.

Anasema ingawa wanasubiri kufungiwa umeme wa REA, lakini umeme jua umekuwa mkombozi wao katika kipindi hiki cha kusubiri. Anasema walinzi wanaolinda minara hiyo wamekuwa wakilipwa na kampuni zinazotoa huduma ili kuepuka kudanganyika na kuuza vifaa hivyo ambavyo ni vya gharama kubwa.

Fundi Mitambo wa kampuni ya Sincro Site Watch inayosimamia minara inayotoa huduma za kampuni ya Tigo, Gratian Kasenene anasema minara inayotumia umeme jua ni gharama nafuu kuliko kuliko ile inayotumia umeme wa jenereta.

Mkazi wa kijiji hicho, Thomas Julius anasema wamekuwa wakitozwa Sh 200 hadi 300 kwa kuchaji simu moja katika umeme jua, hivyo kuwagharimu fedha nyingi kwani kuna simu ni lazima kuchaji kila baada ya siku moja au mbili.

Lakini anasema wanashukuru kwa mawasiliano kufika katika kijiji hicho na kuwezesha wenye umeme jua kuongeza vipato vyao na kuongeza mwamko kwa wengi zaidi kununua vifaa vya umeme huo hata kama vina uwezo wa kuwasha taa tu na kuchaji simu zao.

Mkazi wa kijiji cha Chidya wilayani Masasi, Thecla Evance anaeleza umuhimu wa umeme jua katika maisha yao kuwa ukinunua kwa mara moja hakuna gharama nyingine tofauti na ule wa kulipa kila wakati.

Anawataka wakazi wa mikoa ya kusini kuchangamkia kununu vifaa vya umeme jua ili kujiletea maendelea kwa kuwa na uhakika wa mawasiliano huku nyumbani mwao wakiachana na vibatari ambavyo ni vigumu hata watoto kujisomea usiku.