Kifua kikuu bado tishio kwenye maeneo yenye msongamano

Kifua Kikuu (TB) unatajwa kuwa ugonjwa wa tatu baada ya malaria na Ukimwi kwa kusababisha vifo vya watu wazima wengi hapa nchini.

Kila mwaka wastani wa wagonjwa 62,000 hugundulika kuwa na TB nchini, hali ambayo imechangiwa na maambukizo ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi (VVU). Wanaume wanaelezwa kwamba huathirika zaidi wakilinganishwa na wanawake.

KWA mujibu wa Dk Allan Tarimo wa Kitengo wa Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP), idadi ya wagonjwa ni ndogo kulingana na wagonjwa wapya 160,000 wanaotakiwa kuibuliwa kila mwaka. Idadi hiyo ni kulingana na utafiti zilizofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Dar es Salaam hutoa robo ya wagonjwa wapya na kuongoza kwa maambukizi mapya ya kifua kikuu kila mwaka,” Dk Tarimo aliongeza. Watu wanaoathirika zaidi na ugonjwa huo ni wenye umri kati ya miaka 15 – 45 ambao ni nguvu kazi ya taifa.

Wagonjwa wa TB wanapatikana katika mikoa na wilaya zote nchini kwa viwango tofauti. Kifua kikuu huambukiza na kuenea kwa njia ya hewa. Mgonjwa wa kifua kikuu cha mapafu ambaye hajagundulika na kuanza dawa ni hatari kwa watu wengine kwa sababu huambukiza mtu mmoja hadi mwingine.

Wakati mgonjwa wa kifua kikuu anapokohoa, kupiga chafya, kucheka, kuimba au kuongea, vimelea vya ugonjwa husambaa hewani na hivyo mtu mwingine akivuta hewa hiyo, huambukizwa. Dk Tarimo anaongeza kuwa kuna mambo kadhaa yanayochangia kuenea kwa kifua kikuu miongoni mwa wanajamii.

Mambo hayo anasema ni pamoja na msongamano katika nyumba za kuishi na maeneo mengine ya mikusanyiko yasiyo na mzunguko wa hewa safi ya kutosha yakiwemo maeneo ya vilabu vya pombe, sokoni na vyumba katika maeneo kama Manzese, Tandale na nyinginezo.

Pia anasema umasikini katika jamii husababisha watu kukosa mahitaji muhimu hata kusababisha changamoto za maambukizi ya kifua kikuu.

Kimsingi, anasema ugonjwa huo unaathiri zaidi jamii maskini. Daktari huyo anasema kushuka kwa kinga ya mwili kwa mfano hutokana na kuugua magonjwa kama Ukimwi, saratani na kisukari au kutokana na uzee, umri chini ya miaka mitano, lishe duni huchangia mtu kuugua kifua kikuu.

Kifua kikuu hujitokeza katika aina mbili. Kwanza ni kifua kikuu cha mapafu na nyingine ni ile nje ya mapafu. Kifua kikuu cha mapafu hushambulia mapafu. Wakati ile ya nje ya mapafu hushambulia viungo vingine kama tezi, tumbo, moyo, ubongo na uti wa mgongo.

Kifua kikuu nje ya mapafu hujitokeza zaidi kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (WAVIU) kutokana na kuporomoka kwa kinga ya mwili. Ugonjwa huo hujitokeza kwa dalili mbalimbali kutegemea vimelea vya kifua kikuu vinashambulia sehemu gani ya mwili.

Dalili kuu za kifua kikuu cha mapafu ni pamoja na kikohozi cha muda mrefu kuanzia wiki mbili na kuendelea. Mgonjwa hutoa makohozi na wakati mwingine yaliyochanganyika na damu. Dalili nyingine ni kupungua uzito wa mwili au kukonda, homa za mara kwa mara, kutoka jasho jingi hasa wakati wa usiku hata kama hali ya hewa ni ya baridi.

Wakati dalili za kifua kikuu nje ya mapafu zinategemea kiungo kilichoathirika kwa mfano uvimbe wa tezi za shingo, kuumwa kichwa na kupoteza fahamu kwa mtu mwenye kifua kikuu cha ubongo na kuwa na nundu au uvimbe mgongoni kwa mtu mwenye kifua kikuu cha uti wa mgongo.

Dalili zilizotajwa hapo juu zikiwepo zinaweza kusaidia wataalamu kupata picha juu ya uwezekano wa mgonjwa kuwa na TB. Mgonjwa huagizwa na mtaalamu kuleta makohozi kwa ajili ya kipimo cha maabara. Hivyo vimelea vikionekana kwenye darubini, mgonjwa huyo huthibitishwa kuwa na TB ya mapafu.

TB nje ya mapafu huthibitishwa kwa vipimo mbalimbali kulingana na sehemu iliyoathirika. Kipimo cha picha (X-Ray) kinaweza kutumika pia kuthibitisha ugonjwa wa kifua kikuu. Mtu mwenye ugonjwa wa kifua kikuu hawezi kufanya kazi hivyo husababisha kushuka kwa kipato cha familia na kuongezeka kwa umasikini.

Pia hukumbana na kunyanyapaliwa na familia, rafiki na jamii na hivyo kuathirika kisaikolojia. Vilevile, hupata ulemavu wa viungo kama vile kupooza na utaahira kwa watoto kabla ya kukutana na kifo ikiwa atachelewa matibabu.

Jamii huathirika kutokana na kuupungua kwa nguvu kazi hivyo husababisha kushuka kwa uchumi wa jamii pamoja na kuenea kwa TB kwa jamii kwani mtu mmoja mwenye TB isiyogundulika na kutibiwa huambukiza hadi watu 15 kwa mwaka.

Pia kunakuwa na ongezeko kubwa la watoto yatima kutokana na vifo vya wazazi na walezi wao. Ugonjwa wa TB unatibika pale mgonjwa anapogundulika mapema na kupata tiba sahihi. Lengo la matibabu kwa mgonjwa ni kuponya kabisa TB na kuzuia kurudia kuugua kifua kikuu pamoja na kuzuia usugu wa dawa.

Tiba hiyo pia inalenga kuzuia ueneaji wa TB kwenye jamii na kuzuia vifo. Wizara imeweka kanuni za matibabu ili kupambana na ugonjwa wa TB. Kanuni hizo ni pamoja na kugundua TB mapema na kuanza matibabu mapema pamoja na kutumia dawa mseto kwa muda uliopangwa.

Pia kutumia kiwango sahihi cha dawa, kumaliza matibabu kwa wakati mwafaka, kunywa dawa chini ya muangalizi anayekubaliwa na mgonjwa na mwisho kupima makohozi mara kwa mara kama mgonjwa atakavyoshauriwa na mtaalamu. Tiba ya TB huchukua miezi sita kwa wagonjwa wapya na minane kwa wagonjwa wanaorudia matibabu.

Ugonjwa huu hutibiwa na dawa mseto. Dawa hizo mseto hutumika katika vipindi tofauti vya tiba ya mgonjwa. Mgonjwa anatakiwa kumeza dawa zote chini ya usimamizi wa msaidizi aliyemchagua yeye mwenyewe. Msimamizi huyo anawajibika kuwasiliana na watoa huduma kuhusu maendeleo na changamoto za mgonjwa.

Wakati wa kuanza matibabu, mgonjwa hupewa fursa na mtoa huduma kuamua kumeza dawa nyumbani chini ya msimamizi wake au kwenda kila siku kituo cha tiba kilicho karibu yake na kumeza dawa chini ya usimamizi wa mtoa huduma.

Matibabu yamegawanyika katika sehemu mbili ambayo ni kipindi cha matibabu ya awali ambacho ni miezi miwili au mitatu na kipindi cha muendelezo wa matibabu ambacho ni miezi minne au mitano kulingana na aina ya mgonjwa.

Mgonjwa mwenye TB ya mapafu kabla ya kuanza kipindi cha muendelezo wa dawa anatakiwa kupima makohozi kwanza na kama hayatakuwa na vimelea basi mgonjwa ataendelea na dawa za muendelezo na endapo atakuwa na vimelea ataongeza mwezi mmoja zaidi wa matibabu ya awali.

Wagonjwa wengi hawapati matatizo yeyote watumiapo dawa za kutibu TB lakini wakati mwingine dawa hizo huambatana na maudhi madogo madogo. Hata hivyo, wagonjwa wachache sana wanaweza kupata maudhi makubwa ambayo yanaweza kuhatarisha maisha.

Wagonjwa hawa wanatakiwa kwenda haraka sana katika kituo cha tiba kilicho karibu. TB ni ugonjwa unaozuilika kuenea kwa mtu mmoja au kwa jamii endapo mikakati ya kugundua mapema wagonjwa wa TB na kuwapatia matibabu sahihi mapema iwezekanavyo.

Pamoja na kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa au kupiga chafya na kuhakikisha kwamba watu walio karibu na mgonjwa wa TB hususani watoto chini ya miaka mitano, wazee, na wenye magonjwa ya kusendeka (mfano kisukari, saratani, n.k) wanachunguzwa kama wana TB.

Hatua nyingine ni kuelimisha jamii ili kuondokana na tabia ya kuwanyanyapaa wagonjwa wa TB na Ukimwi, kuiwezesha jamii kiuchumi ili kuboresha makazi na lishe na kuihamasisha jamii kuwatambua mapema wenye dalili za TB na kuwasaidia kwenda mapema vituo vya huduma kwa uchunguzi.

Jukumu la kupambana na TB si la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pekee bali ni la wadau wote ikiwa ni pamoja na waliougua na kupona TB, wagonjwa na jamii nzima kwa ujumla. Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. Kutokana na kuanza kwa wiki ya Kifua Kikuu inayofikia kilele Ijumaa, tutakuwa tunawaletea makala mbalimbali za ugonjwa huo kadri tutakavyozitayarisha.