LIGI KUU BARA: Miujiza yahitajika kwa JKT Ruvu

ZIMEBAKI takriban mechi nne kwa kila timu, kumalizika kwa michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Timu zote isipokuwa Yanga na Toto Africans, zimecheza mechi 26 kabla ya mechi za leo. Toto na Yanga zina mechi 25. JKT Ruvu yenye pointi 22, Toto Africans (25) na Majimaji yenye pointi 26 ndizo zilizo kwenye ukanda wa kushuka daraja, lakini hilo halizifanyi Mbao (27) Ruvu Shooting (29), African Lyon na Ndanda zenye pointi 30 kila moja kuwa salama kwenye nafasi zake.

Hii inatokana na uchache wa pointi zilizoachana kuanzia timu iliyo kwenye nafasi ya 10, Ndanda yenye pointi 30 mpaka JKT Ruvu inayoshika mkia katika nafasi ya 16 ikijikusanyia pointi 22 katika mechi zake ilizocheza. Ligi hiyo inaendelea leo na timu karibu zote zitashuka uwanjani, hivyo hivyo lolote linaweza kutokea kwa timu hizo kuanzia nafasi ya 10.

Kwa mechi hizo nne zilizosalia kwa timu, JKT Ruvu inayoshika mkia ikishinda mechi zake zote itajikusanyia pointi 12, na hivyo kufikisha pointi 34, lakini je, wakati yenyewe ikishinda mechi zake, timu zilizo juu yake zitakuwa hazishindi mechi zake?

Ni jambo gumu kwa mazingira ya ligi yalivyo, hivyo kwa kifupi timu hiyo iliyokuwa ikitoa upinzani mkali karibu misimu yote iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu, inahitaji miujiza kujinasuru na kushuka daraja. Kwa upande wa Toto, ikishinda mechi zake tano zilizosalia itafikisha pointi 40, swali ni lile lile je, Majimaji iliyo chini ya Kalimangonga ‘Kally’ Ongalla haitakuwa ikishinda mechi zake?

Bila shaka hapo kuna ugumu lakini kwa vile kwenye mpira lolote linaweza kutokea, Toto inaweza kubaki Ligi Kuu msimu ujao. Toto itaendelea na kampeni zake za kufa na kupona leo ikiwa mwenyeji wa Simba kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, mechi ambayo haitarajiwi kuwa rahisi, ingawa timu hiyo huisumbua Simba mara kwa mara wakikutana hasa nyumbani kwao.

Kwa upande wa Majimaji bado ina kazi kubwa na yenyewe ya kujinusuru kwani imekuwa na kwikwi katika mechi zake, ikipoteza pointi nyingi na kushinda ama kutoka sare mechi chache. Kocha wake Kally hajakata tamaa, anasema atapambana mpaka dakika ya mwisho kuibakiza timu yake hiyo kwenye Ligi Kuu msimu ujao.

Mbao, ambayo ilipata zali la kucheza Ligi Kuu baada ya sakata la tuhuma za kupanga matokeo kwa timu za Geita Gold na Polisi Tabora katika Ligi daraja la kwanza, na yenyewe isipokaza, inaweza kurudi ilipotoka. Mbao ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo ikiwa na pointi 27, tofauti ya pointi moja kwenye ukanda wa kushuka daraja.

Kwa maana hiyo, timu hiyo nayo haina kazi nyepesi katika kuhakikisha inabaki Ligi Kuu msimu ujao. Mbao mwishoni mwa wiki iliyopita nusura itoke shujaa uwanjani baada ya kuifunga Simba mabao 2-0, lakini zikiwa zimesalia dakika nane mchezo kumalizika, Simba ilipata mabao matatu na hivyo kuipoka Mbao tonge mdomoni.

Tayari timu hiyo imeshaanza kuvurugana kwa kumsimamisha kipa wake namba moja Eric Ngwengwe wakimtuhumu kuwahujumu kutokana na kufungwa mabao matatu ya haraka haraka na kukosa ushindi katika mechi hiyo. Kwa mtiririko huo, ni wazi kati ya timu hizo hakuna iliyo salama, isipokuwa JKT ambayo bila kupepesa macho inahitaji miujiza kubaki Ligi Kuu.

Vita nyingine ipo kwenye kumaliza nafasi nne za juu, ambapo Mtibwa Sugar, Azam, na Kagera zinachuana vikali. Mtibwa iko tofauti ya pointi tisa kwenye nne bora, ikiwa nafasi ya tano na pointi zake 36 huku Azam ilito nafasi ya nne ikiwa na pointi 45.

Msimu uliopita, Azam ilimaliza ya pili, lakini msimu huu ina kila dalili ya kutomaliza nafasi hiyo, na badala yake inapambana kumaliza nafasi ya tatu ama ya nne. Mtibwa Sugar kama ilivyo misimu zaidi ya kumi sasa, kubaki kwenye ligi, ndivyo ilivyo msimu huu pia.

Timu hii, tangu ilipotwaa ubingwa mwaka 2000, haijawa tena kwenye ushindani wa kiwango kile, na misimu yote imekuwa ikimaliza nafasi za katikati. Kagera Sugar, bado ina nguvu ikijitutumua kumaliza nafasi za juu kwa karibu misimu mitatu sasa.

Kazi kubwa bado ipo kwa mahasimu, Simba na Yanga hapo ndipo kwenye shughuli pevu katika kuwania ubingwa. Ni wazi sasa mbio za ubingwa zimebaki kwa wakongwe hao tu wa soka, tofauti na msimu uliopita, ambapo mbio zilibaki kwa Yanga, Simba na Azam.

Msimu huu umerudia enzi za misimu mingine kabla ya Azam kuanza kushiriki ligi, kwamba bingwa kama sio Simba basi Yanga na mshindi wa pili ni timu mojawapo kati ya hizo. Hivi sasa timu hizo zinapishana kwa pointi chache, Simba ikiongoza lakini ikiwa mbele kwa mchezo mmoja dhidi ya Yanga inayoshiriki michuano ya kimataifa.

Awali, kabla haijacheza mechi za kanda ya Ziwa, Simba ilitamba ubingwa wake upo kwenye kanda hiyo ambapo wangeutwaa kama wangeshinda mechi zote tatu. Lakini hali ilikuwa tofauti baada ya kupoteza mechi kwa Kagera Sugar kwenye uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Lakini ushindi wake wa mabao 3-2 dhidi ya Mbao umeifanya Simba kuwa kwenye matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa baada ya kuukosa kwa takriban miaka minne. Leo ina mechi kali ya mwisho ya Kanda ya Ziwa dhidi ya Toto, mechi ambayo ikishinda itajiweka pazuri zaidi.

Kwa upande wa mabingwa watetezi Yanga, nao wapo kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao, hasa kutokana na wachezaji wake bado kuwa kwenye kiwango kizuri. Yanga ina mchezo mmoja kibindoni, ambapo inatarajia kucheza wiki ijayo baada ya kutoka Algeria kucheza mechi ya kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mc Alger ya huko.