CHESCO MLOWE: Mke amenikimbia TASAF imeniokoa

CHESCO Mlowe (52), mkazi wa Kijiji cha Mpakani katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, anasema amekimbiwa na mkewe kutokana na ugumu wa maisha ulioikumba familia yao.

Anasema anakumbuka namna walivyokubaliana na mke huyo kuishi pamoja katika namna yoyote ya maisha wanayopangiwa na Mungu sambamba na juhudi zao za kufanya kazi kwa maarifa, iwe katika shida au raha. Hata hivyo, baada ya miaka kadhaa ya maisha yao, mambo yalianza kwenda mrama.

Anasema mkewe huyo ambaye kwa sasa tunahifadhi jina lake kwa sababu za kitaaluma, alianza kuonesha mabadiliko ya kitabia kadiri siku zilivyokwenda. Hii ni baada ya kuona hakuna mabadiliko yanayoonekana kimaisha katika familia yao tangu waanzishe maisha ya pamoja na badala yake, kauli za “tuvumilie tu ipo siku” kutoka kwa mume zikazidi kuongezeka.

“Niliamini mabadiliko ya mke wangu yalitokana na namna ugumu wa maisha ulivyotuandama. Tulilazimika kula mlo mmoja kwa siku tena kutokana na kile tulichokipata kwenye vibarua vya aina mbalimbali vikiwemo vya kazi mbalimbali kwenye mashamba ya mpunga,” anasema Chesco.

Hata hivyo, Chesco anasema mkewe alichoshwa na ahadi alizokuwa akimpa hivyo, akatokomea kusikojulikana. Anasema, “Wakati anaondoka, familia yetu ilikuwa imebahatika kumpata mtoto mmoja wa kiume.” Chesco anasema hili lilikuwa pigo kubwa kwake kwani kitendo cha mwanamke huyo kuondoka na mtoto huyo pekee waliye naye, kilizidi kumchanganya kwa kuwa pamoja na ugumu wa maisha, alikuwa bado anawahitaji na kuwapenda wote.

“Kwa kweli nimepata wakati mgumu sana. Nilikwishazoea kuishi na mtu na wakati mwingine naamini nilikuwa najituma zaidi kutafuta vibarua kwa kuwa nilikuwa na watu nyuma waliosubiri nirudi na chochote.” “Sasa wameondoka, nakwenda kumtafutia nani? Haya ndiyo huwa najiuliza baada ya kukimbiwa na mke wangu na mtoto.”

Hata hivyo, wahenga walisema mgaagaa na upwa, hali wali mkavu na Mungu si Athumani. Baada ya Mradi wa Kunusuru Kaya Masikini unaoendeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), kutokana na maisha aliyokuwa anaishi, Chesco akawa mmoja wa watu wenye maisha magumu katika Kijiji cha Mpakani waliopitishwa na na kuingizwa katika mpango huo.

“Naamini kabisa nilistahili kuingizwa kwenye mradi huu. Hali yangu ya kimaisha ilionesha wazi nilikuwa masikini ninayehitaji kusaidiwa.” “Niliamini ni msaada pekee kutoka nje ambao ungeyabadili maisha yangu. Ingawa ni makosa kukata tamaa, kwa mipango na uwezo wangu pekee, nilikuwa nimefikia ukomo wa kuwaza. Ilikuwa vigumu kubadilika,” anasema Chesco.

Anaeleza, “Nyumba niliyokuwa nikiishi, mlo niliokuwa nikila wa kubangaiza, mavazi niliyokuwa nikivaa, wewe ukiona tu, unajua kabisa ugumu wa maisha uliokuwa ukinikabili.” “Hata ushiriki wangu katika masuala ya kijamii hususani kuchangia miradi ya maendeleo ulikuwa mdogo. Muda mwingi nilikuwa nalazimika kuwa kwenye vibarua.”

“Waliniandikisha wanakijiji wenzangu baada ya wao wenyewe kujiaminisha kuwa mimi ni masikini ninayehitaji kusaidiwa.” Chesco anasema pamoja na kuwa anaamini kuwa alistahili kuingizwa kwenye mpango wa kuokoa kaya masikini, hakuamini kuwa amekuwa miongoni mwa watu watakaonufaika na Tasaf III.

Kwa msingi huu anafahamisha kuwa, kabla ya kupokea pesa, alianza kupanga na kufikiria ataanza kufanya kitu gani mradi utapoanza kutekelezwa. Anasema baada ya kupokea fedha za awali za Tasaf III pamoja na mahitaji mengine ya nyumbani alijifunza kilimo cha nyanya.

Baadaye alikodi nusu ekari ya shamba la nyanya alipolima na kuvuna kwa msimu wa kwanza. Anasema, huo ndiyo ulikuwa mwanzo wake wa kushika pesa zilizompa wazo la kubadili makazi yake kwa kujenga nyumba mpya na kuondokana na ki-jumba kidogo cha zamani.

“Kwa kuwa uwanja ulikuwepo hapa hapa kwenye mji wangu haikuwa shida sana, nilinunua tofali za kuchomwa na nikawa nakwenda kwa hatua kila nilipopokea fedha za Tasaf na ninapouza nyanya na pia nikipata fedha za vibarua maana bado naendelea navyo.”

Hadi kufikia mwaka jana, Chesco alikuwa amefanikiwa kukamilisha ujenzi na kuhamia kwenye nyumba yake japo baadhi ya miundombinu kama madirisha, sakafu bora bado havijawekwa.

“Ujenzi wangu nao unakwenda pole pole kutokana na kila ninachokuwa nimekipata. Japo sijaweka madirisha, nimeona bora nihamie humu kuliko kubaki kwenye kile kijumba kidogo cha nyasi.” Chesco anasema kwa mara ya mwisho alisikia mkewe ameonekana mjini Makambako mkoani Njombe.

Hii ni baada ya mmoja wa ndugu wa Chesco kukutana na mwanamke huyo kwenye moja ya mtaa wa mji huo. Anasema ndugu huyo alipomsalimia shemeji huyo, alimjulisha kuwa, anaishi mjini hapo.

Anasema pamoja na mafanikio aliyoyapata kupitia Tasaf III, bado anahitaji muda zaidi kuendelea na mradi huu kwa kuwa baada ya kujenga nyumba, amejikita katika mambo yatakayokuza uchumi wake ili utegemezi kwake ubakie historia.

Kuhusu suala la mkewe, Chesco anasema kutokana na dunia hii kukumbwa na magonjwa mengi ya kuambukiza ni vigumu kumrejesha na kuja kuishi nae, kabla ya hatua nyinginemakini kuchukuliwa na anasisitiza kuwa, kwa kuwa Yule ni mzazi mwenzake, hana kinyongo cha kumfanya asisamehe kama imani za dini zinavyotaka.

Anachohitaji anasema, ni kujua hali na maendeleo ya mtoto wao na kwamba ikiwezekana, amweke katika mazingira ya kupata huduma muhimu.

“Shughuli kubwa ninayoona hivi sasa naiweza ni hii ya kilimo cha nyanya. Hii nadhani itaniwezesha kupiga hatua haraka kwa kuwa tayari nimeshuhudia.” “Ila ufugaji nao nataka nijifunze kwa wenzangu wanufaika wa Tasaf maana naona nao wameweza hasa katika kufuga nguruwe na kuku. Itabidi nijifunze kwao na mimi nifanye miradi hiyo. Siwezi kubakia nikitegemea kilimo cha nyanya pekee.”

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpakani, Ignas Ndendya anasema kijiji chake kina wakazi zaidi ya 5500 zilizopo katika kaya 2050.Kati ya kaya hizo 354 zinanufaika na Tasaf III.

Ndendya anasema tangu kuanza kwa mradi wa Tasaf III Serikali ya kijiji imekuwa ikichukua jitihada za mara kwa mara kuhakikisha wanufaika wanapewa msaada kila wanapohitaji hususani wataalamu ili kuwezesha shughuli zao za uzalishaji kuwa na tija.

“Ni faraja kwetu kama uongozi wa kijiji tunapoona mkazi wetu kama Chesco amebadilika kimaisha kutoka maisha magumu zaidi aliyokuwa akiishi miaka michache iliyopita hadi sasa analala kwenye nyumba iliyoezekwa bati japo ni ndogo,” anasema.