Hoja kuu 23 zilizopata majibu Mwanza

JUMANNE ya Aprili 11, itabaki kuwa siku ya kukumbukwa kwa wakazi wa Mwanza kwa kuwa mwenyeji wa Jukwaa la Biashara la pili kuandaliwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN). Jukwaa la kwanza lilifanyika Simiyu mwezi Februari.

Baada ya mada mbalimbali kuwasilishwa na wadau wa maendeleo kwenye jukwaa hilo lililoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, hoja 23 zikiwemo za jumla na zingine zikielekezwa kwa baadhi ya wadau waliowasilisha mada ziliibuliwa. Baadhi ya mada hizo zimeshaandikwa na vyombo mbalimbali vya habari likiwemo gazeti hili na zingine tutaendelea kuziandika kwa kina kutegemea umuhimu wake kwa mkoa wa Mwanza na nchi yetu kwa ujumla.

Mbali na hoja hizo 23 zilizoulizwa hadharani pamoja na majibu yake, washiriki pia waliuliza takribani hoja 30 kwa njia ya kuandika, lakini kutokana na muda, hazikupata nafasi ya kujibiwa. Baadhi ya hoja hizo tutaziandika katika makala zijazo na kuona namna nzuri ya wahusika kuzijibu kupitia TSN inayochapisha magazeti ya HabariLeo, Daily News na SpotiLeo; sambamba na kuendesha mitandao kadhaa ya kijamii inayowafikia takribani watu 87,000 kwa dakika.

Waliotoa mada kwenye jukwaa hilo lililoshirikisha watu takribani 300 ni pamoja na Kampuni ya Simu ya nchini (TTCL), hoteli ya kisasa jijini Mwanza ya Victoria Palace na Mfuko wa Pensheni wa PPF, Benki za NMB, TIB (Development), TIB (Corporate) na Benki ya TPB. Wengine walikuwa ni Mamlaka ya Mapato (TRA), Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bohari ya Dawa (MSD), Watumishi Housing Company (WHC), Mfuko wa Pensheni wa LAPF, Baraza la Biashara Tanzania, Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

TSN na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mwanza kupitia Kitengo cha Uwekezaji na Mpango Jiji wa Mwanza pia waliwasilisha mada zilizowafanya washiriki kukaa vitini mwao kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa 12 na dakika kadhaa jioni. HOJA KWA WHC Hoja zilizoelekezwa Watumishi Housing Company (WHC) ni pamoja kujua ni kwa nini taasisi hiyo ya kiserikali imepanga kujenga nyumba za waalimu za vyumba viwili badala ya vitatu kwani familia huwa na watoto pia wa kiume na wa kike.

Yupo mshiriki aliyetaka kujua pia kama WHC inaweza kumjengea mtu nyumba kwenye kiwanja chake na swali lingine likawa kama taasisi hiyo inaweza sasa kutumia mbao kutoka kwenye msitu wa serikali wa Buhindi, badala ya zile za mtaani ambazo pengine hazina ubora. Hoja nyingine ilitaka miradi ya WHC kama inayojengwa katika eneo la Kiseke, Mwanza, inufaishe vijana wa eneo husika badala ya wageni.

Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Company, Dk Fred Msemwa, alisema ujenzi wa nyumba za waalimu unaofanywa na WHC ni mpango uliobuniwa na serikali na kwa hali ya kifedha ilivyo sasa ikaonekana ni vyema kwa kuanzia wajenge vyumba viwili kwa familia kwa maeneo yenye uhitaji mkuwa wa nyumba. “Kwa sasa tunajenga nyumba kwenye maeneo yenye mazingira magumu sana kwa waalimu.

Kuna maeneo, siyo tu kwamba shule haina nyumba za waalimu bali hata wenyeji hawana nyumba za kupangisha,” alisema na kufafanua kwamba nyumba wanazojenga huwa na vyumba viwili, sebule, jiko na stoo. Alizidi kufafanua kwamba kuna maeneo ambayo mkuu wa shule analazimika kukaa nyumbani kwake na waalimu wanne waliokosa makazi. Kuhusu vijana kunufaika na miradi yao, Dk Msemwa alifafanua kwamba ipo miradi inayojengwa na wakandarasi na mingine wao wenyewe.

Akasema kwa ile ya wakandarasi hawawapangii watu wa kuwatumia wakiwemo vibarua, lakini akasema ana hakika wengi huwa wakazi wa eneo husika. Lakini akasema ile ya kwao wanatumia vijana wa eneo husika kujenga nyumba. Kadhalika alisema miradi hiyo mara nyingi pia hutumia matofali na zana zingine za ujenzi kutoka eneo husika na hivyo kuwanufaisha wenyeji, alimradi tu matofali hayo yawe ya viwango vinavyotakiwa.

Alifafanua kwamba katika mradi wa nyumba wa Kisesa kila kitu kilitoka Mwanza, ikiwa ni pamoja mbao, na kwamba takribani watu 60, wakazi wa mkoa huo walinufaika na ajira. Alisema kwa wale wanaotaka kujengewa kwenye viwanja vyao, wanatakiwa kuwasiliana na uongozi wa WHC ili kujua idadi yao na kuona namna ya kuwajengea nyumba za kisasa.

Alisema pia watafanyia kazi wazo la kutumia mbao zinazotoka kwenye misitu ya serikali ukiwemo wa Buhindi. HOJA KWENDA TRA Kama ilivyotazamiwa, Mamlaka ya Mapato (TRA) ni moja ya wadau muhimu wa maendeleo ambako maswali mengi yaliyoelekezwa huko. Lipo swali lililotaka kujua idadi ya wanaotumia mashine za kielektroniki za EFDs katika kufanya malipo na pia kujua jinsi TRA inavyoweza kuwafikia wote wanaofaa kutumia EFDs.

TRA pia ilihojiwa kwamba kama sasa mtu anaweza kutumia mtandao wa kompyuta kujua makadirio ya kodi ya gari anayotaka kuagiza kwa nini isiwe hivyo pia kwa bidhaa zingine? Kadhalika ikahojiwa kwa nini baadhi ya usajili wa biashara wahusika wanauliza maswali kama unamiliki gari, watoto wangapi ulio nao na wanasoma shule gani. Mamlaka hiyo pia ilihojiwa kuhusu mpango iliyo nayo katika kuwezesha kuwa na eneo moja tu ambalo mtu, kwa mfano anayeanzisha biashara, halazimiki kwenda ofisi zingine za mbali (one stop centre).

Kadhalika kuliibuliwa hoja kwamba katika tovuti ya TRA, maelezo yanayopatikana kwenye Kiingereza ni tofauti na yale ya Kiswahili na kushauriwa kuhakikisha maelezo yanarandana katika kila lugha. Kuna aliyedai kwamba walisajili kampuni ya ushirika lakini kukawa na shida katika kuhamisha namba ya mlipa kodi (TIN) ya mwanaushirika mmoja kutoka mkoa wake wa sasa kwenda walikohamishia biashara.

TRA pia ilitakiwa kutoa ufafanuzi kama makadirio ya mtu anayeanzisha biashara yanafanywa kabla ya kuanza kuzalisha au baada ya kuanza kuzalisha (kufanya biashara). Mkazi mwingine wa Mwanza aliitaka TRA iongeze ofisi Mwanza ili kupunguza foleni kunapokuwa na suala kama la kub adilisha namba ya mlipa kodi (TIN).

Akijibu baadhi ya hoja hizo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi wa TRA, Richard Kayombo alianza kwa kusema kwamba mkakati wa kuhakikisha kunakuwa na eneo moja la kutolea huduma za kodi na ushuru badala ya mtu kuhangaika kwenda huku na kule, liko mezani kwa ajili ya kufanyiwa kazi. Alikiri pia kwamba suala la watu kurundikana ili kuhakiki TIN zao ni changamoto ya kweli ambayo wanaifanyia kazi pia. “Tutaongeza vifaa na watumishi.

Lakini Watanzania nao ni wa ajabu. Unapotangaza suala kama hili, huwaoni siku za mwanzo. Wanasubiri siku za mwisho ndipo wanakwenda na kusababisha mrundikano... Ukiongeza siku huwaoni lakini siku hizo zikikaribia kuisha wanarundikana tena,” alisema akishauri Watanzania kujenga utamaduni wa kutosubiri siku za mwisho ndipo kurundikana kwenye huduma.

Kuhusu maelezo ya Kiswahili kutorandana na Kiingereza kwenye tovuti ya TRA, Kayombo alisema wamelisikia na watalifanyia kazi lakini akasema wanakoangalia zaidi ni kwenye Kiswalihi kwani asilimia 80 ya walipa kodi nchini wanazungumza Kiswahili. Kuhusu makadirio alisema kuna kundi la wafanyabiashara halihusiki na makadirio na wala kulazimika kutunza kumbukumbu.

Akafafanua pia kwamba kimsingi baada ya mtu kupewa TIN ambayo alisisitiza kwamba hutolewa bure, mfanyabiashara anakuwa na siku 90 kabla ya kulipa kodi. “Lakini tatizo ni kwamba wengi wanakimbia baada ya kupata TIN (na ndio maana tunawataka kulipa mwanzo). Lakini tunatafuta njia bora zaidi ya kulishughulikia hili,” alisema. Naye Ofisa Mkuu wa Mapato wa TRA, Julius Siza, alijibu swali lililouliza kuhusu takwimu za walionunua EFDs akisema ilikuwa vigumu kuzipata haraka haraka wakati ule wa Jukwaa.

Lakini alisema kusajili wafanyabiashara washirika (partnerships) hakuna kabisa ulazima wa wahusika wote kusajili katika kila mkoa. “Kinachotakiwa ni alama tu za vidole,” alifafanua. Kuhusu umuhimu wa kila bidhaa mtu kujua kodi yake kama ilivyo kwa magari alisema ni jambo linalowezekana kwani cha msingi ni kuwa na kanzidata (data base). “Hili tunalibeba kama changamoto, pengine siku moja utajua mzigo wangu wowote ule utatakiwa kulipiwa kodi kiasi gani,” alisema.

Alisema suala la kuulizwa idadi ya watoto halihusiki wakati wa kuingiza mzigo bali utaulizwa unapofungua biashara. “Ni muhimu kujua uwezo wako kuhusu fedha ili ukadiriaji mzuri ufanyike,” alisema. HOJA KWA MABENKI Zipo hoja kadhaa zilielekezwa kwa mabenki ikiwa ni pamoja na kwa nini yanapokopa Benki Kuu (BoT), lakini bado yanatoa riba kubwa kwa wananchi.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha wateja wakubwa wa NMB, Nsolo Mlozi, akijibu hoja hiyo alisema kimsingi ni BoT ndiyo unayoyapa mabenki muongozo. “BoT imeruhusu benki za kibiashara kwenda kukopa kupitia hati fungani. Benki ikikopa kwa asilimia 14, nayo itaongeza asilimia 2 tu na kumbuka mtu anakopa kwa muda wa miaka minane hadi 15 kumaliza marejesho ya deni.”

Alifafanua kwamba inabidi mabenki kuongeza riba kidogo ili yaweza kujiendesha kwa maana ya kulipa mishahara na hata kupata faida. “Cha msingi ni Watanzania tuhakikishe tunakuza uchumi ili hata riba ya hati fungani ipungue. Kuna wakati hati fungani zilishuka hadi asilimia 9 na sisi kwenye mabenki tuliona haja ya kushusha riba pia kwa wateja wetu,” alisema.

Hoja nyingine iliyoelekezwa kwa mabenki ni jinsi yasivyosaidia kilimo ambacho kinaajiri zaidi ya asilimia 70 ya wakazi wa mkoa wa Mwanza. Kwamba hata eneo hilo la kilimo halikuzungumziwa vya kutosha na vyombo vya kifedha kwa maana ya namna vinavyoweza kusaidia katika eneo hilo (agro financing). Akijibu swali hilo, alisema mabenki ikiwemo NMB wanajua umuhimu na ndio maana wao (NMB) wameanzisha dirisha la kilimo na kuwataka wakulima kwenda kuona namna wanavyoweza kufaidika na dirisha hilo.

“Tatizo ni kwamba kilimo chetu bado si cha kibiashara. Tuhame kutoka kwenye kilimo cha kujikimu kwenda kwenye kilimo cha biashara,” alishauri. MWANZA NA TEHAMA Yupo mshiriki aliyetaka mkoa wa Mwanza uwe na tovuti yake itakayoonesha fursa zote zinazopatikana Mwanza. Pia alitaka kujua namna mji huo unavyofikiria suala zima la malipo ya maegesho ya magari kisasa.

Akijibu hoja hiyo, Mtaalamu wa masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), George Mulamula, alisema mbali na tovuti ya mkoa, wataanzisha nyingine ikihusisha taarifa kuhusu wafanya biashara na fursa ambazo zipo. Alisema mkoa wa Mwanza umedhamiria kutumia Tehama kutatua changamoto nyingi na ndio maana vijana wanaoweza kutumia Tehama kubuni namna ya kutatua matatizo ya wananchi wanakaribishwa sana.

Alitoa mfano wa changamoto ya mashua nyingi kuibiwa, hatua ambayo wabunifu wanaweza kuona namna ya kukomesha tatizo hilo kwa kutumia Tehama. Kuhusu maegesho, Mhandisi Mulamula alisema Mwanza itaanza kutumia mashine kujua muda ambao mtu ameegesha gari lake na kwamba wanajipanga kuongea na jiji kuhusu hilo. Alisema pia wanataka kuwasaidia wakulima wa Mwanza kuendesha kilimo cha kisasa kinachotumia eneo dogo kwa mavuno mengi maarufu kama green house.

Lipo pia swali liliulizwa kuhusu watoto wengi kufeli darasa la saba na mkakati wa kuwasaidia ili wasiishie vijiweni. Mulamula alisema Tehama inaweza kuwasaidia. “Tunataka mtu akitaka kwenda Veta (chuo cha ufundi stadi), anajifunza ufundi kupitia simu. Baada ya kuelewa masomo yako, unachokifanya ni kwenda kuhakikiwa (kufanya mtihani) katika chuo cha karibu. Ukifaulu, unapata cheti.

Hii itawasaidia vijana wengi wanaoishia darasa la saba.” BOHARI YA DAWA Baada ya Bohari ya Dawa (MSD) kutoa changamoto kwa wakazi wa Mwanza kuhusu kuanzisha viwanda vya dawa kwa kuwa soko lipo, kuna huyu aliyesema kwa wanaotaka kuanzisha viwanda vya aina hiyo, kama vile makasha maalumu ya kutupia taka hospitalini, hawajui waanzie wapi, kama ni MSD, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) au Shirika la Viwango (TBS).

Akijibu, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakuni, aliwaambia wanaotaka kuanzisha viwanda vya dawa kwanza kwenda MSD ili kujua vipimo vinavyotakiwa vya bidhaa zao. Alifafanua kwamba kama bidhaa inahusu dawa au chakula mhusika anatakiwa kwenda TFDA (baada ya kutoka kwao) na zaidi ya hapo anakwenda TBS. HOJA ZA JUMLA Kulikuwa pia na hoja za jumla ambazo baadhi zilijibiwa na Mkuu wa Mkoa, Mongella.

Kwa mfano kuna aliyehoji kwa nini inaonekana sasa bandari inajengwa Misungwi na siyo Mwanza mjini. Mkuu wa mkoa alisema kilichotokea ni suala la eneo tu la mipaka ya kiutawala lakini haiko mbali kutoka Mwanza mjini. Hoja nyingine ilijikita katika kuimarisha utalii Kanda ya Ziwa ambapo mtoa hoja alisema: “Ningeomba Bodi ya Utalii sasa waweke kwenye vipeperushi vyao kutangaza vivutio vya Mwanza.”

Kuna huyu aliyesema kuna shida ya watendaji kukwepa majukumu yao pale unapotaka kusikia ushauri au maelezo yao. Akasema kwa kulijua hilo kuna mtu alimuuliza taratibu za kuanza biashara akamwambia; “We anza tu, wahusika watakukuta huko huko.” Akijibu, Mkuu wa Mkoa alisema yapo mazingira ambayo mtu anatakiwa kujiongeza alimradi anachokifanya kina manufaa kwake na kwa jamii.

Mwingine kutoka wilaya ya Misungwi aliamua kuwa ‘mwamba ngoma’ na kusema: “Misungwi ni walaya iliyobaki kuwa ni kioo cha mkoa wa Mwanza. Tuna ardhi ya kutosha, tena inapatikana kwa gharama nafuu. Kama tutataka kujenga kiwanja cha ndege cha kimataifa, kileteni Misungxwi. Mkuu wa mkoa, Mongella alijibu kwamba ramani inaonesha kwamba kiwanja cha ndege cha kimataifa kitajengwa Mabuki, Misungwi, kilometa chache tu kutoka Mwanza mjini.

Hoja nyingine iliyotolewa ni kutaka jukwaa lingine wadau wa maendeleo wajikite katika kusaidia kilimo cha umwagiliaji kwa kuzingatia kwamba Mwanza ina rasilimali ya maji ya kutosha kwa maana ya Ziwa Victoria. Mwingine aliutaka mkoa kushughulikia tatizo la ongezeko la ombaomba Mwanza. “Kuna vijana wadogo na watu wazima. Kama jamii tujiulize tunatengeneza jamii gani? Tuone namna nzuri ya kuwaondoa hawa vijana na kuwaweka sehemu na kisha kuwaendeleza,” alishauri.

Kuna aliyeshauri suala la urasimishaji wa biashara kuzungumzwa kwa mapana katika majukwaa yajayo. Mwingine alitaka mpango wa upimaji ardhi Mwanza uwe shirikishi ili kuondoa migogoro kwa wananchi. Kadhalika, jukwaa lilisikia habari ya mwekezaji mmoja wa Misungwi ambaye ana zaidi ya ekari 30, ana hati ya kimila na umeme unafika kwake lakini amekosa mtaji wa Sh milioni 30 tu ili kuanza kuzalisha mali.

Tukutane tena Jumatatu kwa ajili ya kuumulika zaidi mkoa wa Mwanza.