‘Uhandisi mitambo umesheheni viwango vya ubora, vitumieni’

KIWANGO cha ubora wa bidhaa au huduma ni nyaraka iliyorithiwa na wataalamu wa sekta husika, ikiwa imejumuisha mahitaji muhimu ya bidhaa inayoandaliwa kiwango. Ofisa Viwango wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Yona Afrika, anasema uhandisi mitambo pekee una aina 280 za viwango hadi sasa, huku vingine vikiendelea kuandaliwa kulingana na mahitaji.

Kwa mujibu wa Afrika, maandalizi ya viwango hivyo huhusisha wataalamu mbalimbali kutoka katika shirika hilo la viwango, wazalishaji wa bidhaa pamoja na wana sekta zinazohusika na bidhaa zinazotengenezewa viwango, ili, pamoja na kuhakikisha havitengenezwi bila kuhususha wazalishaji, vizingatie mapendekezo ya msingi na yanayostahili ya wadau wa bidhaa hizo, kwa faida ya watumiaji, mazingira na uchumi wa nchi pia. Anasema viwango vya ubora wa bidhaa vinavyoandaliwa nchini hufahamika kuwa ni vya kitaifa na vimekuwa vikiandaliwa kwa kuzingatia mazingira ya mahali vinapozalishwa na vinapotumika.

Afrika anaweka wazi kuwa maandalizi ya viwango vya ubora ni mchakato unaohusisha utafiti wa kina wa aina ya bidhaa inayotengenezewa kiwango ili vinapokuwa tayari na kuanza kutumika visigeuke kikwazo kwa afya za watumiaji, bidhaa yenyewe na hata kwa wafanyabiashara wanaoizalisha au wanaoisambaza, ili uchumi pia usipate matokeo hasi kwa maana ya kuvurugwa kwa soko linalopokea bidhaa zilizotengenezewa viwango.

Anaeleza kuwa, kiwango cha ubora kinamhusu mtumiaji pia kwa sababu, anapokuwa ananunua bidhaa anayoihitaji, huweza kukagua na kuona ikiwa kiwango husika kimezingatiwa wakati wa uzalishaji. Anataja baadhi ya bidhaa zinazotumika kujengea nyumba, ambazo kitaalamu huzitambua kama malighafi za ujenzi, zikiwemo nondo, mabati, saruji, misumari na vingine muhimu na kusema kuwa viwango vyake vya ubora vipo katika shirika hilo na vimeanza kutumika muda mrefu uliopita.

Anasema watu wote wanaonunua na kuzalisha bidhaa hawana budi kuhakikisha kuwa wanakuwa navyo na kuvielewa vizuri, ili wanapotaka kuvitumia au kuhakikisha endapo vimezingatiwa kuzalisha bidhaa wanayohitaji kuinunua. Kwa ufupi, mtaalamu huyo anawataka Watanzania wazalishaji na wanaonunua bidhaa za ujenzi waelewe kuwa kuna umuhimu kuvifahamu viwango vya ubora wa bidhaa wanazozihitaji kabla ya kuzinunua, ili kujiridhisha endapo vimezingatiwa.

Anasema kufanya hivyo kuna faida nyingi, ikiwemo kukwepa hasara ya fedha, kuondoa uwezekano wa kupoteza nguvu kazi itakayotumika, muda pamoja na kulinda afya za watumiaji bidhaa husika, pamoja na mazingira yanayowazunguka. WATEJA WATAJUAJE VIWANGO VIMEZINGATIWA? Kwa maelezo ya Afrika, viwango ni lazima viandikwe kwa kuchapwa katika bidhaa husika.

Anasema ikiwa mteja ataona aina ya kiwango imeandikwa kwa kalamu au kwa rangi na kwamba mkono ndio uliotumika badala ya mashine, ni lazima wawasiliane na shirika hilo kupata uthibitisho endapo bidhaa husika imepimwa ubora au la. “Hiyo itamsaidia kupata bidhaa yenye uhakika kuhusu ubora. Anapobahatisha kupata bidhaa iliyotengenezwa bila kiwango husika kuzingatiwa anakuwa na hatari ya kupata hasara kwa kutopata bidhaa inayolingana na thamani ya fedha alizolipa,” anasema.

Anataja bidhaa nyingine ambazo Watanzania wanapaswa kufahamu kwamba viwango vyake vipo katika shirika hilo kuwa ni pamoja na vifaa vya usafiri au usafirishaji ambavyo wengi wamekuwa wakiamini kwamba vinatoka nje ya Tanzania, hivyo kutojisumbua kuvipata. Miongoni mwa vifaa hivyo ni magari yaliotumika ambayo kiwango chake cha ubora ni TZS 698, pikipiki zenye kiwango TZS: 1231, kofia ngumu (Helmet) zenye kiwango cha ubora TZS: 1478 na mfumo wa magari yanayotumia gesi asilia ambao kiwango chake cha ubora ni TZS: 1187 na matairi yanayofaa yenye kiwango TZS :617 na TZS : 618 .

“Viwango vya matairi vilianza kutumika kitaifa miaka ya 1970 hivyo kutuwezesha kama nchi kujua matairi yanayofaa ni yapi na yasiyofaa ni yapi. Matairi chakavu ni yale yasiyokuwa na kiwango chochote kati ya hivyo viwili na kwa sababu ya kuwa hafifu, yamewekwa katika kundi la matairi chakavu, yasiyofaa kwa matumizi kwa sababu ni hatari kuyatumia,”anasema.

Kutokana na maelezo yake, matairi yaliyotumika maarufu kama matairi yaliyochongwa, ni hatari kwa sababu hayajulikani yalikotolewa yalitumika kwa muda gani, hata kama muonekano wake unakuwa ni mzuri. Anasema kwa mujibu wa viwango vya ubora wa matairi, pindi tairi linapofungwa katika gari la aina yoyote, kutumika na kutolewa linakuwa ni chakavu, labda kama mchakato unakuwa umefanywa kulirudisha kupimwa ubora wake na kutangazwa kuwa linafaa kuendelea kutumika.

Anaongeza; “Viwango vya ubora vya matairi vya kitaifa na kimataifa vinatambua tairi jipya kuwa ni lile lililotoka kiwandani moja kwa moja, hata kama linauzwa dukani au katika soko la aina nyingine. Ili kulitambua tairi jipya, mnunuzi anapaswa kuhakikisha liko katika makaratasi yake maalumu yanayotumika kama vifungashio na kuwa na kiwango kilichochapishwa kwa mashine”.

Anaweka wazi kuwa hiyo ni kwa sababu matakwa ya viwango vya ubora wa matairi hayaruhusu yatolewe kiwandani bila kufungashwa kitaalamu. Anasema, tofauti na matairi yaliyotumika ambayo sehemu yake ya juu imelika na kubaki na mfano wa sehemu ya juu yaani vipara, matairi mapya hayapati pancha hovyo wala kuchanwa na vitu vyenye ncha, yanapokuwa katika mikikimikiki ya barabarani.

Anataja sifa nyingine za matairi mapya kuwa ni pamoja na kutovimba, kufunga breki kila dereva anaposhika breki awapo safarini, kutopasuka wakati wa joto na kutulia barabarani ikiwa njia ni nzuri. TBS inasema pia kuwa ina viwango vya ubora kwa ajili ya magari ya kubebea mafuta, vituo vya mafuta, namna ya kutunza mafuta mengi (petroleum deposits), mitungi ya gesi za kupikia, mabomba ya maji safi na maji taka, vifaa vya zimamoto, vifuniko ya mitaro ya maji, matrekta ya kulimia ikiwemo power tiller na vya vilainishi vya mitambo na magari.

Vingine vilivyotajwa ni viwango vya spea za magari, tube za magari, baiskeli pamoja na viwango vya ujenzi wa mabasi ya abiria. “Viwango vya ubora wa bidhaa au huduma huandikwa na kuchapishwa, hivyo mteja au mzalishaji anapofika kuvichukua TBS hueleweshwa maana ya viwango hivyo, ikiwa atahitaji, ili asivitumie kwa makosa au kwa kubahatisha,” anasema na kuongeza kuwa, viwango huuzwa kwa ukurasa kulingana na matakwa ya mhitaji.