Kutamani kula udongo huashiria upungufu wa madini mwilini

UPUNGUFU wa damu ni hali itokanayo na seli nyekundu za damu kuwa chini ya kiwango cha kawaida. Seli hizi zina protini iitwayo hemoglobin ambayo hutumika kubeba Oksijeni kutoka kwenye mapafu na kuisambaza katika viungo mbali mbali vya mwili.

Katika hali hiyo, viungo vya mwili havipati Oksijeni ya kutosha na husababisha muathirika kujisikia uchovu usio wa kawaida, kuishiwa pumzi, kizunguzungu, kichwa kuuma au kuongezeka kwa kasi ya mapigo ya moyo. Daktari Bingwa wa magonjwa ya damu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Clara Chamba anasema, takwimu zinaonesha kuwa takriban asilimia 25 ya watu ulimwenguni wana upungufu wa damu.

Anaeleza makundi yaliyo athirika zaidi kwa upungufu wa damu ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wanawake walioko kwenye umri wa kuzaa. Anasema tafiti zilizofanyika nchini, zinaonyesha kuwa, asilimia 60 ya watoto chini ya umri wa miaka mitano wana tatizo la upungufu wa damu, huku Shinyanga ikiongoza.

“Kwa tafiti zilizofanywa kwa wanawake, karibia nusu ya wanawake wote wana upungufu wa damu, hasa Kaskazini Pemba, ambapo asilimia 72 ya wanawake katika kisiwa hiki wana upungufu wa damu,” anasema daktari huyo. Anasema, upungufu wa damu ni hali inayotokana na maradhi mengine ndani ya mwili. Hivyo upungufu huo ni ishara au dalili kuwa mtu ana ugonjwa fulani.

Anasema ingawa sababu za kupungukiwa damu ni nyingi, zinaweza kugawanywa katika makundi makuu matatu ambayo kundi la kwanza ni upungufu wa damu utokanao na kuvuja damu. Daktari huyo anasema kuvuja damu huko hutokea kwenye ajali, vidonda vya tumbo, wakati wa hedhi kwa wanawake, saratani ya utumbo au wakati wa upasuaji.

Dk Chamba anasema upungufu mwingine wa damu unatokana na uboho kushindwa kuzalisha damu au kuzalisha damu kwa uhafifu, hali am bayo husababishwa na upungufu wa virutubisho vinavyohitajika kuzalisha damu yaani madini chuma, vitamin B12 na folic acid. Vile vile anasema magonjwa ya maambukizi kama vile ukosefu wa kinga mwilini, kifua kikuu na magonjwa sugu kama saratani, kisukari, shinikizo la damu la juu na magonjwa ya figo, huchangia tatizo.

“Matumizi ya dawa za aina fulani, mfano dawa zinazotumika kwenye matibabu ya saratani, chloramphenicol, zidovudine pamoja na vinywaji vyenye kileo, matibabu ya mionzi pamoja na hitilafu katika seli zinazohusika na uzalishaji wa damu,” anasema daktari huyo. Pia anasema upungufu wa damu unatokana na uharibifu au kuvunjwa vunjwa seli nyekundu za damu.

Anaelezea kuwa kwa kawaida seli nyekundu za damu huishi kwa muda wa siku 120 hivyo hitilafu zinapotokea kwenye seli hizi, mwili hulazimika kuzitoa mapema kwenye mzunguko wa damu kabla ya kutimiza siku hizo 120. Lakini pia anasema baadhi ya magonjwa hayo, mtu huzaliwa nayo. Mfanoo mzuri ni ugonjwa wa selimundu.

“Huu ni ugonjwa wa kurithi unaosababisha seli nyekundu za damu kuwa na umbo lisilo la kawaida (mundu) na kukwama ndani ya mishipa ya damu. Hii husababisha maumivu makali kutokea katika sehemu mbali mbali za mwili zilizoathirika na huweza pia kuleteleza madhara makubwa zaidi kama ugonjwa wa kupooza au kuharibu ufanisi wa viungo mbali mbali,” anasema.

Anasema miongoni mwa mambo yote hayo yanayosababisha upungufu wa damu, upungufu wa madini chuma una mchango mkubwa katika upungufu wa damu. Asilimia kubwa ya watu wenye upungufu wa damu mara nyingi hukutwa na upungufu wa madini chuma. Upungufu wa madini chuma hutokana na lishe hafifu, matumizi makubwa ya madini chuma ndani ya mwili hususani wajawazito, watoto na kuvuja damu muda mrefu.

Hedhi zisizo za kawaida na vidonda vya tumbo, huchangia tatizo. Anasema watu wengi husumbuliwa na upungufu wa damu kutokana na kutokuwa na mazoea ya kula mlo kamili anasema madini chuma hupatikana kwa wingi kwenye mboga za majani, dagaa, nyama na maini. Anaelezea dalili mojawapo ya upungufu wa madini chuma ni kuwa na hamu ya vitu visivyo vya kawaida, mfano, hamu ya kula udongo au hamu ya kula barafu.

Ili kuepuka kuwa na upungufu wa damu anasema ni muhimu kuhakikisha mtu anakula mlo uliokamilika. Pia anashauri iwapo mtu ana dalili zozote za upungufu wa damu, aende hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Iwapo mhusika ana magonjwa sugu, afuatilie matibabu yake na kufanya uchunguzi wa mara kwa mara. “Unapokutwa na upungufu wa damu, hakikisha unafanya uchunguzi zaidi kujua chanzo, na usitumie dawa ovyo bila kujua chanzo kwa kuwa si kila upungufu wa damu unatibika kwa kutumia dawa za kuongeza madini chuma,” anasema .

Dk Chamba anashauri kwamba, endapo mgonjwa amepewa dawa za kuongeza damu, afuate masharti na azitumie kama inavyotakiwa