Korea Kusini yaja na mafunzo ya nishati mbadala

TANZANIA na Korea Kusini zimekuwa na uhusiano wa kidiplomasia kwa takribani miaka 25. Katika utekelezaji wa uhusiano huo wa kidiplomasia, Serikali ya Korea Kusini imejikita kuisaidia Tanzania katika kukuza na kuendeleza teknolojia mbalimbali, lengo likiwa ni kusaidia ukuaji wa sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Kituo cha Teknolojia Ubunifu na Nishati (iTEC) kwa kushirikiana Chuo Kikuu cha Taifa cha Seoul cha nchini Korea wamejipanga kuinua ukuwaji wa tekinolojia husani vijijini ili kuwainua watu wa maeneo ambayo si rahisi kufikika.

Mkurugenzi wa iTEC, Dk Herb Rheen anasema pamoja na Tanzania kugundua gesi asili, Serikali ya Korea Kusini kupitia chuo hicho cha Seoul imejipanga kusaidia Tanzania katika kukuza nyanja ya teknolojia, ikiwamo utoaji wa mafunzo ya nishati mbadala ili kurahisisha upatikanaji wa nishati ya umeme kwa urahisi zaidi.

Hatua hii itasaidia katika kufikia lengo namba 7 la maendeleo endelevu ambalo linataka kila mtu awe na uwezo wa kufikiwa na nishati mbadala kwa gharama nafuu ifikapo 2030. Rheen anasema hatua hiyo ni katika kupambana na tatizo ukosefu wa nishati ya umeme vijijini kwa kujenga mtambo wa kuzalisha umeme jua kwa baadhi ya vijiji.

“Mitambo hiyo itakuwa nje ya gridi ya taifa, na lengo ni kuhamasisha utumiaji wa umeme jua maeneo ya vijijini, umeme huo utakuwa ni nafuu, lengo ni kuhakikisha kila mwanakijiji anaweza kutumia umeme,” anasema.

Rheen anasema pia kituo kimepanga kutoa elimu ya teknolojia ya habari (IT) na uanzishwaji wa biashara na mafunzo ya kupromoti vituo vya afya vya umma kupitia utoaji chanjo salama,” alisema.

Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, iTEC kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi cha Nelson Mandela cha jijini Arusha, kinatarajia kuanza kutoa mafunzo ya nishati mbadala, usafirishaji na usambazaji mazao ya kilimo.

Akizungumzia mafunzo ambayo yanatarajia kuanza muda wowote kuanzia Agosti mwaka huu, anasema pia yatalenga fani za afya na maji, mafunzo ya ufundi na biashara. Rheen anasema kituo kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 1,000 kwa mwaka ambao watachukua kozi hizo tano zitakazotolewa na kituo hicho.

“Tuna furaha kuwaletea habari njema za kuanza kwa mradi ambao unatekelezwa na Chuo cha Seout chini ya udhaminiwa na Serikali ya Korea Kusini. “Tutakuwa na kituo cha teknolojia ambacho kitakuwa kwenye Chuo Kikuu cha Sayansi cha Nelson Mandela Arusha.

Hatua hii imekuja ikiwa imepita miaka minne ya iTEC kufanya miradi mbalimbali ya ubunifu ikiwamo kutoka elimu na mafunzo ya IT kwa wanafunzi na walimu mkoani Arusha,” anasema. Anasema kabla ya kuja na mpango huo, kituo cha iTEC kilitoa mafunzo ya IT na kuwafikia wanafunzi 300 wa shule za sekondari katika mkoa wa Arusha na walimu 200 wa shule ya msingi na sekondari, lengo likiwa ni kupata walimu wenye elimu ya teknolojia hiyo.

“Tumekuwa tukitoa mafunzo ya ICT kwa miaka minne ya nyuma tangu mwaka 2013 na Serikali ya Korea Kusini ilipopata taarifa hizi ndio wakaamua kutoa ufadhili wa kuanzisha kituo.

“Tulikuwa tunatoa mafunzo kwa eneo dogo, lakini kwa ufadhili wa serikali tutatoa mafunzo kwa wigo mpana zaidi, lengo likiwa ni kuwapata wabunifu wengi maeneo ya vijijini,” anasema.

Anapofafanua zaidi kuhusu kituo hicho cha ubunifu na nishati mbadala, Rheen anasema: “Lengo la kuanzisha mafunzo hayo ni kuhamisha teknolojia kutoka Korea Kusini kuja kwa Watanzania. Lengo ni kuwajengea uwezo hususani kwa wale wa vijijini ili kuwapa ubunifu wa kuweza kutengeneza mitambo midogo itakayoweza kuzalisha umeme.

“Tunataka wataalamu wa vijijini ambao watakuwa na uwezo wa kutengeneza mitambo midogo ya kuzalisha umeme jua ambayo itaweza kuunganisha umeme kwa nyumba 200, shule, vituo vya afya na zahanati.

Anasema hatua hiyo pia itafanyika katika kukuza kilimo na upatikanaji wa maji na teknolojia ya mawasiliano ya habari jambo ambalo litainua ubunifu na maendeleo ya wananchi wa vijijini.

“Tutafanya hivi mara nne kwa mwaka, kwa miaka minne, na kila mwaka tutakuwa tunarudia haya katika eneo tofauti, kila mwaka tutakuwa tunarudia haya kwa undani zaidi kwa kushirikisha wanafunzi zaidi, viongozi wa serikali za vijiji,” anasema.

Anaongeza: “Tunataka kuwashirikisha viongozi wa vijiji, tunaamini kwa kufanya hivyo miradi hii itakuwa ni endelevu, na tayari watakuwa wamejifunza jinsi ya kufanya na kuwa rahisi kuisimamia.”

Anasema ili kuwapata wanafunzi watakaofundishwa katika kituo hicho, wanashirikiana na Chuo cha Nelson Mandela, kwa kudahili wanafunzi ili kuhamisha teknolojia kwa usahihi zaidi.

“Tunachokifanya ni kuwezesha wananchi kutumia umeme jua, sambamba na kukuza sekta ya kilimo, kwa sababu tunaamini watu wa Tanzania ni watu wazuri wenye uwezo na hasa ukizingatia kuwa udongo wa Arusha ni mzuri,” anasema.

Anasema katika mpango huo, pia wamelenga katika sekta ya afya kwa umma, kwa kusaidia vifaa vya kubebea na utoaji wa chanjo, ili kufika maeneo ambayo ni vigumu kufikika na maeneo ambayo hakuna vituo vya afya na zahanati.

“Utakuwa ni ubunifu wa kutengeneza jokofu ndogo la kuhifadhia chanjo hizo.” Mwanzilishi na Katibu Mkuu wa iTEC, Ji huyun Moon anasema watatumia teknolojia katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja ya afya, ujasiriamali na elimu na kufikia maeneo ya vijijini kwa njia ya ICT.

Anaendelea kufafanua lengo la kuanzisha kituo hicho kuwa ni kutoa mafunzo na kuendeleza mawazo ya kuwa na wajasiriamali kwa vijana nchini Tanzania, badala ya wao kutegemea ajira rasmi.

Akitolea mfano utekelezaji wa utoaji elimu ya ICT kuanzia mwaka 2013 katika maeneo kadhaa mkoani Dodoma na Arusha, Ji-Young anasema wameweza kuwapa mafunzo ya IT wanafunzi wa sekondari 300 na walimu wa shule za msingi na sekondari wapatao 200.

“Tulibaini tatizo ni kutokuwapo kwa karakana, uhaba wa walimu kwenye somo la ICT na kubwa kukosekana kwa umme maeneo ya vijijini, hivyo tumewapa elimu ya msingi na wakiwa tayari tutajua namna ya kusonga mbele,” anasema.

Anasema kupitia miradi ya awali, waliweza kupatikana kwa umeme jua kwa baadhi ya vijiji jambo ambalo limechangia kuibua shughuli ya ujasiriamali na kufungua kituo cha mawasiliano ambapo wananchi wanaweza kupata taarifa kupitia luninga na huduma ya intaneti.