Veta, Sido na mkakati wa kuwapa ujuzi wajasiriamali

HIVI karibuni Mamlaka ya Kusimamia Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Shirika la Kusimamia Maendeleo ya Viwanda Vidogo Nchini (SIDO) walitia saini makubaliano ya miaka mitatu kuimarisha maandalizi ya kufikia uchumi wa viwanda. Inafahamika azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ifikapo mwaka 2025 liwe taifa la uchumi wa viwanda.

Taarifa zinaonesha mataifa mengi yaliyofanikiwa, yaliingia katika uchumi wa aina hiyo kwa kutegemea viwanda vidogo. Veta na Sido zimejipambanua katika shughuli za kijasiriamali, ambapo kuna wanaotoa elimu ya ufundi stadi na wanaosimamia maendeleo ya viwanda vidogo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhelm Meru aliyehudhuria hafla ya kusaini makubaliano hayo, anasema Tanzania imeamua kwa dhati ifikapo mwaka 2025, iwe na uchumi wa viwanda.

“Ndiyo sababu ya kufanya yote haya… tunataka pato la taifa linalotokana na viwanda lifikie asilimia 15,” anasema Meru. Fursa hizi si za vijana tu kama wengi wanavyotazamia kuwa masuala yanayohusu masomo ni ya watu wenye uwezo wa kusoma. Kila mmoja ana nafasi yake katika kuifikisha nchi anayoipenda mahali pazuri.

Mkurugenzi Mtendaji wa SIDO, Profesa Sylvester Mpanduji anasema wanataka baada ya kukamilika programu hii wanafunzi watakaopitia VETA wawe na uwezo wa kuanzisha viwanda vidogo na vya kati pamoja na kuviendeleza. Programu hii inafanyaje kazi? Hili ni swali linalojibiwa na watendaji hawa.

Majibu kwa swali hili yanazingatia ukweli kwamba, mitaani kuna watu wengi wanaofanya shughuli za kijasiriamali kwa kurithi au kujifunza mitaani. Lakini mafanikio yanakuwa madogo kutokana na kukosa elimu rasmi. Veta inawajibika kufanya kazi ya kuandaa mafundi na wataalamu wa shughuli za mikono.

Kwa hiyo watakachofanya Sido ni kupeleka wataalamu wao kusoma chuoni hapo. Wakishahitimu, wanarudi kwenye taasisi yao kwa mafunzo kwa vitendo na wale watakaokuwa tayari kuanzisha viwanda kuna utaratibu wa kupata mikopo.

Profesa Mpanduji anafafanua juu ya uwezeshaji wa vijana wabunifu kupitia mikopo akisema: “Vijana wabunifu tutawatengenezea programu maalumu ili wawe na uwezo wa kujiajiri, watakaoandika miradi mizuri na ikapitishwa watapewa mikopo kwa ajili ya kuanzisha viwanda.” Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Veta, Dk Bwire Ndazi anasema dhamira ya chuo hicho tangu kilipoanzishwa mwaka 1994 ni kutoa ujuzi kwa vijana ili wapate uwezo wa kujiajiri.

Hivyo kuwepo makubaliano haya kutasaidia kutimiza dhamira ya serikali kuwa na vijana watakaozalisha ajira nyingi hasa katika upande wa viwanda na ufundi stadi. Inaelezwa kuwa upo utaratibu wa masomo kulingana na uwezo wa msomaji.

Wapo watakaosoma kwa mwaka mmoja wengine miezi sita na wapo watakaosoma kwa wiki kadhaa na kuhitimu kisha watakabidhiwa vyeti. Kwa kuwa uchumi wa viwanda unaendana na kuuza bidhaa bora. Ili hilo lifanikiwe, lazima mafunzo aina hii yawepo.

Inafafanuliwa kwamba, Sido tangu siku nyingi wana njia nyingi za kufundisha ujasiriamali kupitia vituo vyao atamizi (incubator), lakini wameona mahitaji ni makubwa kwa sababu mitaani kumejaa mafundi wasio na ujuzi. Kwa kuwa masuala haya ya kusaidia jamii lazima liwepo swali juu ya upatikanaji wa fedha, Katibu Mkuu Meru anasema wameweka mkakati wa kutosha kifedha.

“Kwanza kuna mfuko wa wajasiriamali (NEDFU) unasaidia kutoa mikopo kwa wajasiriamali wenye nia ya kujiajiri,” anasema Meru. Aidha, anasema bajeti ya mwaka huu imetenga Sh bilioni 2.4 kwa ajili ya kusaidia wajasiriamali katika sekta ya viwanda na pia upo mpango, mwaka ujao wa fedha serikali itaongeza zaidi. “Lakini pia kuna zile fedha zilizoahidiwa na serikali ya awamu ya tano, shilingi milioni 50 kwa kila kijiji, tutazitumia vema kufanikisha hili,” anasema Meru.

Kama hiyo haitoshi, Profesa Mpanduji ameweka wazi umuhimu wa kupatikana fedha na kusisitiza wajasiriamali hawapaswi kuwa na shaka katika hili kwa sababu mipango ipo mingi kuhakikisha fedha zinapatikana. “Viwanda vidogo kabisa, vidogo na vya kati vinahitaji fedha.

Wapo vijana wenye uwezo lakini hawana fedha na hawajui namna ya kuomba mikopo, hivyo baada ya mafunzo kwa wale watakaoweza kuandaa maandiko watapatiwa mikopo kulingana na mahitaji,” anasema Profesa Mpanduji.

Mpango huu utawafikia vijana 20,000 kila mwaka ambapo kwa mujibu wa wawakilishi kutoka Veta, huenda idadi ikaongezeka kila mwaka kwa sababu watakaohitimu watakuwa mabalozi kwa wengine.

Wakati dunia ikishangazwa na kasi ya China kwenye ulimwengu wa teknolojia na viwanda, inaelezwa kuwa mafanikio hayo hayakuja kama zawadi au bahati nasibu bali mikakati ya muda mrefu na kufanya kazi kwa bidii ndiyo siri ya mafanikio.

Tangu mwaka 1978 China ilielekeza nguvu zake katika viwanda vidogo na sekta ya kilimo. Hapa ndipo walipoanza kuona mwanga wa mafanikio na sasa inatajwa kuwa nchi ya pili kwa uchumi wa viwanda baada ya Marekani.