Miguu bandia, suluhisho la unyayo uliopinda kwa watoto

TATIZO la miguu pinde kwa watoto limeendelea kuwasumbua wazazi na walezi ambao wengi hushindwa kujua njia mbadala za kulitatua . Miguu pinde kwa watoto ni hali ya mtoto kuzaliwa akiwa na unyayo uliopinda na lisipotatuliwa, husababisha ulemavu.

Lakini likiwahiwa kwa kutumia teknolojia ya kunyoosha nyayo, mtoto hupona na kuendelea kuwa kwenye hali ya kawaida kama watoto wengine. Unyooshaji hufanyika kwa kutumia mguu bandia. Teknolojia ya miguu hiyo ilibuniwa na raia wa Hispania, Dk Ignacio Ponseti ambaye ni mwanzilishi wa Chama cha Madaktari wa kusaidia tatizo hilo la miguu pinde.

Kutokana na harakati zake hizo, kila ifikapo Juni 3, huadhimisha siku ya miguu pinde kwa watoto. Daktari huyo aliyezaliwa Juni 3, 1914 na kuaga dunia Oktoba 2009, anatajwa kujikita zaidi katika uunganishaji wa mifupa.

Mwaka huu, siku hiyo ya miguu pinde kwa watoto, hapa nchini iliadhimishwa katika Hospitali ya CCBRT, Dar es Salaam ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa ni ‘Kabiliana na miguu pinde kwa watoto’.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Erwin Telemansin anasema kuwa teknolojia hiyo imewasaidia watoto zaidi ya 1000 hadi sasa. Anasema, watoto wanaokabiliwa na changamoto hiyo wanatibiwa kirahisi zaidi iwapo watawahi tiba hiyo.

Watoto wanaozaliwa na shida hiyo, hupewa huduma bure ya tiba kutokea hospitalini hapo na wazazi hawatakiwi kulipia gharama ya aina yoyote ile kuanzia siku ya kwanza hadi ya mwisho wa matibabu.

Mtaalamu huyo anaelezea miguu pinde kwa watoto kuwa matibabu yake huweza kuchukua hadi mwezi mmoja. Mtoto hufanyishwa mazoezi ya kunyoosha misuli ya unyayo uliopinda, ikiwa ni pamoja na kuvalishwa mguu huo wa bandia kuanzia kwenye sehemu ya unyayo.

Dk Telemansin anasema, kabla ya kuanzishwa na teknolojia hiyo ya uvaaji wa viatu kama njia rahisi ya kunyoosha unyayo wa mtoto, madaktari walikuwa na wakati mgumu zaidi wa kutibu tatizo hilo. Anasema, kwa kuwa utoaji huo wa huduma kwa sasa umerahisishwa zaidi na tiba inatolewa bure ni vema wazazi wakawapeleka watoto wao hospitalini hapo kwa tiba.

Anasema, “Ni vema kwa wazazi kutambua kuwa tatizo la miguu pinde sio ulemavu wa kudumu isipokuwa ni hali ambayo kama wakiwahi hospitali wanaweza kusaidiwa.” Anaongeza,”kwa kuwa huduma hii ni ya bure ni vema wakawahi kutatua tatizo hilo kwa kuwa wakichelewa na miguu ikakomaa, linakuja kuwa ni gumu kutatuliwa.”

Licha ya huduma hiyo kuwa ya bure, changamoto inayotajwa kuwakabili ni kwa wazazi na walezi wengi kutokuwa na taarifa za kutosha juu ya wapi pa kuwapeleka watoto wao waliozaliwa na shida hiyo. Dk Telemansin anasema kuwa wapo wazazi na walezi ambao hudhania kuwa watoto wanaozaliwa na tatizo hilo ni sawa na wanaozaliwa wakiwa na ulemavu mwingine usiotibika.

“Lakini kumbe wakielimishwa kuhusu tiba wanaweza kutatua mapema,” anasema. Anasema kuwa licha ya kuwa huduma hiyo ni ya bure bado kuna haja ya wadau wengine zaidi kujitokeza kuiwezesha hospitali yake kutoa huduma.

Anashukuru kampuni ya simu za mkononi, Tigo kwa kuchangia huduma hiyo kwa kutoa sh milioni 110. Kwa upande wake, Mkuu wa Udhibiti na Masuala ya kiserikali wa kampuni ya Tigo, Sylvia Balwire anasema wametambua nafasi ya teknolojia hiyo katika kusaidia watoto wenye ulemavu wa miguu na ndio maana kampuni imeamua kuchangia upatikanaji wa huduma hiyo ya bure.

Baadhi ya wazazi waliojitokeza kupeleka watoto ni pamoja na Anli Aboubakar na mkewe Wirda Mohamed ambao wametokea nchini Comoro kumleta mtoto wao mwenye tatizo la miguu pinde.

Wakizungumzia mtoto wao mwenye tatizo hilo, wanasema baada ya kuzaliwa na kubaini kasoro kwenye miguu yake, walihangaika bila mafanikio. Anasema, awali kama wazazi walikuwa wakijua kuwa ni mapenzi ya Mungu kwa mtoto wao kuzaliwa hivyo lakini wamekuja kugundua kuwa mtoto wao huo shida yake hiyo inaweza kutatuliwa.

Baba wa mtoto huyo anasema, alipata taarifa kwamba kuna huduma hiyo ya bure inayotolewa hospitalini CCBRT ndipo wakatoka nchini kwao kwa kusaidiwa na ndugu zao walio hapa nchini na kuja kuanza mchakato wa tiba.

Aboubakar anasema, baada ya kuwekewa mguu huo wa bandia kwa mtoto wao mabadiliko yameanza kuonekana kwani unaonekana kurejea kwenye uhalisia wake. “Kila siku tunakuja kumleta kwenye zoezi la kunyoosha viungo na kwa kiasi kikubwa imeanza kusaidia kuurejesha mguu wake kwenye hali yake ya kawaida,” anasema.

Katika kudhihirisha namna ambavyo teknolojia hiyo inavyoweza kuunyoosha unyayo wa mtoto kwa urahisi, Joan Masudi ni mzazi mwingine anayeshuhudia. Anasema binti yake, Saida alikuwa na tatizo hilo la kupinda mguu.

Anasema, ilimchukua takribani mwezi mmoja na nusu kukamilisha tiba na mtoto wake kuendelea tu kuuvaa mguu huo hadi sasa, amepona kabisa na anaendelea vema na masomo.

“Ni vema kwa wazazi na walezi kuwafikisha watoto wao kwenye huduma hii ya bure na yenye tija kwa watoto kwa kuwa wanatibiwa mapema na wanarejeshwa kwenye hali yao ya kawaida na hawatokuwa walemavu,” anasema.