‘Kila mwenye nia anayo fursa kusoma sekondari’

NEEMA Joseph (53) mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam ni miongoni mwa watu walionufaika na elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi maarufu kama QT. Kama angekata tamaa kwa kujiona kuwa hawezi kujiendeleza tena kama ilivyo kwa baadhi ya watu, Neema angeendelea na maisha ya kuwa mama wa nyumbani akiwa na elimu ya shule ya msingi.

Lakini kutokana na uthubutu, mama huyu aliamua kujiendeleza nje ya mfumo rasmi hadi akahitimu chuo kikuu. Neema ambaye sasa anafanya kazi katika kampuni binafsi jijini Dar es Salaam, anasema: “Nimejiendeleza kielimu hadi kufikia elimu ya chuo kikuu kupitia mafunzo ya elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi.” Mama huyu wa watoto watano, ni mfano wa kuigwa na watu wengi wenye shauku ya elimu, lakini waliojikatia tamaa.

Anaeleza kuwa awali alikuwa mama wa nyumbani lakini kuna ndugu yake alimshauri kupata mafunzo ya QT ili aweze kujiendeleza kimasomo aweze kuwa nafasi ya kupata kazi nzuri. “Niliamua kufuata ushauri huo na baadaye nikaanza masomo hayo Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo nilienda kwa ngazi nikafaulu mtihani wa kidato cha nne na baadaye nikafanya mtihani wa kidato cha Sita,” anaeleza.

Kwa mujibu wa mama huyu katika matokeo ya kidato cha sita, alifanya vizuri kwenye masomo yote akapata nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stephano Moshi (SMUCCO) cha Chuo Kikuu cha Tumaini.

Anasema alifanya vizuri katika masomo yake ya chuo na sasa ni muajiriwa wa kampuni moja binafsi. Njia aliyoipitia Neema ni mbadala ambayo serikali kwa kuona umuhimu wa elimu imekuwa na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha watu wengi wanajiendeleza pia kupitia vituo binafsi.

Elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi hailengi kundi maalumu la watu bali huwahusisha watu mbalimbali wakiwamo vijana hususani waliomaliza elimu ya msingi na pamoja na watu wazima ili kutoa fursa ya elimu ya sekondari kwa waliokosa nafasi ya kuendelea kwa sababu mbalimbali. Elimu hii nje ya mfumo rasmi ni mpango unaoendeshwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kufanikisha malengo yake.

Mpango huu ambao huchangia kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata elimu ya sekondari, umekuwa lulu katika kipindi hiki ambacho serikali ya awamu ya tano inataka kuipeleka Tanzania kwenye nchi ya uchumi wa kati unaotegemea viwanda. Unaendeshwa kupitia shule huria na masafa zipatazo 420 ambazo kati yake, zinazomilikiwa na TEWW ni 83 na watu binafsi ni 337 katika mikoa yote ya Tanzania Bara.

Vijana na watu wazima 95,140 wamefanikiwa kupata elimu ya sekondari kupitia mpango huu kwa kipindi cha kati ya mwaka 2010 hadi 2016. Huu ni mpango ambao unatajwa na wengi kuwa umekuwa mkombozi kwa watu wengi ambao kwa sababu mbalimbali walishindwa kupata elimu ya sekondari, lakini sasa wamejikuta wakisoma hadi chuo kikuu.

Kutokana na serikali kufungulia milango, hata hivyo inaelezwa wapo baadhi ya watu na taasisi ambao wamekuwa wakienda kinyume katika utoaji wa elimu hiyo nje ya mfumo rasmi.

Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi Taaluma wa TEWW, Dk Kassim Nihuka, vipo vituo 420 nchi nzima vinavyotoa mafunzo ya elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi. Programu hii ambayo inaendeshwa katika majengo ya shule za msingi na sekondari za serikali inahusisha vituo 83 vinavyosimamiwa na TEWW.

Vituo 337 viko vinajiendesha kwenye shule za wadau mbalimbali. Dk Nihuka anasema vijana na watu wazima 95,140 wamenufaika na mfumo huu wa elimu tangu mwaka 2010 hadi mwaka jana.

Hata hivyo, anasema kumekuwapo na vitendo vya baadhi ya vituo kutofuata taratibu zinazotokiwa. Kwa mfano, mwanzoni mwa mwaka huu, TEWW ilisema kati ya vituo 420, vituo 182 ndivyo vilikuwa vimesajiliwa na kufuata taratibu.

Hivyo vituo 155 vilivyoonekana vinakiuka taratibu, viliambiwa vitafutwa iwapo havitarekebisha kasoro mbalimbali zilizobainika. Miongoni mwa masharti yaliyokiukwa na vituo hivyo ni pamoja na kutokulipa ada ya uratibu ambayo ni Sh 20,000 kwa kila mwanafunzi aliyesajiliwa.

Vituo vingine vinaelezewa kuwa mazingira yake ya kufundishia hayaridhishi. Hata hivyo, viliagizwa vifanye marekebisho ya kasoro zilizobainika ili vijiendeshe kwa kuzingatia utaratibu.

Lengo la taasisi kuweka kanuni na taratibu kwa vituo hivyo, ni kuhakikisha wanafunzi wanaosoma katika mfumo huo wanapata elimu bora inayotambulika katika mfumo wa elimu wa nchi.

Wanafunzi wenye miaka chini ya 23 wakimaliza elimu ya kidato cha nne na kufaulu vizuri, wana fursa ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita, kama walivyo wanafunzi walio kwenye mfumo rasmi. Lakini mwenye miaka zaidi ya 25 atasoma kwa mwaka mmoja kidato cha tano na sita.

Anasema katika programu hiyo, masomo yanayotolewa katika hatua tatu kubwa moja ikiwa hatua ya kwanza inayobeba masomo ya kidato cha kwanza na cha pili. Hatua ya pili inabeba kidato cha tatu na nne na hatua ya tatu inabeba hatua ya kidato cha tano na sita.

Aidha anasema, mlengwa anasoma kwa mwaka mmoja na kuwa na sifa ya kufanya mtihani wa maarifa na anasoma masomo saba ambayo yanatolewa katika hatua hiyo ambayo ni Historia, Jiografia, Kiingereza, Kiswahili, Hisabati Biologia na Uraia.

Jamii inahimizwa kuendelea kutumia fursa hiyo kujipatia elimu ya sekondari .Wakati huo huo, Naibu Mkurugenzi Taaluma wa TEWW anatoa mwito kwa mamlaka za serikali za mitaa kuwahimiza wazazi kuwapeleka vijana wao waliokosa alama za ufaulu katika mtihani wa darasa la saba, kutumia fursa ya elimu kupitia taasisi ya elimu ya watu wazima.

Anakariri takwimu zilizotolewa na UNESCO za mwaka 2014 zinazoonesha jumla ya vijana na watu wazima milioni 3.5 wapo nje ya shule huku miongoni mwao, vijana milioni 2.5 wakihitaji elimu ya sekondari na wengine milioni moja wakihitaji elimu ya msingi.

Anasema idadi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka kutokana na ukweli kwamba vijana wanaomaliza elimu ya msingi na kupata alama za ufaulu chini ya 100 kati ya 250 wamekuwa wakiachwa bila kwenda sekondari katika mikoa mbalimbali.

Anasema katika kutekeleza mpango wa elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi, changamoto mbalimbali zinajitokeza ikiwemo kukosekana kwa elimu ya kutosha kwa umma na wazazi kuhusu mpango huo.

Wanashindwa kuelewa namna mfumo unavyoendeshwa na hivyo kusababisha baadhi ya wazazi na walezi kuhoji sababu za kutozwa ada wakati serikali ya awamu ya tano inatoa elimu msingi bila malipo. Changamoto nyingine inatajwa kuwa ni kutokana na baadhi ya wadau kuipotosha jamii na wazazi na walezi kwa kuwaelezea vijana wanaoingia katika mpango huo kuwa ni sawa na ‘chaguo la pili’.

Anasema dhana hiyo si sahihi kwani vijana hao ni wale waliokosa ufaulu wa kujiunga na shule za sekondari katika utaratibu wa kawaida. Nyingine ni kukosekana kwa mwamko chanya miongoni mwa wazazi kuhusu kuwapeleka vijana kupata elimu kupitia mpango wa elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi wakidhani kuwa elimu inayotolewa nje ya mfumo rasmi haitambulika na serikali.

Kuwapo kwa mfumo huu wa elimu, ni ujumbe tosha kwa waliokosa elimu ya sekondari, bila kujali umri au mazingira yake ya maisha, kutambua kuwa wanayo fursa ya kujiendeleza kadri wawezavyo hata kufika kiwango cha juu kabisa cha elimu.