Ijue homa ya nguruwe na ilivyowatoa machozi wafugaji

MLIPUKO wa homa ya nguruwe umekuwa ukikumba mikoa ya Mbeya, Rukwa, Iringa, Morogoro na Songwe. Ugonjwa huu unaosababishwa na virusi vinavyojulikana kitaalamu kama ‘African Swine Fever Virus’, umezikumba wilaya za Kalambo na ya Sumbawanga katika mkoa wa Rukwa na kusababisha vifo vya nguruwe zaidi ya 360.

Homa ya nguruwe ambayo husambazwa kutoka kwa nguruwe mmoja kwenda kwa mwingine kwa kasi kubwa, hujitokeza kwa nguruwe wanaofugwa na nguruwe pori. Pamoja na ugonjwa huu kujitokeza kwa nguruwe wanaofugwa, inaelezwa kwamba nguruwe pori pia hutunza vimelea vya ugonjwa huu bila wao wenyewe kuugua. Lakini wana uwezo wa kueneza vimelea vya ugonjwa huu kwa nguruwe wanaofugwa kwa njia ya kupe laini wanaojulikana kitaalamu kama Ornithodoros moumbata.

Inasemekana nguruwe wanaofugwa ambao wanaachiwa kuzurura ovyo, huwa ndiyo chanzo cha kuenea kwa ugonjwa huo pale watapoumwa na kupe ambao watadondoshwa na nguruwe pori.

Mganga wa Mifugo wa Kituo cha Magonjwa ya Mifugo Nyanda za Juu Kusini, Dk Kaini Kamwela anasema mara baada ya kuona dalili za kuwepo kwa ugonjwa huo, walichukua sampuli kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya kitaalamu na kuisafirisha kwenye maabara kuu iliyopo Dar ers Salaam.

Wilaya hizo zilizokumbwa na mlipuko, (Kalamabo na Sumbawanga), zimetoa hadhari kwa wachinjaji, wafanyabiashara na wananchi wote kuhusu ugonjwa wa homa ya nguruwe (AS F). Takwimu zinaonesha idadi ya nguruwe waliokufa kwenye mabano katika wilaya hizo; Kalambo (200), manispaa ya Sumbawanga (80) na halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga wamekufa nguruwe 89.

Uwapo wa ugonjwa huo umethibitishwa na wataalamu wa Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Wanyama Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi (ZVC). Ugonjwa huo ulianzia Kalambo na kisha ukaingia halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga.

Kwa kuzingatia mamlaka aliyopewa kwa Sheria namba 17 ya Magonjwa na Wanyama ya mwaka 2003, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania ametangaza eneo lote la Manispaa ya Sumbwanga na Halmashauri ya Kalambo kuwa chini ya uangalizi maalumu kwa kuwa kuna maambukizo au yapo katika hatari kubwa ya muambukizwa ugonjwa huo.

Vijiji ambavyo vilikumbwa zaidi na ugonjwa ni Kalembe, Legeza Mwendo na Mkombo katika wilaya Kalambo. Mganga wa mifugo Dk Kamwela anasema mara baada ya kuona dalili za kuwapo ugonjwa huo, walichukua sampuli kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya kitaalamu.

Walisafirisha sampuli kwenda maabara kuu jijini Dar es Salaam. “Matokeo ya vipimo hivyo yalithibitisha kuwepo kwa ugonjwa huo na tukaanza kuwahadharisha wananachi juu ya kuwakinga nguruwe wao na ugonjwa huo ikiwemo kutosafirisha mazao ya mnyama huyo kuepusha kuenea kwa ugonjwa huo,” anasema.

Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Simon Ngagani kuwatuma wataalamu wake kwenye maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo ili wakatoe elimu sahihi ya kuukabili na kudhibiti usafirishaji wa nguruwe. Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Halfani Haule amethibitisha kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya nguruwe katika wilaya ya Sumbawanga.

“Kuanzia sasa ni marufuku wanyama hao na bidhaa zake kusafirishwa kutoka eneo moja kwenda eneo jingine ndani na nje ya wilaya hii,” alisema na kusisitiza nguruwe wote wafungiwe wasiachwe wakizurura ovyo.

Akisisitiza kuwa ugonjwa wa homa ya nguruwe hauna tiba, Dk Haule anasisitiza watu wasije kula nyama ya waliokufa. Elimu imeanza kutolewa kwa wafugaji kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji hadi kata kwa kusambaza vipeperushi vinavyoeleza namna ya kujikinga na ugonjwa huo na athari zake kiuchumi.

Wananchi wote hawaruhusiwi kuingiza, kutoa au kupitisha wanayama hai au mizoga jamii ya nguruwe katika Manispaa ya Sumbawanga bila kibali cha Mkurugenzi wa Huduma ya Mifugo. Uchinjaji na biashara ya nguruwe hauruhusiwi hadi hapo tangazo litakapotolewa tena.

Lakini pia hakuna ruhusa ya kuingiza, kuondoa au kupitisha mazao yanayohusika na nguruwe ikiwa ni pamoja na nyama, mbolea, manyoya, mifupa, ngozi na vyakula vya kusindika.

Ofisa Mifugo wa Manispaa ya Sumbawanga, Victor Nziku anaagiza wanyama nguruwe wote watakaokufa wateketezwe kwa moto au kufukiwa katika shimo la kina chenye futi zisizopungua nne ili kuzuia maambukizi na uchafuzi wa mazingira.

Jambo lingine linalosisitizwa kwa wafugaji, ni kuhakikisha nguruwe wote wanakuwa mabandani na wakati wote inapulizwa dawa ya V – Rid (Gluteraldehyde), Vircon na/au Fomaldehyde.

Ili kuimarisha ulinzi dhidi ya ugonjwa huo, imekubalika kwamba, nguruwe yeyote atakayeonekana akizurura ovyo nje, atakamatwa na iwapo mmiliki wa nguruwe huyo hatajitokeza basi nguruwe atauawa na kuteketezwa bila ya fidia.

Nziku anasema, changamoto kubwa iliyopo sasa, ni ya wafugaji walio katika maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo kuuza mizoga ya nguruwe kwa bei ya kutupa kwa wafanyabiashara ambao pia huisafirisha usiku wakitumia pikipiki.

“Changamoto kubwa iliyojitokeza mizoga ya nguruwe hao inauzwa kwa bei ya kutupa… wafanyabiashara wenye uchu wa utajiri wa haraka wanaisafirisha usiku kwa pikipiki kutoka kwenye maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo na kuisafirisha na kuiuza kwa walaji katika maeneo ambayo hayajakumbwa na hivyo kusababisha ugonjwa uenee,” anasema Nziku.

Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Kalambo, Wilbroad Kansapa akizungumza na mwandishi wa makala haya anasema wilaya hiyo itaendelea kuwekewa karantini hadi hapo wataalamu watakapojiridhisha kuwa ugonjwa umekoma.

Anataja vijiji vilivyoathirika zaidi ni Legeza mwendo, Mwambwe Kenya, Kalembe na Tunyi vyote vya Kata ya Legezamwendo. Baadhi ya wafugaji, wanakiri kupata athari kubwa za kiuchumi kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo kuzikumba wilaya za Sumbawanga na Kalambo.

“Ni hasara kubwa sana nimeipata. Nilikuwa na nguruwe 14 wote wamepukutika na ugonjwa huu nimebaki masikini,” anasema mmoja wa wafugaji katika kijiji cha Kalembe akisisitiza kuwa ugonjwa huu umeleta kilio kikubwa miongoni mwao.

Lakini mfugaji huyu anasema, kupitia elimu wanayoipata baada ya mlipuko, wamejifunza kuwa ufugaji bora wa wanyama hawa ni kuwajengea mabanda imara na siyo kuwaachia wazurure. Anatamani kila mfugaji kufahamu hilo ili kuwaepusha balaa hili la homa ya nguruwe