Uchomaji mkaa unavyosababisha ‘kilio’ kwa miti asilia

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe akizungumza katika makumbusho ya taifa ya Majimaji Songea, alisema mkoa wa Ruvuma bado una misitu mingi ikilinganishwa na mingine nchini.

Amesema ni vema viongozi wote kuanzia ngazi ya Mkoa, wilaya, tarafa, kata hadi vijiji kuanza kuchukua hatua za kulinda misitu iliyopo kabla ya kuharibiwa kama ilivyo katika mikoa mingine nchini. “Moja ya vitu ambavyo vinaharibu misitu kupita vitu vingine vyote ni biashara ya mkaa, umewahi kuona mkata miti na muuza mkaa amekuwa tajiri?’’ anasema Profesa Maghembe.

Anasema miti ni viumbe hai ambayo ikikatwa hulia, na mkataji anapata dhambi kubwa kwa Mwenyezi Mungu. “Pigeni marufuku kuchoma mkaa Mbinga na kuleta Songea, badala yake mkaa uuzwe katika eneo ambalo umekatwa, usisafirishwe ili kuzuia nchi isije kugeuka jangwa. Watu wa misitu acheni kutoa leseni ya misitu kusafirishwa nje ya wilaya, mkaa ambao unasafirishwa kutoka wilaya nyingine kwenda wilaya nyingine kamateni’’, Maghembe anaagiza.

Tafiti zilizofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN HABITAT) mwaka 2008 zimeonesha kuwa Tanzania inaongoza kwa matumizi ya nishati ya mkaa. Hii ina maana ya kwamba uharibifu wa mazingira hasa ukataji wa miti holela ni mkubwa na unahitaji nguvu ya ziada na ya pamoja kwa wadau kutoka ngazi zote kuanzia familia, kitongoji, mtaa kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla ili kurekebisha na kurudisha miti inayokatwa kwa ajili ya uchomaji mkaa na kuni.

Kwa miaka mingi, Mkoa wa Ruvuma umekuwa ni miongoni mwa mikoa michache ambayo mazingira yake yana unafuu ikilinganishwa na mikoa mingine nchini. Uharibifu mkubwa wa mazingira katika mikoa mbalimbali nchini umesababisha maeneo mengi kuwa na ukame kutokana na kukauka kwa vyanzo vingi vya maji.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dk Binilith Mahenge mara kadhaa akizungumza na wananchi katika wilaya za mkoa amewaonya wananchi wanaoharibu mazingira ikiwemo ukataji miti na uchomaji misitu kuacha mara moja, vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria. Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa katika baadhi ya wilaya Ruvuma unaonesha ukataji wa misitu na uchomaji moto ovyo ni vitendo ambavyo vinafanyika kwa kasi katika mkoa wa Ruvuma hivi sasa.

Wilaya ya Songea ni miongoni mwa maeneo ambayo kasi ya ufyekaji misitu ni kubwa hivyo vitendo vya uharibifu visipodhibitiwa mapema, ipo hatari baada ya miaka michache ijayo, misitu ikateketea hasa kutokana na biashara ya mkaa ambayo imekithiri. Serikali imeshaagiza kufanyike utafiti katika baadhi ya wilaya na kubaini kiwango cha uharibifu wa misitu unaofanywa na wafanyabiashara wa mkaa ambao inadaiwa wengi wao wanatoka nje ya mkoa wa Ruvuma.

Utafiti huo umebaini kuwa wafanyabiashara hao wanafyeka misitu katika kasi ya kutisha wilayani Songea na kuchoma mkaa ambao unasafirishwa na kujipatia faida kubwa bila kujali athari za mzingira zinazotokea. Hata hivyo kisheria, mfanyabiashara yeyote wa mkaa ni lazima awe na kibali kinachomruhusu kufanya biashara hiyo.

Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi, Balozi Salome Sijaona anaelezea masikitiko yake kutokana na uharibifu wa kutisha wa mazingira unaofanywa katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma. Sijaona anakumbuka misitu minene ya asili ambayo ilikuwepo zamani katika mkoa wa Ruvuma ambayo hivi sasa imeteketea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo biashara ya mkaa.

Balozi Sijaona ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Msindo wilayani Namtumbo, anasema mtu aliyefika Ruvuma miaka 15 iliyopita akifika leo atashangaa kuona misitu minene ya asili ya kuvutia imeharibiwa. Anahadharisha kuwa hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo hakuna hatua za makusudi za kukabiliana na uharibifu huo.

“Mimi ni mzaliwa wa mkoa wa Ruvuma tabia ya ukataji wa misitu kwa ajili ya kutengenezea mkaa haikuwepo kabisa katika mkoa huu, watu walikuwa wanapikia kuni lakini hivi sasa wengi wameanzisha biashara ya mkaa, hivyo wanashambulia misitu ya asili na kuvuna miti kiholela hili ni jambo la hatari sana,” anasisitiza Sijaona. Uchomaji mkaa unavyosababisha ‘kilio’ kwa miti asilia Ukataji wa misitu hovyo unaendelea katika maeneo mbalimbali wilayani Songea.

Biashara ya mkaa ambayo imeshamiri katika wilaya ya Songea mkoa wa Ruvuma na kusababisha misitu kuteketezwa. Uchunguzi umebaini kuwa watu wengi wanachoma mkaa na kupasua mbao katika misitu mbalimbali ya asili mkoani Ruvuma bila kuchukua hatua za kukabiliana na uharibifu huo kama vile kupanda miti kwa kasi inayolingana na uvunaji.

Uharibifu wa misitu ya asili katika mkoa wa Ruvuma unaweza kuongezeka zaidi baada ya sasa milango ya Mtwara korido kufunguka na kuunganisha mikoa ya Kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma sanjari na nchi jirani za Malawi na Msumbiji. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 86 ya Watanzania wanatumia mazao ya misitu ikiwemo kuni na mkaa kama nishati ya kupikia pamoja na matumizi mengine hivyo ni changamoto kwa serikali kutafuta njia mbadala zitakazowawezesha wananchi kupata nishati bila kutumia mkaa na kuni.

Kwa mujibu wa sera ya Taifa ya misitu ya mwaka 1998, Tanzania ina karibu hekta milioni 33.5 za misitu ambapo theluthi mbili ya hekta hizo ipo mashakani kutokana na ukosefu wa usimamizi mzuri hali inayosababisha watu kuvamia na kuharibu misitu.

Licha ya kwamba hakuna takwimu za kuaminika kuhusu kasi ya kutoweka kwa misitu, inakadiriwa kuwa hapa nchini ni kati ya hekta 130,000 hadi 500,000 za misitu zinafyekwa kila mwaka hali inayokatisha tamaa kwa sababu ukame na jangwa ni vitu ambavyo vinaweza kutokea iwapo hatua za kukabiliana hazitachukuliwa.

Mtaalam wa Maji kutoka Bonde la Ziwa Nyasa, Philip Kaduma anasema ili kutunza vyanzo vya maji inatakiwa kuacha kukata miti ovyo, kuacha kuchoma misitu; badala yake, ipandwe miti kila mwaka.

“Moto holela unaosababishwa na wachoma mkaa ni moja ya sababu za kuharibu vyanzo vya maji hivyo kuharibu uoto wa asili hali inayosababisha maji kukauka au kupungua baada ya miti inayohifadhi maji kwenye bonde kukauka,’’ anasisitiza mtaalam huyo.

Ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira, asasi ya Povert Alleviatio Organization (PAO) ya Songea imeamua kufanya mradi wa kutoa elimu ya mazingira kwa wananchi wa wilaya ya Songea vijijini ambayo inaongoza kwa vitendo vya uharibifu wa mazingira hasa ukataji wa miti ovyo.

Mratibu wa Shirika la PAO, Samweli Nyanguru anasema shirika hilo limedhamiria kutoa mchango wake katika kulinda, kutunza na kuhifadhi rasilimali ya ardhi, misitu na mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Hata hivyo anabainisha kuwa kwa kuanzia shirika hilo limeamua kuwajengea wananchi uwezo na uelewa kuhusu utunzaji wa mazingira . Walengwa ni wananchi kutoka kata ya Maposeni wilayani Songea, ambako kumeshuhudiwa uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu wilayani humo.

“Katika mradi huo tumehakikisha kuwa kila kijiji kinapanda miti zaidi ya 22,000 lengo ambalo pia limependekezwa na serikali ili kuhifadhi na kutunza mazingira,’’ anasema mratibu huyo.

Wananchi kutoka vijiji saba vya kata ya Maposeni wilayani Songea wameazimia kuanzisha mradi wa vitalu vya miti ili kuunga mkono serikali azma ya kuhifadhi na kutunza mazingira.

Sheria ya usimamizi wa mazingira namba 20 ya mwaka 2004 fungu namba 187 kwa makosa yanayohusu uchafuzi wa mazingira ya maji, hewa, ardhi na uchomaji misitu hovyo,inaagiza kuwa mtu yeyote akitiwa hatiani kwa makosa hayo atatozwa faini isiyozidi milioni 50 au kifungo kisichozidi miaka saba jela ama vyote viwili. Mwandishi ni Mchangiaji wa gazeti hili, mawasiliano yake ni Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona., simu 0784765917