Majaribio yafanywa muhogo ulimwe popote nchini

MUHOGO ni zao ambalo awali lilichukuliwa kuwa ni la chakula lakini hivi sasa, pia ni la biashara kutokana na matumizi yake mengine, ikiwamo kutengeneza wanga na nishati. Kampuni nyingine zimeonesha nia ya kuwekeza katika uzalishaji mkubwa wa zao hili.

Hivi sasa soko la muhogo kimataifa linatajwa kuwa kubwa na kwamba ndiyo maana Tanzania imesaini mkataba na China kwa ajili ya kufanya biashara ya zao hili. Nchi hiyo inataka kununua zao hili kutoka hapa nchini.

Mkataba huo wa kuuza bidhaa za muhogo, ulisainiwa mjini Bijing, China Mei mwaka huu. Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki alisaini kwa niaba ya serikali na kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mkuu mkuu wa taasisi ya udhibiti na ukaguzi wa mazao, Li Yuanping kwa niaba ya serikali ya China.

Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mikocheni (MARI), kupitia mradi unaofadhiliwa na Shirika la Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa ajili ya kuboresha zao hili, kinafanya majaribio ya aina 75 za mihogo katika maeneo mbalimbali nchini.

Lengo la majaribio hayo ni kupata aina itakayoweza kustahimili changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi kama vile ukame, baridi na ongezeko la joto. Mtafiti Mkuu Kituo cha Utafiti Mikocheni, ambaye ni Mratibu wa Mradi wa Kimataifa wa Muhogo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Malawi, Zambia na Msumbiji, Dk Joseph Ndunguru anasema gharama za mradi huo ni dola za Marekani 480,000 ambazo ni takribani Sh milioni 900 kwa miaka minne.

Dk Ndunguru ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa Uboreshaji Muhogo kwa ajili ya kukabiliana na changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi, Tanzania, Kenya na Hispania na Mratibu wa Utafiti wa Bayoteknolojia Tanzania, anasema hivi sasa aina hizo 75 za mihogo zinazofanyiwa majaribio lengo ni kupata aina ambazo zitastahimili baridi kali.

Anasema mbegu hizo zinazostahimili baridi kali zimepandwa wilaya ya Njombe katika kijiji cha Lupembe ambako kiwango cha baridi ni sentigradi 18. “Utafiti huu unafanywa kwa kushirikisha halmashauri ya Wilaya ya Njombe.

Mategemeo ni kwamba aina ya muhogo itakayofanya vizuri katika eneo hilo ambazo zitachaguliwa zitazalishwa kwa ajili ya wakulima wanaoishi ukanda wa baridi,” anasema Dk Ndunguru. Anataja maeneo ya ukanda huo wa baridi kuwa ni Njombe, Makete, Tukuyu mkoani Kilimanjaro pamoja na maeneo mengine yaliyoko katika ukanda wa baridi.

Anasisitiza kuwa mihogo itakayofanya vizuri itachukuliwa na wazalishaji kwa ajili ya kuboresha aina nyingine za mihogo. Dk Ndunguru anasema kwa ajili ya eneo la ukame, aina hizo hizo 75 zimepandwa katika eneo la Hombolo mkoani Dodoma ili kupata aina za mihogo inayostahimili ukame.

Aina hizo za mihogo zitazalishwa kwa wingi kwa ajili ya matumizi ya wakulima waishio maeneo yenye ukame; kama vile Dodoma, Singida na Shinyanga. Kwa mujibu wa Dk Ndunguru, aina hizo zimepandwa katika wilaya ya Bagamoyo kwenye Kituo Kidogo cha Utafiti Chambezi ili kubaini aina ambazo zitastahimili joto.

“Aina ambazo zitafanya vizuri zitazalishwa na kutumika maeneo yenye ukanda wa joto. Maeneo hayo ni Pwani ikiwemo visiwa vya Zanzibar, Pemba na Mafia,” anasema. Anasisitiza kuwa, utafiti kama huu unafanyika Kenya kwa kushirikiana na watafiti kutoka Hispania.

Mtaalamu na mtafiti huyo anasema, watafiti hao watatumia njia za bayoteknolojia ili kufupisha muda wa kuzalisha mbegu. Anaongeza kuwa kwenye utafiti huo unaoendelea pia wamewashirikisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Dk Ndunguru anasema hapa nchini tukisharuhusiwa matumizi ya uhandisi jeni (GMO), teknolojia hiyo itatumika kuhamisha jeni zinazosaidia muhogo kupambana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi ambazo zinaweza kupelekwa kwenye mazao mengine kuyapatia uwezo wa kustahimili ukame, joto na baridi.

Anasema kwa sasa changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi ni kubwa sana hivyo kama teknolojia ya uhandisi jeni ikianza kutumika kutakuwa na manufaa makubwa sana. Kwa sasa Tanzania hakuna bidhaa za teknolojia ya uhandisi jeni, ila utafiti unaendelea katika Kituo cha Utafiti Makutupora.

Pia mahindi yanayostahimili ukame yanafanyiwa utafiti pale. Utafiti huo unafanywa na mradi wa mahindi yanayostahimili maji (WEMA), uliopo Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

Kuhusu mradi huo wa WEMA ambao unatumia teknolojia ya uhandisi jeni, mapema mwaka huu ulitembelewa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba ambaye alisema serikali itaangalia upya taratibu na kanuni zilizopo kuharakisha tafiti za kilimo zinazofanyika nchini, zianze kufanya kazi kwa wakati.

Mradi huo upo Kituo cha Utafiti Makutupora mkoani Dodoma. Waziri alikiri kuwa teknolojia hiyo hapa nchini imechelewa kutokana na taratibu na kanuni zilizopo ambazo zinachelewesha kwani kwa ucheleweshwaji huo maarifa ya watafiti hayatafika mapema kwa walengwa.

Mbegu hiyo ya mahindi inayofanyiwa utafiti hapa nchini, tayari Afrika Kusini imeshaanza kutumika kwa wakulima na imeonesha mafanikio makubwa lakini kwa hapa nchini ili kukamilisha taratibu na kanuni itaanza kutumika mwaka 2021.

Utafiti huo wa Makutupora ndio utakuja na majibu yatakayoondoa sintofahamu juu ya teknolojia hii ikizingatiwa kwamba kumekuwepo na wanaoipinga. Watu binafsi na asasi mbalimbali zimekuwa zikipinga matumizi ya bayoteknolojia ya uhandisi jeni hapa nchini.

Historia ya muhogo Muhogo ulitokea Amerika ya Kusini na Kati na kuletwa Afrika na wafanyabiashara wa Kireno karne ya 16 na kufikia Afrika Magharibi. Karne ya 18 ulisambaa Afrika Mashariki, kisha India. Dk Ndunguru anasema maeneo ambako muhogo ulitokea, ndipo ambapo inapatikana mihogo pori inayofanyiwa utafiti nchini.

Umuhimu wa mihogo pori ni kwamba, inaweza kutumika kuboresha aina mbalimbali za mihogo. Kwa ujumla, majaribio hayo ya mbegu 75 yanayoendelea kufanywa na watafiti, yatakapowezesha kupatikana aina itakayoweza kustahimili changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi kama vile ukame, baridi na ongezeko la joto, ina maana itakuwa fursa kwa kila eneo la nchi kulima zao hili kwa ufanisi na kujipatia chakula na kipato.