Zama za tatizo la maji D’Salaam zinavyoishia

SEKTA ya maji ni miongoni mwa vichocheo vikubwa vya uwekezaji, hasa katika maendeleo ya viwanda ambapo Tanzania imeelekeza nguvu kubwa kufika uchumi wa viwanda.

Kwa kutambua hilo, Serikali imekuwa ikibuni na kutekeleza miradi mbalimbali ya maji ili kurahisisha shughuli za uwekezaji wa viwanda sambamba na kuboresha afya za wananchi kwa kuwa na uhakika wa maji.

Hivi karibuni Rais John Magufuli alizindua mradi wa upanuzi wa mtambo wa uzalishaji maji wa Ruvu Juu na ujenzi wa mabomba ya kusafirisha maji kutoka Ruvu Juu eneo la Mlandizi hadi Kimara, Dar es Salaam.

Rais alipongeza juhudi kubwa zilizofanywa na Wizara ya Maji katika kusimamia mradi huo. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Emmanuel Kalobelo anasema Mradi wa upanuzi wa mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu na ujenzi wa mabomba ya kusafirisha maji kutoka Mlandizi hadi Kimara, ni sehemu ya miradi mikubwa saba ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali.

Anasema lengo ni kuongeza uzalishaji maji kutoka lita milioni 300 za sasa hadi kufikia lita milioni 756 kwa siku ifikapo mwaka 2020. Anasema nyongeza hii ya uzalishaji wa maji itaboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam, Kibaha na Bagamoyo kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 72 hadi kufikia asilimia 95.

Anafafanua kwamba miradi ya kimkakati katika kufikia lengo hilo ni pamoja na ule wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini, upanuzi wa Mtambo wa Ruvu Juu, uchimbaji wa visima virefu vya Kimbiji na Mpera na Ujenzi wa bwawa la Kidunda.

Mkakati pia unahusisha upanuzi wa mtandao wa usambazaji maji katika maeneo yote yanayohudumiwa na mradi, kupunguza upotevu wa maji sambamba na uboreshaji wa mfumo wa mitandao ya majitaka.

Mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu umelenga kuongeza uwezo wa mtambo wa kuzalisha maji kutoka lita milioni 82 hadi lita milioni 196 kwa siku ili kukabiliana na kasi ya ukuaji wa miji ya Mlandizi, Kibaha na Jiji la Dar es Salaam.

Kalobelo anasema kazi zilizotekelezwa chini ya mradi huo ni pamoja na ukarabati wa kituo cha zamani cha kutoa maji mtoni kwenda kwenye mfumo wa uchujaji maji, ambapo pampu mpya sita zimefungwa, kila moja ikiwa na uwezo wa kusukuma lita milioni 53 kwa siku.

Idadi ya pampu zinazofanya kazi kwa wakati mmoja anasema ni kati ya tatu hadi nne kutegemea wingi wa maji mtoni. Pampu zingine ni za akiba. Pia anasema ukarabati wa kituo cha kusukuma majighafi kutoka Ruvu Darajani kwenda Mlandizi pia umefanywa ambapo pampu mpya nne zimefungwa na kila pampu ina uwezo wa kusukuma lita milioni 32 kwa siku.

Pampu tatu zinafanyakazi kwa wakati mmoja na pampu moja ni ya akiba. “Kituo kina uwezo wa kusukuma majighafi lita milioni 138 kwa siku. Kituo hiki kinafanya kazi sambamba na kituo cha zamani kinachozalisha wastani wa lita million 82 kwa siku. Hivyo, majighafi yanayosukumwa kutoka mtoni ni jumla ya lita milion 220 kwa siku,” anasema Kalobelo.

Aidha ujenzi wa bomba jipya la kusafirisha majighafi lenye kipenyo cha mita 1.2 na urefu wa km sita kutoka Ruvu Darajani hadi Mlandizi kwenye Mtambo wa kusafisha maji sambamba na ujenzi wa mfumo mzima wa kusafisha na kuweka dawa maji. Anasema kazi ya ujenzi wa tangi la kuhifadhia majisafi lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 10 umefanywa sambamba na ujenzi wa kituo kipya chenye pampu mpya sita cha kusukuma majisafi kutoka Mtambo wa Mlandizi kwenda Kimara kupitia tangi jipya la Kibamba.

Kila pampu ina uwezo wa kusukuma lita milioni 53 kwa siku. Pampu nne zinafanya kazi kwa wakati mmoja na pampu mbili ni za akiba. Mtambo huu unazalisha maji kwa wastani wa lita milioni 196 kwa siku pamoja na ujenzi wa nyumba 17 za wafanyakazi.

Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo anasema kazi nyingine iliyofanyika ni ujenzi wa njia mpya ya umeme kutoka Chalinze hadi Mlandizi ya msongo wa kilovoti 33 na urefu wa kilometa 45 ili kuongeza umeme wa kuendesha mitambo mipya ya maji pamoja na ufungaji wa transfoma mpya katika mitambo ya Ruvu darajani na Mlandizi.

Ili kusafirisha maji yaliyoongezeka kutoka katika mtambo wa Ruvu Juu kwenda Kimara, Serikali pia imetekeleza mradi wa ujenzi wa mabomba, tangi kipya la kuhifadhi maji na ofisi. Kazi zilizotekelezwa chini ya kandarasi hiyo ni pamoja na ujenzi wa bomba lenye kipenyo cha mita 1.2 na urefu wa kilomita 40 kutoka Mlandizi hadi Kibamba.

Pia ujenzi wa bomba lenye kipenyo cha milimeta 900, urefu wa kilomita 20 kutoka Kibaha Tanita hadi Kibamba, ujenzi wa tangi lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 10 eneo la Kibamba sambamba na ujenzi wa bomba lenye kipenyo cha mita 1.0 na urefu wa kilomita 10 kutoka Kibamba kwenye tangi jipya hadi Kimara.

Kalobelo anasema kukamilika kwa miradi hiyo tayari kumeanza kuimarisha huduma ya maji katika maeneo ya Mlandizi, Kibaha na vitongoji vyake, Kibamba, Mbezi, Kimara, Kinyerezi, Segerea na Tabata. “Maeneo haya yalikuwa na uhaba mkubwa wa maji na baadhi tayari yameanza kupata maji.

Baadhi ya mabomba ambayo kwa kipindi kirefu hayakuwa na maji, maarufu kama mabomba ya Mchina, sasa yanapata maji baada ya kukamilika kwa mradi huu. Kazi inayoendelea hivi sasa anasema ni ujenzi wa mfumo wa kusambaza maji, ukarabati wa mabomba machakavu na kuunganisha wateja.

Awamu ya Kwanza imeanza katika maeneo kati ya Kibaha na Mbezi hadi Kimara, na kati ya Bagamoyo na Changanyikeni. Aidha, mradi mwingine wa kimkakati ambao utekelezaji wake umekamilika, ni upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini na ujenzi wa bomba kuu la kusafirisha maji kutoka Ruvu Chini hadi Jijini Dar es Salaam ambapo hivi sasa kuna mradi mwingine unaoendelea wa uchimbaji wa visima virefu 20 vya Kimbiji na Mpera.

Kalobelo abasema hadi sasa uchimbaji wa visima 17 umekamilika na uchimbaji wa visima vitatu unaendelea na kwamba baada ya uchimbaji kumalizika, kazi itakayofuata ni ujenzi wa miundombinu ya kuyasafirisha maji kwenda kwa wananchi.

Kabolelo anasema mradi mwingine wa Kimkakati ni ujenzi wa Bwawa la Kidunda katika Wilaya ya Morogoro Vijijini ambalo litahifadhi maji ya kutosha wakati wa msimu wa mvua ili wakati wa kiangazi maji yafunguliwe na kutiririkia katika mto Ruvu ili kuwezesha mitambo ya Ruvu Juu na Chini kuwa na maji ya kutosha katika kipindi chote cha mwaka.

Anasema kwa sasa, wakati wa kiangazi maji ya mto Ruvu hupungua na hivyo uzalishaji maji kupungua pia, hatua ambayo huathiri huduma ya maji kwa wananchi. Endapo Bwawa hilo halitajengwa mapema, ni wazi kuwa hali inaweza kuwa mbaya kwani mahitaji ya maji ghafi yameongezeka baada ya upanuzi wa mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini.

Kalobelo anasema usanifu wa bwawa na utayarishaji wa makabrasha ya zabuni za ujenzi umekamilika. Gharama za ujenzi wa bwawa hili zinakadiriwa kufikia kiasi cha Dola za Marekani milioni 215