Kabudi: Miswada ya madini itatupa manufaa makubwa

“TUTAFAKARI mustakabali wa wapenzi wa Mungu ambao ni wananchi wasio na uwezo wa kujisemea. Tuweke maslahi ya Watanzania wa kawaida na wala si maslahi ya sisi ambao Mungu ametupa angalau cha kuingiza mdomoni.

Tuwakumbuke wale ambao hawana hata kidogo cha kuingiza mdomoni…” Maneno hayo yanayopaswa kuandikwa kwa wino wa dhahabu yanasema Waziri wa Katiba na Sheria, Palamagamba Kabudi, kabla ya kuwasilisha miswada miwili (kati ya mitatu) kwenye kamati ya pamoja ya Bunge.

Hii ni miswada ambayo imeanza kujadiliwa jana Bungeni baada ya kuwasilishwa kwa hati ya dharura na kukumbana na upinzani huu na ule. Anapowasilisha Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili kwa mwaka 2017 kwenye Kamati ya Pamoja ya Bunge, Waziri Kabudi anasema chimbuko la muswada ni Katiba kwamba inaweka masharti yanayohusisha misingi iliyomo katika Katiba ya mwaka 1997.

Pia anasema mikataba inahusisha pia misingi ya sheria mbalimbali za kimataifa ambazo zinatambuliwa na ambazo Tanzania imeridhia. “Sheria inayopendekezwa katika muswada huu na misingi yake iko katika Ibara ya 8, ibara ndogo ya 1 ya Katiba ambayo inaweka masharti kuwa Tanzania ni nchi inayozingatia msingi wa kidemokrasia na haki ya kijamii. Kwa msingi huo, wananchi wake ndio msingi wa mamlaka yote ya nchi na serikali inawajibika kwa wananchi wake.

Hii ni kwa sababu mwisho wa siku mamlaka yote yawe ya serikali, bunge au mahakama yanatoka kwa wananachi,” anasema. Anasema Tanzania kama nchi yenye uhuru wake kamili ina haki na mamlaka ya kusimamia rasilimali, maliasili na utajiri wake, hivyo serikali ina wajibu wa kulinda maslahi ya wananchi katika mikataba yote inayoingia kama inavyosema Ibara ya 27. Kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.

“Hii inatupa wajibu kizazi hiki cha sasa kuitumia na kuisimamia mali hii sio kwa faida yetu sisi, lakini pia kwa kuzingatia maslahi ya vizazi vijavyo. Hatuwezi kutumia maliasili hizi na utajiri huu kama sisi ndio wa mwisho kuishi katika nchi ya Tanzania na ndio maana tunalileta hili. Anasema pia Ibara ya 9, inaelekeza shughuli za serikali ni kuhakikisha utajiri wa taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na kutumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine.

“Tumeanza na ibara tatu za Katiba ni kuonesha kwamba haya tunayoleta mbele yenu (miswada) sio ya uzushi ni mambo ambayo misingi yake ilishawekwa kwenywe Katiba, tunachofanya ni kutamka na kujipa wajibu wa kuyaheshimu na kuzingatia tunapochukua maamuzi yote yanayohusu rasilimali na mali zetu ambazo ni mali zetu za pamoja.

“Ni katiba ambayo mwasisi wa taifa hili, Baba wa Taifa (Mwalimu Nyerere) alihakikisha nchi hii ambayo yeye kwa miaka 23 alikuwa anaiongoza anaiacha katika misingi ya haki za binadamu. Hivyo tunatakiwa kuhakikisha tunajadili maliasili na rasilimali sio kwa faida yetu ila kwa vizazi vijavyo na tutaaniwa tukifanya kwa faida yetu.

Anaongeza: “maliasili hizi tunazozungumzia nyingi, zikiondoka zimeondoka, madini ukiyachimba yamekwenda hayaoti tena gesi haiongezeki, lakini hii ni mali ya pamoja kwa walio hai na watakaozaliwa baadae.”

Anasema mambo yaliyozingatiwa ni pamoja na kutoka katika sheria za kimataifa ambazo Tanzania imesaini ikiwamo Azimio la Umoja wa Mataifa ambalo linaruhusu nchi kuwa na haki katika kusimamia na kutumia rasilimali kwa ajili ya maendeleo na haki ya kutatua migogoro kisheria. “Tunaleta kitu mbele yenu ambacho kina mashiko, kwa hiyo hatuendi kinyume na katiba yetu hatuendi nje ya misingi ya sheria za kimataifa.

Hatua zinazopendekezwa zinalenga kulinda mali na rasilimali za taifa na kuondoa aina yoyote ya upotevu au ubadhirifu wa rasilimali za nchi.” Muswada umegawanyika katika sehemu tatu ikiainisha masharti ya utangulizi, msingi katika kuhakikisha rasilimali za taifa zinatambuliwa na kulindwa huku sehemu ya tatu ikitambua na kulinda mamlaka ya Jamhuri ya Muungano juu ya rasilimali na inampatia mamlaka waziri mwenye dhamana ya sheria hii kutunga kanuni kwa ajili ya utekelezaji madhubuti wa sheria.

Muswada wa pili wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa mwaka 2017. Kabudi anaendelea kusema: “Kwa kutambua wajibu wa Bunge kama chombo cha uwakilishi, sheria imelipa nguvu Bunge kupokea taarifa ya mikataba yote inayohusiana na maliasili ya nchi, ili kujiridhisha kuwa masharti ya nchi yaliyomo kwenye mikataba hiyo yamezingatia maslahi ya Watanzania na Taifa kwa ujumla na kuishauri serikali.

“Baada ya kubaini kuna masharti hasi katika mikataba, Bunge linaweza kuitaka serikali kufanya majadiliano upya na upande wa pili wa mkataba.” Timu ya wataalam ambayo iliundwa kufanya kazi hii na Rais John Magufuli anasema ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (taaluma), Profesa Florence Luoga ambaye amebobea katika sheria za kodi, mikataba ya uwekezaji na biashara za kimataifa, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Kasimiri Sumba, Saidi Kalunde kutoka Mkurugenzi wa Sheria katika Wizara ya Nishati na Madini na Honorius Njole, mkurugenzi wa sheria kutoka mamlaka ya usimamizi wa hifadhi za jamii.

Kuhusu muswada wa tatu wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017, Kabudi anasema lengo ni kuwezesha wananchi na Taifa kunufaika na maliasili ya madini, Petroli na gesi asilia na kuimarisha mifumo ya udhibiti, uwajibikaji na kupanua wigo wa makusanyo ya kodi katika sekta ya madini na petroli. Anasema marekebisho katika Sheria za Kodi na Bima yanalenga kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato yanayohusiana na sekta ya madini na Bima.

“Muswada huu umebadilisha vifungu vya Sheria kwa kufuta baadhi ya vifungu vya Sheria husika hizi na kuviandika upya, pia baadhi ya maneno kwenye vifungu vya sheria, kuongeza maneno mapya na kuongeza vifungu vipya.

Sheria zinazopendekezwa kurekebishwa kupitia Muswada huu ni Sheria ya Madini, Sura ya 123, Sheria ya Petroli, Sura ya 392, Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332, Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura ya 148, Sheria ya Bima, Sura ya 394 na Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura ya 438.

“Mabadiliko yatatambua na kuweka umiliki wa madini, petroli na gesi asilia kwa wananchi chini ya usimamizi wa Rais kwa niaba ya Wananchi tofauti na ilivyokuwa hapo awali. Kadhalika mabadiliko yataipa serikali umiliki na mamlaka ya mazao yote yanayopatikana katika uchimbaji, uchakataji na uchenjuaji wa madini, ikiwa ni pamoja na ‘makinikia’.

Anafafanua kwamba Serikali itakuwa na haki na dhamana juu ya makinikia na kuweka utaratibu wa kuyahifadhi sehemu maalumu migodini, kuweka chini ya uangalizi wa Serikali maeneo yote ya uchimbaji wa madini na kuwepo kwa ulinzi mahsusi wa maeneo yote ya uchimbaji wa madini.

Pia anasema mabadiliko yataweka utaratibu wa Serikali kufanya ukaguzi na udhibiti wa uzalishaji wa madini, uwezo wa kudhibiti na kutambua viwango vya madini yanayotolewa kwenye maeneo ya migodi na uwezo wa kufanya majadiliano na kupitia upya baadhi ya masharti kwenye mikataba iliyokwishafanyika.

Anasema muswada pia unatoa fursa ya kupunguza madaraka ya waziri na kamishina wa madini kwa kupunguza baadhi ya majukumu na kuyahamishia kwa Kamisheni ya Madini itakayoanzishwa.

Kingine ni kuanzishwa kwa Hifadhi ya Dhahabu na Vito chini ya Benki Kuu na maghala ya serikali ya kuhifadhia madini na kuanzisha maeneo maalumu ya masoko ya dhahabu na vito na kuanzisha mfumo mahsusi wa kukusanya na kuhifadhi taarifa zote za shughuli za madini.

Kupitia miswada hiyo pia mfumo wa udhibiti na usimamizi wa shughuli za uzalishaji utaimarishwa sambamba na uchenjuaji na usafirishaji wa madini na kuweka utaratibu kwa wanaojihusisha na uchimbaji madini kula kiapo cha uadilifu.

Pia unalenga kuweka utaratibu wa mafunzo na mfumo utakaosaidia kuhamisha teknolojia ya uchimbaji wa madini kwenda kwa Watanzania na kuweka utaratibu bora wa kulinda mazingira kwenye shughuli za madini.

Miswada inalenga kuweka misingi ya Bunge kupitia, kujadili na kuridhia mikataba ya utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia sambamba na kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya kuboresha madini hapa nchini.

Maoni ya wadau Wadau waliojitokeza kutoa maoni wamelishauri Bunge kujadili na kupitisha miswada ambayo itawasharikisha kikamilifu Watanzania kwenye biashara ya madini na kuhakikisha nchi inanufaika na maliasi zake.

Wadau wengi walibainisha kuwa sheria za sasa za madini na maliasili hazisaidii taifa na Watanzania kwa ujumla. Mkurugenzi Mtendaji wa Timu ya Wanasheria watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), Dk Rugemeleza Nshala, anataka serikali kujiondoa kwenye mikataba ya MIGA ambayo inataka migororo ya mikataba ikaamuliwe kwenye mahakama za kimataifa na badala yake mashauri hayo yafanyike hapa nchini.

“Najua kuwa suala la kujitoa kwenye MIGA na ICSID haitachukua chini ya miaka mitano kukamilika lakini ni vyema kujitoa kwani mahakama zetu zina uwezo wa kufanya maamuzi katika kesi za madini,” anasema. Akizungumzia kuhusu kuundwa kwa Kamisheni ya madini, Nshala anasema pamoja na mabadiliko kuondoa madaraka ya waziri katika kujadili mkataba ya madini lakini haioneshi ni nani ambaye atajadili.

Naye, Rais wa Shrikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa madini (FEMATA), John Bina anasema ni vyema madini ya Tanzanite yakaundiwa sheria yake pekee ili kuyalinda. Pia anasema sheria zinazofanyiwa marekebisho vyema zikatambuwa wachimbaji wadogo. Bina pia ametaka katika marekebisho yanayofanywa yaangalie pia namna ya kupunguza ukubwa wa maeneo wanayopewa wawekezaji wakubwa na kuongeza muda wa umiliki kwa wachimbaji wadogo.

Anataka pia marekebisho hayo yaangalie na kubainisha madini ambayo wawekezaji kutoka nje wanatakiwa kuwekeza. “Ielezwe wazi ni madini gani ambayo wawekezaji wa nje wanatakiwa kuwekeza na yake ni yale ambayo sisi hatuwezi kuyachimba, lakini sasa cha ajabu kuna wawekezaji kutoka nje wamewekeza hadi kwenye uchimbaji wa kokoto,” anasema, Naye mtaalamu wa sheria wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico), Mudrikat Kiobya, anasema sheria mpya zinatakiwa kusema kwamba hisa za serikali katika sekta ya madini zinatakiwa kusimamiwa na shirika hilo kwani kwa sasa hisa za serikali hazina msimamizi anayemtabuliwa kisheria.

“Tungependa serikali ikaimarisha Stamico ili iwe na uwezo wa kufanya shughuli zake na kuhakikisha inatetea maslahi ya taifa,” anasema. Anasema ni muhimu sana sheria ikasema ‘ni lazima serikali iwe na hisa kwenye madini na kuwa kifungu hicho kitake kuwapo wawakilishi kwenye shughuli za uzalishaji na za utawala.’

“Ningeweza kusema ni vyema Serikali ikabaki kupata mirahaba, kuliko kuwa na hisa, kwani bila kuongezea kifungu cha kumlazimisha mwanahisa kuingiza kwenye shughuli za uzalishaji wanahisa hao (serikali) wanaw