Wafaransa wachagua chama kipya na kuvikataa vikongwe

KATIKA uchaguzi uliofanyika nchini Ufaransa, Juni 18 mwaka huu, matokeo yake ni kuibuka kwa chama cha Rais Emmanuel Macron (La République en Marche - REM - yaani Jamhuri inasonga mbele) ambacho kimenyakua viti 295 kati ya jumla ya viti 577 katika bunge la nchi hiyo.

Chama cha MoDem (Democratic Movement) ambacho kinashirikina na kile cha Macron kimepata viti 41 Macron ameunda chama cha REM mwaka mmoja uliopita. Yeye ni “kijana” wa miaka 39 aliyekuwa waziri katika chama cha Socialist kabla ya kujitoa na kuunda chama chake. Maana ya matokeo haya ni kuwa vyama hivyo viwili vikijumlisha viti vyao vitakuwa na viti 336.

Hivyo wataweza kuunda serikali ya mseto wakati Macron tayari akiwa ameshinda uchaguzi wa rais . Halafu kuna chama cha Republican ambacho kimepata viti 112 kikifuatiwa na chama cha Socialist ambacho kimepata viti 30 na Communist kimepata viti 10.

Chama cha National Front kinachoongozwa na Marine Le Pen kimepata viti vinane na chama cha Unsubmissive France (Ufaransa Ngangari) kinachoongozwa na Jean-Luc Melenchon kimepata viti 17 Matokeo haya yanamaanisha kuwa vyama vya muda mrefu vya mrengo wa kulia (Republicans) na kushoto (Socialist) pamoja na Communist vimeporomoka kwa kupata viti vichache na badala yake chama kipya cha Macron kimetia fora.

Hii imefanyika katika uchaguzi wa bunge na wa rais ambapo Macron ameshinda Kabla ya uchaguzi chama cha Socialist kilikuwa kinaongoza serikali kwa muda wa miaka mitano chini ya Rais Holland, nacho kilipata pigo kubwa. Ikabidi kiongozi wake, Jean-Christophe Cambadélis aachilie uongozi wa chama Kitu kingine ni kuwa idadi kubwa ya wananwake walichaguliwa.

Hivyo bunge litakuwa na wabunge wanawake 223 ikiwa ni asilimia 38.65 ya wabunge wote. Hii haijawahi kutokea. Pia kutakuwa na idadi kubwa ya wabunge waliochaguliwa kwa mara ya kwanza, takriban asilimia 75. Hii inaashiria kukataliwa kwa vyama vya zamani na wabunge wa zamani na kuibuka kwa wabunge wapya Tukizungumzia uchaguzi wa Ufaransa kura inapigwa pia katika makoloni yake ambayo wao wanadai ni sehemu ya Ufaransa.

Hivi ni visiwa vya Mayotte (Comoro), Papeete, Tahiti na Polynesia Ni vizuri tukajua kuwa katika uchaguzi huu ni asilimia 43 tu ya waliojiandikisha walijitokeza na kupiga kura. Katika duru ya kwanza asilimia 49 walijitokeza. Hivyo duru ya pili hali ilikuwa mbaya zaidi. Ushiriki ulikuwa mdogo zaidi katika maeneo wanakoishi watu wenye kipato cha chini.

Hali hii imekuwepo hata katika chaguzi zilizopita, kwani hamasa ya kupiga kura imekuwa ikipungua katika muda mrefu Sababu moja ni kuwa wananchi walipoteza imani na wanasiasa kwa ujumla. Rais wa Ufaransa aliyeondoka madarakani, Francois Hollande, alikuwa wa chama cha Socialist lakini wananchi wengi hawakupendezewa na utendaji wake. Alishindwa hata kuomba duru ya pili. Hii haijawahi kutokea katika muda wa miaka 60 Macron aliwahi kuwa waziri wake.

Ingawa alijitoa na akaunda chama chake, lakini bado wananchi hawakuona tofauti kubwa baina yao. Ingawa Macron wakati wa kampeni alionekana akitumia baiskeli katika mitaa ya Ufaransa bado hakupata ushindi wa sunami au wa kishindo Hata kampeni ya miezi saba haikusaidia kuwahamasisha wananchi kujitokeza. Wananchi walioulizwa sababu ya kutopiga kura walisema: “Kuna umuhimu gani wa kupiga kura?

Kwanini tujisumbue? Kwanza hao wabunge wakishachaguliwa wanaangalia zaidi maslahi yao na kujipa mishahara minono.” Katika utafiti uliofanywa na Kitivo cha Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu, Desemba 2016, asilimia 70 ya Wafaransa walisema kuwa demokrasia haifanyi kazi ya kuridhisha nchini humo. Ni asilimia 11 walisema wana imani na vyama vya siasa Asilimia 56 walisema hawaziamini kampuni za matajiri na asilimia 55 hawaamini mfumo wa mahakama.

Asilimia 41 walisema mfumo wa kibepari unapaswa kufanyiwa mageuzi makubwa, wakati mwaka uliotanguliwa ni asilimia moja tu walisema hivyo Utafiti mwingine ulioendeshwa na asasi iitwayo Generation What? Ulionesha kuwa asilimia 62 ya vijana wanaamini kuna haja ya kufanyika kwa mapinduzi makubwa Na ndipo tunaona shirika la habari la Reuters likiripoti kuwa siku ya uchaguzi watu 141 walikamatwa na polisi jijini Paris.

Mamia ya askari walitumika kuwadhibiti waandamanaji waliobeba mabango yakisema “huu ni uhuru wa kuchagua kati ya ukoma na kipindupindu”. Macron alilaani maandamano hayo akisema serikali yake itaajiri askari wapya 10,000 na jeshi la polisi litapewa uwezo zaidi wa kuwakamata na kuwafunga watu bila vikwazo vya kisheria. Hiyo ni ahadi ya Macron Wakati wa kampeni, Macron pia aliahidi mambo kadhaa.

Muhimu zaidi ni kuwa anakusudia kubadili sheria ya ajira, kupunguza wafanyakazi serikalini na kurekebisha mafao ya wastaafu. Anakusudia kubadili sheria ya ajira ili kurahisisha kwa muajiri kumfukuza kazi mfanyakazi wake Aliahidi pia kuwekeza zaidi katika mafunzo ya kazi na katika nishati endelevu yaani inayotumia miali ya jua na upepo Rais Macron aliwahi kufanya kazi katika benki na kwa hivyo anatarajiwa kuelewa jinsi uchumi wa nchi unavyoendeshwa.

Ni Rais mwenye umri mdogo kushinda marais waliomtangulia. Ameahidi kusafisha siasa ya nchi na kubadili uchumi wa Ufaransa katika Umoja wa Ulaya (EU). Katika umoja huo Ufaransa inashika nafasi ya pili kiuchumi ikitanguliwa na Ujerumani. Si ajabu mara tu baada ya kushinda urais ziara yake ya kwanza ilikuwa nchini Ujerumani kuonana na Kansela wa nchi hiyo, Angela Merkel ambaye alimuunga mkono wakati wa kampeni.

Sasa wakuu hawa wawili wanategemewa kufanya mabadiliko katika muundo na katiba ya EU. Uchaguzi ulifanyika wakati uchumi wa Ufaransa umekuwa ukiyumba tangu mwaka 2007/8 wakati uchumi ulipoporomoka katika nchi za Ulaya. Ufaransa ikaachwa nyuma na Ujerumani. Mwaka 2016, wakati uchumi wa Ujerumani ulipokua kwa kiwango cha asilimia 1.9 Ufaransa ilikua kwa asilimia 1.1 Tangu kuanza kwa sarafu ya Euro mwaka 1999, bei za hisa nchini imeanguka kwa asilimia 27 wakati Ujerukani imeanguka kwa asilimia 21.

Maana yake wawekezaji wamejikuta faida yao inayumba nchini Ufaransa na wakati huohuo asilimia 10 ya wafanyakazi wamejikuta hawana kazi. Hata hivyo Ufaransa imemudu kuendeleza huduma ya afya pamoja na mafao ya uzeeni. Pia muda wa kazi umebaki kuwa saa 35 kwa wiki. Kutokana na haya Ufaransa imekuwa ikiongoza nchi nyingi za Magharibi.

Lakini chini ya Rais François Hollande na chama chake cha Socialist (PS) mambo hayakwenda vizuri kwa wafanyakazi, hasa pale alipopitisha sheria za kubana matumizi ya afya na malipo ya uzeeni. Macron akiwa waziri wa uchumi chini ya chama cha Socialist, alisimamia sheria iliyoathiri wafanyakazi kwa kupunguza ujira wa kazi ya ziada (ovataimu) na kuwapa waajiri uwezo wa kuwaajiri na kuwafukuza wafanyakazi bila ya masharti.

Matokeo yake ni kuwa, mnamo mwaka 2016/17 asilimia 86 ya wafanyakazi walikuwa ni vibarua bila ya mkataba wa kudumu. Asilimia 43 ya wasio na kazi walikuwa nje ya ajira kwa muda unaozidi mwaka mmoja. Hii ndiyo kazi inayomkabili Macron katika kuinua uchumi wa Ufaransa. Lakini pia kuna matumaini kuwa chini ya Macron nchi hiyo itageuza sera yake ya kigeni. Hivi majuzi alipohojiwa na waandishi alisema Ufaransa na marafiki zake inafanya kosa kubwa nchini Syria sawa na kosa la kuivamia Libya mwaka 2011.

Akasema haoni kuwa kumuondoa kijeshi Rais Bashar Assad nchini Syria ni jambo muhimu. Badala yake ni vizuri wananchi wa Syria wakafanya mazungumzo na kufikia muafaka Haya ni mabadiliko makubwa kwa Ufaransa ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kutumia majeshi yake duniani. Huko Libya ilikuwa mstari wa mbele kuongoza majeshi ya NATO katika kumpindua Gaddafi na kumuua kikatili.

Matokeo yake nchi ikaparaganyika na haitawaliki hadi leo Sasa Rais Macron anaungama kuwa Ufaransa ilifanya kosa Libya na inaendelea na kosa hilohilo nchini Syria. Labda angeongeza pia na Iraq, Afghanistan na Afrika Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona. +1 613 699 2933