Tambo za wagombea urais Kenya na ahadi lukuki

SIKU zinahesabika kwa Wakenya kabla ya kutumia haki yao ya kidemokrasia, kuchagua viongozi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 8 mwaka huu. Hiki ni kipindi ambacho wagombea wanazidi ‘kutunishiana misuli’ kwa tambo za kisiasa zinazolenga kuteka nyoyo za wapiga kura wawachague kuongoza taifa hili lililopo Afrika Mashariki.

Katika kinyang’anyiro cha urais, wagombea wanane ndio walioidhinishwa na Tume ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC) kuwania nafasi hiyo nyeti kwenye uchaguzi huo uliobakiza takribani siku 35 ufanyike. Zaidi ya watu 10 waliotaka kuwania urais, wameenguliwa na tume kwenye kinyang’anyiro hicho cha urais kutokana na kutotimiza vigezo.

Kwa hali hiyo, kazi imebaki kwa wagombea hawa wanane ambao kila mmoja anauza sera zake kwa kadri awezavyo ili kuufanya umma wa Wakenya umwelewe na kisha upige kura nyingi za ‘ndiyo’ aibuke kuwa rais.

Wagombea wanaochuana vikali ni wawili ambao ni Rais Uhuru Kenyatta anayewania muhula wa pili kupitia muungano wa Jubilee na Raila Odinga ambaye ni mgombea wa muungano wa vyama vya upinzani vinavyojiita Nasa (National Supper Alliance). Wagombea wengine na vyama vyao kwenye mabano ni Cyrus Jirongo (UDP), Ekuru Aukot (Thirdway Alliance) na Abduba Dida (ARC).

Wagombea binafsi ni Joseph Nyagah, Michael Wainaina na Japhet Kavinga. Hata hivyo, kama ilivyodokezwa hapo juu, ushindani mkubwa upo kati ya Rais Uhuru na Odinga. Itakumbukwa kuwa, kwa muda mrefu Odinga amekuwa akitoa upinzani kwa chama tawala lakini bila kutimiza ndoto yake ya kuingia ikulu. Hii itakuwa ni mara ya nne kwa Waziri Mkuu huyo wa zamani kugombgea.

Rais Uhuru katika kuendelea kuwashawishi Wakenya kumpa nafasi nyingine ya kuwaongoza katika muhula wa pili, ameanisha ilani ya chama chake cha Jubilee kuelekea uchaguzi huo mkuu.

Ahadi za Uhuru Amekaririwa na vyombo vya habari vya ndani na hata vya kimataifa akiahidi kuwa, serikali yake itaunda nafasi mpya za kazi milioni 6.5 kwa muda wa miaka mingine mitano atakayokuwa madarakani.

Ameeleza kuwa hili litafanyika kwa kuhakikisha kuwa anajenga kiwanda kimoja katika kaunti zote 47 nchini humo. Elimu katika shule za serikali za sekondari itakuwa bure huku akisisitiza kuwa, hakuna mwanafunzi atakayelipa ada ili kupata elimu. Uhuru ameahidi pia kuimarisha sekta ya afya kwa kupanua hospitali, kununua vifaa na kuinua kiwango cha tiba katika hospitali za serikali.

Wajawazito ni kundi ambalo limeahidiwa kuwa wataendelea kujifungua bure na kupata huduma muhimu bila malipo yoyote kama ambavyo ilani ya Jubilee inavyosema. Ilani hiyo ilizinduliwa wiki iliyopita jijini Nairobi. Mambo mengine ‘matamu’ ambayo Uhuru amewaahidi Wakenya ni kwamba, ikiwa atashinda, atajenga makazi 500,000 ya bei nafuu kote nchini.

Pia anasema atajenga mabwawa ya maji 57 kwa lengo la kuimarisha sekta ya kilimo. Ilani hiyo ya Jubilee inasema Uhuru akichaguliwa pia Wakenya wote wataunganishwa na nguvu za umeme kwa muda wa miaka mitatu ya uongozi wake.

Ahadi nyingine ni ya kujenga viwanja vipya vya kisasa vya michezo katika maeneo mbalimbali nchini humo. Lakini pia, anasema serikali yake inaimarisha usalama, kujenga reli ya kisasa na kuinua uchumi wa taifa hilo.

Odinga katika nyayo za JPM Miongoni mwa mambo ambayo mgombea huyu amekuwa akiwaahidi Wakenya kuwa atayatekeleza atakapochaguliwa kuwa rais ni pamoja na kusimamia ipasavyo katiba ya nchi hiyo katika kuhakikisha kuwa serikali za Kaunti zinafanya majukumu yao ipasavyo.

Kama ilivyo kwa mgombea wa chama tawala, pia Odinga ameahidi kuwa elimu kutoka kidato cha kwanza hadi cha nne itakuwa bure; ahadi itakayotekelezwa ndani ya mwezi mmoja baada ya uchaguzi (Septemba mwaka huu).

Jambo lingine ambalo upinzani kupitia kwa Odinga unasema utalifanyia kazi ni kuhakikisha kunakuwa na uwiano wa kitaifa katika uteuzi huku ukinyooshea kidole serikali ya Jubilee kwamba imekuwa haifanyi hivyo jambo linaloongeza ukabila.

Ahadi nyingine za upinzani ni kuunda nafasi za kazi hasa kwa vijana na pia kupambana na ufisadi. Kuhusu usalama, upinzani unasema utashughulikia kumaliza uvamizi wa kigaidi ulioshuhudiwa kipindi cha rais Uhuru Kenyatta.

Odinga katika kuomba ridhaa ya kuchaguliwa na Wakenya, hivi karibuni akiwa katika mkutano wa kampeni alioufanya katika eneo la Isebania lililopo kaunti ya Migori mpakani mwa Tanzania (Sirari), alijinadi bila kumung’unya maneno kuwa atafuata nyayo za Rais John Magufuli wa Tanzania.

Kupitia mkutano huo, Odinga alimpongeza Rais Magufuli kwa kutetea rasilimali za taifa na wakati huo huo kupambana na watumishi hewa, ufisadi na rushwa. Amewaomba wananchi kumpa kura na pia kuwachagua wagombea wa Nasa kwa maana ya madiwani, magavana na wabunge ili waondoe ufisadi nchini mwao.

“Uongozi wa Rais John Magufuli ni mfano wa kuigwa na viongozi wengine wa Afrika ambao ni wazalendo na nchi zao wanaotetea wananchi wao hususani wanyonge ambao ndio wengi; Wanaopambana na ufisadi kutoka moyoni mwao na mafanikio kuonekana.

“Nikifanikiwa kuwa rais nitafuata nyayo zake, nitamuomba anipe ufagio wa mafisadi niwafagie hapa Kenya. Hapa kwetu wananchi wamekuwa masikini, hakuna chakula, sukari na vitendo vya ufisadi viko juu. “Wananchi wanafananishwa na punda aliyebeba mzigo mkubwa ambao hauwezi.

Lazima huu mzigo wa Jubilee tuuteme na kuwapumzisha wananchi wetu. Mkinichagua wanafunzi watasoma bure hadi kidato cha nne,” alisema Odinga kwenye mkutano huo.

Uhuru na Odinga ambao wameonesha wazi walivyo na mchuano mkali huku harakati zao za kisiasa zikichambuliwa kuwa zinawakumbusha historia ya siasa kati ya baba zao; Jomo Kenyatta aliyekuwa rais wa kwanza na Jaramogi Oginga Odinga aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais baada ya uhuru mwaka 1963.

Tambo hizi za wagombea urais hawa ni fursa nzuri kwa wananchi wa Kenya kuwafahamu kabla ya kutoa ‘hukumu’ mwezi ujao kupitia sanduku la kura katika kuamua mustakabali wa taifa lao.