‘Kipaumbele cha mtoto wa Kimasai sasa ni elimu’

“UMASAI wa leo ni tofauti na tulikotoka kwa vile sasa unahubiri amani, kujikomboa kielimu na kujiletea maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi,” anasema Rebecca Lembile, Muuguzi Mwandamizi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro anayetoka katika jamii ya Kimasai.

Rebecca anatoa maelezo hayo kwenye mkutano wa siku tatu uliowashirikisha waumini wa madhehebu mbalimbali ya Kikristu wa ndani ya mkoa na nje ya nchi wa kabila hilo ulioandaliwa na Kanisa la Azusa wilayani Mvomero. Anasema kutokana na msingi huo, jamii ya Wamasai waliobahatika kupata elimu, hivi sasa wamejipa kazi ya kujitolea kuwatembelea wenzao walioko vijijini ili kuwahimiza kuwasomesha watoto wao kwani faida ya elimu ni kubwa katika karne ya sasa.

Muuguzi huyo ambaye pia ni mwezeshaji wa elimu inayohusu athari za ukeketaji kwa watoto wa kike wa jamii hiyo, anasema wanapokuwepo wasomi wengi ndani ya jamii yao ni moja ya fursa ya kuwawezesha kuajiriwa katika sekta ya umma. “Elimu ni chachu ya kubadili maisha ya Wamasai, familia na taifa kwa ujumla; kijamii na kiuchumi ili kwenda na mabadiliko ya kizazi cha sasa na kijacho,” anasema.

Akizungumzia uchache wa Wamasai katika sekta ya umma, anatoa mfano kuwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro yenye watumishi zaidi ya 600 wa kada mbalimbali, anayetoka jamii ya Kimasai ni mmoja pekee ambaye ni yeye. “Nimekuwa nikijitolea kwa kutumia siku za mapumziko kwenda kuwatembelea akina mama wa Kimasai vijijini ili kutoa elimu kuhusu faida ya kusomesha watoto wao,” anasema Lembile.

Anasema mwitikio umeanza kuwa mkubwa tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma na hilo linaleta faraja ya kuelekea kwenye mabadiliko ya kijamii na kiuchumi bila kuathiri mila, desturi na utamaduni wao.

Kiongozi wa kimila wa kabila la Kimasai, yaani Leigwanani wa kanda ya Mashariki inayojumuisha mikoa ya Morogoro, Pwani na sehemu za maeneo ya mikoa ya Iringa na Tanga, Dikikala Lopejo maarufu kwa jina la Mzee Sawasawa, anasema wakati mwingine akina mama wa jamii hiyo wanakuwa kikwazo kwa elimu ya watoto wao. Anasema akina mama wana jukumu muhimu la kuhakikisha watoto wanaandikishwa shule bila kukosa lakini wanashindwa kutekeleza jukumu hilo kwa uzembe na kutojua umuhimu.

Anasema yeye kama kiongozi wao hakuna mwana mama wa Kimasai aliyewahi kumshitaki mumewe kwamba anakwamisha mtoto asiende shule na kwamba kwa mujibu wa majukumu ya jamii ya Kimasai yalivyo ni lazima akina mama wabebe lawama hiyo. Leigwanani ni cheo kikubwa na kinachoheshimika sana katika kabila la Kimasai na huwa hakiombwi au kugombewa bali wazee wa kimila wa kabila hilo hukaa na kumchangua mtu wanayemwona anafaa kuwa kiongozi wao.

“Nikiwa kiongozi wa kimila wa kabila hili kwa ukanda huu wa mikoa ya mashariki nimetembelea maeneo ya wafugaji wa jamii yangu kuanzia Iringa, Tanga, Pwani na wilaya za Morogoro, sijaona wakisoma shule na wanaosoma shuleni ni wachache sana,” anasema akionesha masikitiko Lopejo. Anaongeza: “Hata hawa waliopo shuleni mahudhurio yao si mazuri. Wengi hawapo madarasani.”

Anawataka wanawake wa jamii ya Kimasai kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wao wenye umri wa kwenda shule wanapata fursa ya kuandikishwa na kuendelezwa. “Lazima mtoto wa Kimasai aandikishwe shule kuanzia darasa la awali, la kwanza na kumwendeleza ngazi ya sekondari hadi elimu ya juu itakayosaidia kuwaletea mabadilikio ya kijamii na kiuchumi,” anabainisha Lopejo.

Kiongozi huyo anajipa jukumu la kuhakikisha watoto wa jamii hiyo wanapata elimu kwani ni ukombozi mkubwa kwao kwa maisha ya sasa na baadaye. Kutokana na kuguswa na kilio cha Leigwanani Lopejo, mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe ametumia fursa ya kufunga mkutano huo wa siku tatu kuiasa jamii hiyo suala la elimu kwa watoto wao liwe la kipaumbele cha kwanza.

Ili kuhakikisha watoto wote walioandikishwa shule wanakuwa madarasani mkuu wa mkoa anapiga marufuku kwa jamii ya wafugaji kuwatumikisha watoto walio na umri wa kwenda shule katika shughuli mbalimbali ikiwemo za uchungaji wa mifugo. Dk Kebwe anasema, lengo ni kuwawezesha watoto hao wapate fursa ya elimu bure inayotolewa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Mkuu huyo wa mkoa anaonya wazazi na walezi ambao watabainika kuendelea kuwatumia watoto wao kuchunga mifugo badala ya kuwa shuleni kwamba mkono wa sheria vitawashughulikia ipasavyo. “Ndugu zangu jamii ya wafugaji wa Kimasai, kwenye suala hili la elimu mtanichukia. Ni bora mnichukie wakati ninasimamia watoto wapate elimu kwa manufaa yao na taifa kwa ujuma na hili hata Mungu atakuwa upande wangu,” anasema Dk Kebwe.

“Leigwanani wenu amewashitakia kwangu. Sasa akina mama ninawataka mbadilike. Wapelekeni watoto shule na msipofanya hivyo nanyi mtachukuliwa hatua za kisheria,” anabainisha Dk Kebwe. Baadhi ya wazee wa jamii hiyo kwa nyakati tofauti akiwemo Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji mkoa wa Morogoro, Longido Shambakubwa wanasema suala la elimu kwa watoto wao si la kupuuziwa tena katika karne ya sasa.

“Binafsi umuhimu wa elimu niliuona muda mrefu, nikawapeleka watoto wangu shule na sasa mmoja yupo nchini China akisomea shahada ya ufamasia. Elimu ni urithi mkubwa kwa watoto,” anasema Shambakubwa. Naye Adam Ole Mwarabu, mkazi wa wilaya ya Kilosa anasema mkakati wa sasa ni kuwawezesha vijana wao kielimu kwa vile ni elimu pekee itakayowawezesha kuendesha ufugaji bora wa kisasa.

“Elimu ni nguzo kuu na ni ufunguo wa maisha na hata Waziri mkuu wa awamu ya kwanza hayati Edward Moringe Sokoine alihimiza elimu kwa jamii ya Kimasai,” anasema Mwarabu.