Mradi wa umeme na uhifadhi wenye manufaa

HIFADHI ya Selous (tamka Saluu) ni kubwa kuliko zote nchini na pia ni kati ya hifadhi kubwa za wanyamapori zinazotambuliwa duniani. Hifadhi hiyo yenye eneo la kilomita za mraba 50,000 inapakana na mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Eneo hilo ni kubwa kuliko nchi 70 duniani ikikadiriwa kuwa na eneo sawa na nchi ya Kostarika (Amerika ya Kati) na takribani ukubwa mara mbili wa nchi za Rwanda, Burundi na Ubelgiji (Ulaya).

Kwa lugha nyingine, nchi za Rwanda na Burundi zikiunganishwa pamoja bado pori la Selous linabaki kuwa kubwa kwa eneo! Tangu mwaka 1982 hifadhi hiyo iliingizwa katika orodha ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) ya urithi wa dunia.

Jina la hifadhi hiyo linatokana na Mwingereza Frederick Selous aliyekuwa mwindaji wakati wa kuanzishwa kwa ukoloni katika Afrika ya Kusini na Mashariki na ambaye aliuawa hapa Tanzania wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Sehemu kubwa ya hifadhi hiyo iko katika hali ya asili bila kuvurugwa na shughuli za binadamu, ikiwa na utajiri mkubwa wa wanyamapori wakiwemo tembo, vifaru, simba, twiga, viboko na mamba.

Hivi karibuni Rais John Magufuli alikutana na timu ya wataalamu wa masuala ya umeme na ujenzi wa miundombinu ya mabwawa ya maji kutoka Ethiopia kujadili mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa maji hapa nchini. Rais alikutana na wataalamu hao kujadili namna ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji maarufu kama Stiegler’s Gorge Power Project.

Mradi huu utakuwa katika Pori la Akiba la Selous na utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,100 za umeme. Nia ya rais ambayo ilikuwepo tangu zama za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ni kuzalisha umeme mwingi utakaosaidia kuharakisha maendeleo hapa nchini, mintarafu suala zima la ujenzi wa viwanda.

Katika kuunga mkono dhamira hiyo njema ya Rais Magufuli, Wizara ya Maliasili na Utalii imewataka wadau wa uhifadhi kote nchini kuunga mkono mpango wa Serikali wa kujenga mradi huo wa uzalishaji umeme wa maji katika mto Rufiji kwenye pori la akiba la Selous.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Gaudence Milanzi anasema utekelezaji wa mradi huo wa umeme ni wa muhimu kwa taifa kwani utasaidia kuharakisha maendeleo kupitia uchumi wa viwanda utakohitaji umeme wa kutosha na wa uhakika.

Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya wiki sita ya askari wa wanyamapori 98 kutoka Mamlaka yaUsimamizi wa Wanyamapori Tanzania- (TAWA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA), Milanzi anasema mradi huo wa umeme pamoja na mradi wa bwawa la maji la Kidunda vitachukua eneo dogo sana la pori hilo kubwa.

Mafunzo hayo ya wiki sita ya kijeshi yalifanyika katika Kituo cha mafunzo cha Mlele kilichopo katika Pori la Akiba la Rukwa –Lwafi lililopo katika wilaya ya Mlele mkoani Katavi.

Anasisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huu mkubwa wa kuzalisha nishati ya umeme hautaathiri mazingira ya Pori la Akiba la Selous kama ambavyo wengine wanaweza kufikiri. Anasema ujenzi wa miradi hiyo hauna tafsiri kwamba Tanzania haithamini masuala ya uhifadhi bali unazingatia uhifadhi wenye manufaa kwa jamii na maendeleo ya taifa.

Anaongeza kwamba Tanzania inatambua umuhimu wa uhifadhi na ndiyo maana imetenga zaidi ya asilimia 28 ya eneo lote la nchi kavu (Tanzania bara) kwa ajili ya uhifadhi wa aina mbalimbali ukiwemo wa wanayamapori, misitu na vyanzo vya maji ambayo ni muhimu kwa shughuli za kijamii na kiuchumi. “Ni nchi chache sana duniani zenye eneo kubwa la uhifadhi kama Tanzania,” anasisitiza Katibu Mkuu.

Ni kwa msingi huo, Milanzi anawataka wafanyakazi wa wizara yake na watanzania kwa ujumla kutokuwa kikwazo katika utekelezaji wa mradi huo na kwamba wadau wanaotaka kuisaidia Tanzania wasaidie kuhakikisha inatumia maliasili zake kupiga hatua za maendeleo.

Anatoa mfano wa nchi ya Qatar ambayo ilikuwa na eneo la uhifadhi likiwa na baadhi ya viumbe adimu kama mnyama Oryx, lakini walipogundua mafuta, waliamua kujitoa kwenye urithi wa dunia ili wachimbe mafuta na kuinufaisha nchi hiyo na maendeleo ya wananchi wake.

Akizungumzia tatizo la mifugo kwenye maeneo ya hifadhi, Katibu mkuu huyo anawataka wahifadhi kuhakikisha wanakabiliana na changamoto hiyo na kusimamia sheria zilizotungwa na Bunge ambazo zinakataza mifugo kuingia hifadhini.

Anasema Serikali ikisaidia na wadau mbalimbali inatumia fedha nyingi kugharamia mafunzo ya askari wa wanyamapori na wahifadhi ili kuwaongezea ujuzi na weledi wa kulinda maliasili za taifa kwa kuzingatia sheria zilizopo.

Milanzi pia ameeleza umuhimu wa kuhakikisha mapori ya hifadhi yanatumiwa kwa uhifadhi badala ya mambo mengine ikiwemo kilimo cha bangi na maficho ya majambazi na majangili.

Ni katika muktadha huo amewataka wahifadhi na askari kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuwafichua wahalifu wanaojificha kwenye mapori hayo na kufanya ujangili na uhalifu mwingine.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Martin Loibooki, anasema mafunzo hayo yamesaidia kuimarisha uhifadhi kwenye mapori mbalimbali ya akiba nchini na maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori.

“Ulinzi wa rasilimali za wanyamapori umeendelea kuimarika ndani na nje ya nje ya mapori ya akiba na tengefu sambamba na kumarisha ukaguzi wa nyara za Serikali katika maeneo ya mipakani kwa kushirikiana na wadau wengine,” anasema.

Anawashukuru wadau mbalimbali wa uhifadhi wa ndani na nje ya nchi wanaofadhili mafunzo hayo na vitendea kazi, juhudi ambazo anasema zimeanza kuzaa matunda ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya tembo na wanyamapori wengine.

“Mamlaka hii imeungwa mkono na wawekezaji zikiwemo kampuni za uwindaji wa kitalii, mashirika ya kimataifa na taasisi mbalimbali ambazo zimetoa michango ya kusaidia uhifadhi,” anasema.

Anataja baadhi ya mashirika hayo kuwa ni pamoja na World Wildlife Fund (WWF) ambalo limetoa ndege nane zisizo na rubani na United States Agency for International Development (USAID) ambalo limedhamini mafunzo ya kupambana na ujangili kwa watumishi 90 wa Hifadhi ya Rungwe.

Mashirika mengine ya kitaifa yaayosaidia uhifadhi ni pamoja na Frunkfurt Zoological Society (FZS) ambalo limechangia magari kumi ya doria na vifaa mbalimbali vya doria. Mafunzo hayo yaliyowashirikisha askari wa wanyamapori wapatao 98 wa TAWA na NCCA ni mwendelezo wa mafunzo yanayotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa askari wa wanyamapori na watumishi wengine wa wizara hiyo baada y