Tanzania inavyoweza kunufaika na Mkanda mmoja, Njia moja

NCHI nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania zimekuwa na mkakati wa kujitegemea ili kuondokana na utegemezi wa misaada kwa wahisani katika kutekeleza miradi ya maendeleo, matumizi ya kawaida na kujijengea uwezo katika masuala mbalimbali.

Hili ni jambo analopigania Rais John Magufuli tangu alipoingia madarakani huku kichwani akiwa na mipango na vipaumbele vingi ambavyo utekelezaji wake utaisukuma mbele nchi yetu. Hata hivyo, hazina yetu bila shaka inakabiliwa na madeni ya ndani na nje pamoja na mahitaji ya kila siku, kiasi kwamba haitoshi kutekeleza malengo yaliyopo licha ya mikakati mizuri inayofanyika ya kubana matumizi, kukusanya kodi na kuziba mianya inayotorosha mapato ya serikali.

Ni katika mazingira kama hayo, Dk Cheng Cheng wa Chuo Kikuu cha Watu wa China (Renmin) kilichoko Beijing, anasema Afrika ina mahala pa kukimbilia ambako ni China inakoweza kupata mikopo isiyo na masharti magumu.

Masharti magumu yanaweza kuwa kulazimisha nchi zinazoomba mikopo kufanya mambo hata yasiyokubaliana na tamaduni zao kama vile kubariki vitendo vya ushoga na mengine kama vile kuambiwa kwamba hamkufuata demokrasia uchaguzi wa Zanzibar wakati baadhi ya wagombea walisusa wenyewe kushiriki uchaguzi wa marudio.

Dk Cheng aliyasema hayo kwa waandishi wa habari waandamizi 35 kutoka nchi 10 za Afrika, waliokuwa wakishiriki kwenye semina ya wiki mbili, jijini Beijing, China, mwezi uliopita. Kwa mujibu wa Dk Cheng, njia rahisi ya Afrika kushirikiana na China kwa utaratibu wa kila upande kunufaika ni kupitia mpango wa Belt and Road Initiative (B&R) unaoitwa pia ‘Mkanda mmoja, njia moja’ (One Belt One Road).

Mpango wa B&R ni nini hasa? Dk Cheng anasema Belt and Road Initiative ni mpango wa kuiunganisha China na nchi zingine kiuchumi ulioasisiwa na Rais wa China, Xi Jinping mwaka 2013 akiutangaza kama kielelezo cha ushirikiano mpya utakaochochea maendeleo ya pamoja na mafanikio ya kila upande. Ni mpango ambao umekuwa muhimu zaidi katika mwelekeo wa sera za kigeni za China.

Dk Cheng anasema: “Ni mkakati mkubwa wa kiuchumi ulio huru unaohusisha ugawaji bora wa rasilimali na ushirikiano mkubwa unaounganisha soko la China na ya mabara ya Asia, Ulaya na Afrika.” Ni mpango unaolenga kwamba ifikapo mwaka 2050 uwe umechangia asilimia 80 ya ukuaji wa pato la taifa la nchi zitakazokuwa zimejiunga nao. Kadhalika, Dk Cheng anasema hadi muda huo, watu zaidi ya bilioni tatu watakuwa wamewezeshwa kutoka maisha ya chini hadi ya kati.

”Ni mpango ulio wazi kwa nchi zote na mashirika ya kimataifa na ya kikanda katika kushirikiana na China kwa njia ya kuheshimiana katika kutafuta maendeleo ya kila upande,” anasema Cheng. B&R na Afrika Akizungumzia namna mpango huo unavyoweza kunufaisha nchi za Afrika ikiwemo Tanzania, Dk Cheng anasema utasaidia kuimarisha miundombinu na hivyo kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji na hivyo kusisimua uchumi wa nchi husika.

Pili, anasema ni mpango unaozipa nchi za Afrika njia mbadala ya kupata fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo isiyo na masharti magumu kama yanayotolewa baadhi ya nchi wafadhili wa asili (waliokuwa wakoloni) na hivyo kuepuka nchi zinazopokea misaada kuwekwa ‘kiti moto’ na wafadhili hao kupitia umoja wao uiso rasmi uitwao Paris Club. Tatu, anasema ni mpango utakaoisaidia Afrika kufanya mapinduzi ya viwanda na hivyo kuingia katika soko la kimataifa kwa kuzalisha bidhaa shindani.

Faida nyingine ya kujiunga na B&R, Dk Cheng anasema ni kupeana uzoefu wa kufikia maendeleo endelevu hususani katika nyanja zote zinazosaidia kupunguza umaskini. Hali ya China na B&R China, nchi ya tatu kwa ukubwa dunani nyuma ya Urusi na Canada na ya pili kwa uchumi mkubwa duniani nyuma ya Marekani imepiga hatua kubwa kwenye mtandao wa reli, barabara na usafiri wa anga. China inajivunia kuwa na maelfu kwa maelfu ya kilometa za barabara za kasasa kuliko nchi yoyote duniani.

Kwa mfano, licha ya umbali wa kilometa takribani 1,200 kutoka Beijing hadi Shanghai, mtu anatumia saa tano kwa usafiri wa kasi wa reli kati ya miji hiyo wakati kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam, umbali wa kilometa takribani 500 mtu anatumia wastani wa saa saba. China ambayo pia imefanya maendeleo makubwa ya ujenzi viwanja vya ndege katika kipindi cha miaka 30 ilipoanza mageuzi ya kiuchumi, hakuna ubishi kwamba maendeleo yake ya haraka yamechangiwa sana na kuimarika kwa usafiri.

Tanzania ya viwanda Wakati Tanzania inajielekeza kwenye uchumi wa viwanda, funzo linalopatikana hapa ni kwamba ni muhimu pia iendeleze ujenzi wa miundombinu itakayoharakisha usafirishaji wa bidhaa na malighafi nchini kote. Hivyo mkakati wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa ni mpango mwafaka. Ipo pia haja ya kuihuisha reli ya Tazara ambayo ilijengwa na Wachina kwa kiwango hichohicho.

Imekuwa ikielezwa kwamba kutokana na nchi za Afrika kukosa miundombinu ya kuziunganisha, iwe ndani ya nchi moja au nchi moja na nyingine imekuwa ni kikwazo kikubwa cha ukuaji wa maendeleo ya bara hilo. Mwandishi Eric Biegon, akiandika katika jarida moja la Kenya anamkariri Profesa Wang Yiwei wa Chuo Kikuu cha Renmin mjini Beijing akisema.

“Afrika imejaaliwa rasilimali nyingi za asili. Bara hilo lina uwezo mkubwa hata wa kuanzisha viwanda vikubwa. Tatizo ni kwamba hata nchi jirani hazijaunganishwa, usafirishaji ni kikwazo.” Kwa maoni yake, Afrika ina uwezo wa kupunguza sana umaskini kama itawekeza vya kutosha katika ujenzi wa miundombinu ya ardhini, majini na angani sambamba na ujenzi wa viwanda na kwamba mpango wa China wa ‘Mkanda mmoja, njia moja’ unatoa nafasi hiyo kwa Afrika.

Zaidi ya hayo anasema mpango huo utaimarisha ubadilishanaji wa utamaduni, kuhamasisha ustaarabu tofauti na kujifunza kutoka kwa kila mmoja na hivyo kila upande kunufuka.

Kwa mujibu wa Biegon, kupanda kwa gharama za kuendesha viwanda China kumekuwa kukihamasisha baadhi ya wawekezaji nchini humo kuelekeza macho yao Afrika na kwamba nchi itakayokuwa imejiimarisha vyema kimiundombinu, pamoja na mambo mengine muhimu kama za amani, sera nzuri za ndani na umeme wa uhakika bila shaka ndio itakuwa kimbilio la wawekezaji hao.

Kwa sasa nchi ya Ethiopia imevutia viwanda vya viatu na nguo vya kampuni ya Kichina ya Hujian Group vinavyoajiri maelfu ya Waethiopia. Kimsingi, mpango wa R&B unalenga, mbali ya kuimarisha miundombinu, pia kuwezesha uwekezaji mkubwa wa biashara, kupunguza vikwazo vya uwekezaji, kupunguza gharama za uwekezaji katika biashara pamoja na kukuza ushirikiano wa kikanda wa kiuchumi miongoni mwa nchi zitakazojiunga nao. Katika muktadha huo, B&R ni mpango muhimu kwa Tanzania kujiunga nao