Tofauti iliyopo kati ya methali na nahau-2

Katika makala haya kuhusu tofauti ya methali na nahau, wiki iliyopita tuliishia kwa kuangalia mifano kadhaa ya methali na kueleza maana yake na leo tunatoa mifano ya nahau, hatua itakayokusaidia kujua tofauti semi hizi mbili.

Nahau

• Chapa usingizi ………..lala sana

• Kula chumvi nyingi …..zeeka

•Chimba mkwara …fanyia mtu vitisho

• Chapa maji ………lewa •

Enda mrama …….haribika au pata matatizo. Baada ya kujadili maana, kusoma na kuangalia miundo ya methali wiki iliyopita na miundo hii ya nahau, bila shaka umeanza kubainisha tofauti iliyopo kati ya methali na nahau.

Kimaana nahau huwa na maana iliyofichika ambapo maneno yaliyotumika huwa tofauti sana na maana inayojitokeza. Kwa mfano, mtu anaposema amechapa maji, kwa maana ya kawaida, tunaweza kusema kuwa, huenda mtu huyo ametumia fimbo kupiga maji.

Na hii ndiyo maana ya kawaida kabisa ambayo mtu ambaye si mmilisi wa lugha hii atakavyoelewa. Maana halisi ya nahau hii ni kunywa pombe sana na kulewa. Badala ya mtu kusema amelewa, nahau hii hutumika kuficha ukali wa maneno na kuleta staha ya lugha na hivyo watu husema “amechapa maji.”

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa zote mbili methali na nahau maana zao huwa zimejificha mpaka uwe unaijua methali au nahau husika ndipo unaweza kung’amua maana yake. Ingawa nahau hutumia maneno yanayoleta picha ambayo ni tofauti sana na huwa haitoi fununu ya jibu au maana ya usemi huo.

Kwa kiasi fulani semi hizi zinafanana lakini tofauti bado ipo na tutaiona tunapoendelea kujadili. Sasa tuangalie dhima ya methali na nahau katika jamii. Tunaposema dhima katika jamii tunamaanisha jinsi nahau na methali zinavyotumiwa na wanajamii katika maisha yao ya kila siku, ingawa tulikwishaeleza kazi zake katika lugha, sasa tunaangalia dhima yake katika jamii.

Methali kama zilivyo semi nyingine hutumiwa na jamii kuonya, kuburudisha, kuadibu, kuelimisha kutunza utamaduni na amali za jamii, n.k. Hapa chini ni mfano wa methali zinazoonya:

•Samaki mkunje angali mbichi

•Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu

•Usipoziba ufa utajenga ukuta

•Mficha uchi hazai

•Mficha maradhi kifo humuumbua, n.k. Hizi ni baadhi tu ya methali zinazoonya na wanajamii huzitumia wanapotaka kuwaonya watu au watoto ambao wanakwenda kinyume na maadili ya jamii.

Hali kadhalika zipo methali zinazoelimisha ambazo jamii pia huzitumia kuwaelimisha wanajamii wao. Methali hizi ni kama vile Afadhali kukopa kuliko kuomba, Akomeapo mwenyeji na mgeni koma papo, Fuata nyuki ule asali, Mtaka cha uvunguni sharti ainame, Kupotea njia ndio kujua njia, n.k. Hizi ni baadhi tu ya methali zinazoelimisha.

Tungeweza kutaja methali zinazoburudisha, kuadibu na zile zinazodumisha utamaduni na amali za jamii inayohusika lakini ni nyingi mno kutajwa katika makala haya. Kitu cha msingi kujua ni kwamba methali zimegawanyika katika makundi hayo ya kidhima na zipo kwa ajili ya matumizi ya jamii. Hizi ndizo dhima za methali katika jamii.

Dhima ya nahau katika jamii, haina tofauti kubwa sana na ile ya methali. Nahau hutoa taarifa na kuhimiza jambo fulani kulingana na muktadha. Hutumika kama mafumbo ya kuficha jambo kwa mtu asiyejua nahau fulani. Nahau hutumika kama lugha ya mkato ambayo haitumii maneno mengi na kutoa ujumbe uliokamilika.

Nahau ni pambo la lugha. Huifanya lugha iwe na mvuto kusikiliza na kufanya msikilizaji asichoke kusikiliza. Hapa chini kuna mifano ya nahau zinazomhimiza mtu kufanya jambo. Baadhi ya nahau hizo ni kama vile aga ukapera - oa, tia nia - amua kufanya jambo, chapa kazi- jitahidi zaidi kufanya kazi, chapa miguu- kazana kutembea, jikaze kisabuni - vumilia mpaka mwisho ili kukamilisha jambo, n.k.

Hizi ni baadhi ya nahau zinazohimiza mtu kufanya jambo. Zipo pia nahau zinazoburudisha kulingana na maneno yaliyotumika kiasi kwamba mtu anaposikia huweza akacheka. Kwa mfano, amechinjiwa baharini – poteza mtu au nyang’anya, kuacha kumshirikisha mtu katika jambo bila kujali au sababu maalumu, kula kona - toroka, amekwaa mkenge - amepata kitu kibovu asichokuwa anatarajia au ameingia matatizoni bila kutarajia, pigwa kibuti - achwa na mke, ingia mitini - kimbia au jifiche n.k.

Utaona kuwa nahau hizi zinatumia maneno machache lakini ujumbe wake huwa kamilifu. Watu hupenda kuzitumia katika mazungumzo yao kwa sababu hupamba lugha na kuifanya inoge. Baada ya kuangalia dhima ya semi hizi mbili katika jamii, sasa tuangalie tofauti ya methali na nahau kimuundo.

Zifuatazo ni tofauti zilizopo baina ya semi hizi mbili. (Angalia kwenye jedwali). Kwa ufupi tunaweza kusema kuwa hizo ni baadhi ya tofauti zilizopo baina ya methali na nahau. Tofauti iliyobayana zaidi ambayo inaweza kumfanya msomaji kupambanua methali na nahau ni kwa kutumia miundo yao.

Miundo ya semi hizi ipo bayana zaidi kuliko tofauti nyingine za kimaana na kidhima. Bila shaka baada ya kusoma makala haya, sasa unaweza kupambanua ipi ni methali na ipi ni nahau.

Makala haya yatakuwa msaada kwa wale ambao walikuwa wanachanganya methali na nahau wakati wa kuzungumza na kuandika. Makala haya yatakuwa msaada kwa wadau wa Kiswahili na hasa wanafunzi na walimu wa somo la Kiswahili.

Shime Watanzania tukipende Kiswahili kwani ni Lugha ya Taifa. Kumbuka nguo ya kuazima haisitiri maungo. Mwandishi wa makala haya ni Mchunguzi Lugha Mwandamizi, Idara ya Lugha na Fasihi, BAKITA, SIMU: 0713340959, 0683680556