Viuatilifu ni muhimu pia hatari kwa vyanzo vya maji

MATUMIZI ya viuatilifu, yamekuwa na msaada kwa maana ya kumhakikishia mkulima mavuno zaidi, lakini kwa upande mwingine wa shilingi vinatajwa kuwa hatari kwa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini.

Uchunguzi uliofanywa katika wilaya za Songea na Mbinga umebaini wakulima bado wanatumia mbolea za chumvichumvi aina ya SA na dawa za kuua wadudu aina ya bluecopper, kimatila, DDT, theonix, sumithion, karate na selecrone ambazo zinatajwa kuwa ni hatari kimazingira na kiafya.

Dawa nyingine ambazo wakulima wanatumia kupulizia kwenye nyanya kwa lengo la kuzuia ugonjwa wa ukungu ambao unakausha nyanya ni nidithane, milthane, bravo, rido, ridomil, victory, farmazeb, helicozeb, mancozeb na lincomil.

Msimamizi wa chanzo cha maji cha mto Luhira kilichopo Songea, Swalehe Kinana anasema wakulima katika chanzo cha mto Luhira licha ya kwamba wengi wameanza kuogopa kulima baada ya kuanza kuchukuliwa hatua za kisheria, hata hivyo bado wanalima kando kando ya chanzo hicho cha maji. “Wakulima hawa wanapulizia kemikali hatari kuanzia Desemba hadi Agosti kila mwaka, miezi ambayo kuna wadudu wengi waharibifu wa mimea.

Miezi ambayo huwa hawatumii dawa hizo ni kuanzia Septemba hadi Novemba,’’ anasema. Josephat Maliselo ni Mdhibiti wa Ubora wa Maji na Viwango kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Songea (Souwasa) anasema kemikali aina ya bluecopper na redcopper zinapoingia kwenye chanzo cha maji cha mto Luhira, zinapenya moja kwa moja, jambo ambalo linaweza kuathiri afya za watumiaji.

Maliselo ambaye ni Daktari wa Maji anabainisha kuwa maabara ya maji iliyopo Songea haina mashine ya kupima na kutambua kemikali za bluecoper au red copper ambazo zimeingia kwenye maji na kwamba hapa nchini mashine ambazo zinaweza kupima zipo maabara ya Wizara ya Maji, Mkemia Mkuu na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Baadhi ya wakazi wanaozunguka milima ya Matogoro wakiwemo wa kijiji cha Mahiro, Charles Haule, Oliver Mbilinyi na Alois Haule wanakiri kulima katika vyanzo vya maji na kutumia kemikali. Wananchi hao wanaeleza kuwa wanatumia kemikali hizo kwa uzoefu tu kwa kuwa zinawahakikishia mavuno zaidi lakini hawana elimu ya athari za mazingira zinazotokana na kemikali hizo ambazo wanazitumia kila mwaka katika kilimo cha mboga ili kuua wadudu waharibifu wa mazao.

“Wakulima wanaozunguka milima ya Matogoro baadhi wamelima kahawa ambayo wanapulizia dawa aina ya bluecopper ambayo wakati wa masika inachuruzika na kuingia kwenye vyanzo vya maji vilivyopo Matogoro,” anasema Mtaalamu wa Mazingira, John Nchimbi wa Kijiji cha Mahiro.

Moses Ndunguru, mtaalamu wa dawa za mimea, anasema matumizi ya dawa ya kahawa aina ya bluecopper karibu na vyanzo vya maji ni hatari kwa kuwa wakati wa masika dawa hizo zinaingia moja kwa moja kwenye vyanzo vya maji na kusababisha athari endelevu katika mazingira.

Ndunguru anabainisha kwamba uwepo wa shamba la mwekezaji la kahawa lenye ukubwa wa ekari 5000 linalolimw akwa njia ya umwagiliaji katika Mto Ruvuma na matumizi ya dawa za kuua wadudu wa zao hilo la kahawa katika kijiji cha Lipokela wilayani Songea, vinanaweza kuleta athari za kimazingira.

Anabainisha kuwa matumizi ya dawa za kahawa kwenye vyanzo vya maji kwa kupulizia dawa za kuua wadudu za kahawa ni hatari katika mazingira na kiafya hivyo inatakiwa kuchukua tahadhari ili kuepukana na madhara ambayo yanaweza kuleta athari za kiafya kwa wananchi wanaoishi kando kando ya mto Ruvuma.

“Dawa za kahawa zinaweza kuchuruzika na kuingia mto Ruvuma uliopo jirani na shamba hilo. Wananchi wanaoishi kando kando mwa mto huo wanaweza kuathirika kiafya na kimazingira,’’ anasisitiza Ndunguru.

Madhara ya dawa ya blue copper (shaba ya bluu) kwenye maji na chakula kwa mujibu wa utafiti ambao umefanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ni kusababisha magonjwa mbalimbali kwa binadamu kupitia maji au chakula .

Utafiti wa WHO ulifanyika mwaka 2004 ulibaini kuwa madini ya shaba ya bluu kwenye maji na vyakula yanachangia asilimia 40 ya magonjwa katika nchi zinazoendelea na kwamba athari za shaba ya bluu kuingia katika maji na vyakula ni chanzo kikuu cha magonjwa mengi kama vile ngozi, matumbo, ubongo, figo, mapafu, moyo na ini.

Hata hivyo, kwa mujibu wa WHO, dalili za magonjwa yanayotokana na kuathirika na shaba ya bluu yanachukua muda mrefu na kwamba kuchelewa kwa dalili huathiri zaidi mfumo wa fahamu, ubongo na macho.

Meneja wa Maji Bonde la Ziwa Nyasa, Witgal Mkondora anasema bonde hilo linahusika na kuulinda mto Luhira lakini anakiri kuwa kuna changamoto katika kuwadhibiti wakulima wanaolima kando kando mwa mto huo kutokana na wengi kupenda kulima katika maeneo oevu ambayo yana rutuba nyingi na maji ya kumwagilia.

Hata hivyo, Mkondora anabainisha kuwa sheria ya mazingira namba 57 ya mwaka 2004 inataka shughuli za kibinadamu kufanyika umbali wa meta 60 kutoka katika kingo za mto na kwamba wote wanaolima kando kando ya mito ndai ya meta hizo wanafanya makosa na wanatakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria. Mwandishi ni mchangiaji wa gazeti hili, mawasiliano yake ni baruapepe: albano. Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.,simu 0784765917