Wafugaji, wakulima wanavyokwamisha utunzaji ikolojia hifadhi ya Ihefu

HIFADHI ya taifa ya Ruaha, upande wa bonde la Ihefu inakabiliwa na changamoto inayotokana ama uelewa mdogo wa wananchi au kile kinachodaiwa ni baadhi ya watu kutotii serikali katika suala la utunzaji.

Jitihada mbalimbali zilizofanywa na serikali katika kulinda bonde hili la Mto Ihefu ni pamoja na kuhamisha wakazi wa baadhi ya vijiji na kuondoa mifugo katika bonde hilo; kulikofanyika mwaka 2008.

Jitihada hizo zinaonekana kuanza kuleta matumaini ya ikolojia ya Ruaha kurejea katika asili yake ya kuweza kuwa na maji mwaka mzima. Lakini pamoja na hali kuonekana kuanza kuleta matumaini bado kuna dalili za uharibifu wa mazingira unaolikabili eneo hili muhimu.

Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na wadau wengine, wanafanya juhudi kuhakikisha Hifadhi ya Ruaha inarejea katika hali yake ya asili. Hata hivyo bado vipo vitendo vya uingizaji wa makundi ya mifugo katika eneo hilo.

Wafugaji wanadaiwa kuingiza mifugo usiku na kuitoa alfajiri wakitambua kuwa si rahisi kukamatwa usiku. Mhifadhi Msaidizi, Alexander Haguma katika hifadhi hiyo ya Ruaha, anathibitisha kuwapo vitendo hivyo vya wafugaji na kwamba, ikifanyika doria mchana, hawakuti ng’ombe.

Hata hivyo, Haguma anasema katika kukabili changamoto hiyo, askari wa Tanapa wamekuwa wakiweka mitego mbalimbali ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikifanikiwa kuwanasa wafugaji wanaoingiza mifugo na kisha kuwatoza faini kulingana na makosa yao.

“Tunashukuru jitihada zilizofanywa na wadau mbalimbali zimezaa matunda kwa ikolojia kuanza kurejea katika hali yake ya kawaida. Sasa hapa wanyama na ndege kama tembo, swala, kanga na kwale wameanza kupatikana katika eneo hili.

Tunaamini kadiri ikolojia inavyozidi kurejea katika hali yake ya awali wanyama wataongezeka zaidi.” “Lakini changamoto za uingizaji mifugo hasa usiku, ujangili hasa wa uvuvi haramu katika mabwawa na mto pamoja na mioto isiyo pangwa, bado inatutatiza,” alisema Haguma.

Mbolea inayotumika kwenye mashamba ya mpunga katika bonde la Usangu wilayani Mbarali, inatajwa kuwa changamoto nyingine inayokwamisha utunzaji wa ikolojia katika hifadhi. Haguma anasema mbolea hizi zinasababisha nyasi ndani ya hifadhi kurefuka kupita kawaida na kusababisha ugumu wa kudhibiti moto unapotokea.

Kwa asili uoto wa bonde, ni wa nyasi fupi lakini mbolea za kwenye mashamba ya mpunga husombwa na maji hadi ndani ya bonde hilo. Matumizi ya maji ya mito katika maeneo ya mashamba yasiyozingatia maelekezo ya wataalamu, pia yanasababisha viumbe hai kukosa maji kwenye baadhi ya makazi hasa mabwawa yaliyopo ndani ya bonde hilo.

“Wapo wakulima ambao wakati wa kilimo wanachepusha maji yote na kuyaingiza mashambani. Hii inatokea hasa katika skimu za umwagiliaji zisizofuata ushauri wa kitaalamu wa namna ya kutumia maji ya mito katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji. Jambo hili ni kinyume cha sheria za matumizi ya maji ya mito” Aidha, ujenzi wa mazizi kando mwa mto Ruaha katika upande usio wa hifadhi ni changamoto nyingine.

Wahusika wanakiuka sheria inayotaka ndani ya meta 60 kusifanyike shughuli zozote za kibinadamu. Hivi karibuni mkuu wa wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune aliamuru wafugaji wa Kata za Imalilo Songwe na Luhanga kuondoa mazizi yaliyojengwa pembezoni mwa Mto Ruaha na Mto Mbarali.

Pia ameamuru wanaolima ndani ya mita sitini kando kando ya mito hiyo miwili kuondoa mashine za kuvutia maji kwa ajili ya kumwagilia mimea mashambani. “Lakini wale walioendelea kulima ndani ya mita sitini na kutumia pampu nakumbuka kabisa nilitoa agizo na hata Kikosi Kazi cha Makamu wa Rais kilipofika katika wilaya yetu wajumbe walitoa maagizo kwamba wale wote waliokuwa bado wanaendelea na shughuli za kilimo mwisho wa kutumia pampu ilikuwa ni Juni 30 mwaka huu”.

Baada ya agizo, utekelezaji wa kisheria ulianza kwa Kamati ya Ulinzi na usalama wilaya kuvunja na kuchoma mazizi yote yaliyokutwa pembezoni mwa mto Ruaha upande usio wa Hifadhi.

Mazizi 28 yalichomwa moto katika operesheni iliyofanyika siku moja kwa kushitukiza. Operesheni hiyo iliyofanyika ikiwa ni siku nne tangu mkuu wa wilaya atoe agizo, yalikutwa mazizi pekee bila kuwapo mifugo ikidhihirisha wafugaji waliitii serikali kwa kuondoka wenyewe.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Kivuma Msangi anazungumzia operesheni hiyo iliyofanyika upande wa Kijiji cha Mwanavala akisema, itakuwa ya kushitukiza na endelevu.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Mnazi, katika kijiji cha Mwanavala, Ditila Sanyiwa anaahidi kuendelea kushirikiana na serikali kusimamia wafugaji wasijenge mazizi kando ya mito ili kulinda mazingira na hifadhi irejeshe ikolojia yake.

Uongozi wa serikali, mkoa wa Mbeya, umekuwa na mikakati kuhakikisha ikolojia ya hifadhi ya Ruaha upande wa Ihefu inarejea na kutunzwa. Katika mikutano yake kadhaa mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amekuwa akitoa maagizo mbalimbali na kuonya wanaotaka kuharibu Ikolojia iliyokwisha rejea.

Katika ziara ya hivi karibuni ya Makala, maofisa wa Tanapa pamoja na Kamati za ulinzi na Usalama za Mkoa wa Mbeya, Makalla alisema ni jambo la kupongeza kuona uoto wa asili wa eneo la Ihefu unarejea katika hali yake ya kawaida.

Katika jitihada za kuhakikisha uoto huo haupotei, mkuu wa mkoa anasema ni pamoja na kuhamishia mahakama maalumu katika eneo la Hifadhi ya Ruaha upande wa Bonde oevu la Ihefu ili ifanye kazi maalumu ya kudhibiti wafugaji jeuri wanaoingiza mifugo ndani ya hifadhi hiyo.

Anasisitiza kuwa hakuna mfugaji yeyote anayekaidi atakayefumbiwa macho na mahakama hiyo. “Maana tumechoka, kuna wafugaji asubuhi unamtoza faini, analipa kwa kuwa fedha zipo tu jioni anaingiza tena mifugo hifadhini sasa tunaleta mahakama huku huku na kazi yake itakuwa kushughulika na wafugaji wa aina hii,” anasema mkuu wa mkoa.

Wakuu wa mikoa ya Iringa, Amina Masenza na mkuu wa mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka pia wamekuwa wakikemea uharibifu wa mazingiza ya Mto Ruaha wakisema hawatavumilia yeyote atakayekwenda kinyume na mikakati ya serikali ya kurejesha ikolojia ya mto huo.

Msimamo huo waliutoa mwaka huu kwenye maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kwa Ukanda wa Mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe ilifanyika wilayani Mbarali mkoani Mbeya.

“Wakuu wote wa mikoa hii ambayo kikanda tunaunganishwa na Ikolojia tumekubaliana kwa pamoja kwa asilimia mia kwa mia. Mazingira ni suala mtambuka linalogusa kila mmoja aliye hai awe binadamu, ndege, mnyama, mdudu na hata vilivyomo ndani ya ardhi. Ni jukumu letu kwa kuwa mazingira ni maisha yetu, hivyo lazima tuone umuhimu wa kuyatunza,” anasema Makala.