Thamani ya uvuvi Tanga na uharibifu wa mazingira

MAZINGIRA ya viumbe hai baharini wakiwemo samaki yanazidi kuwa hatarini duniani kote kutokana na kukithiri kwa shughuli za kibinadamu, ikiwemo uvuvi usio endelevu. Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Chakula Duniani (FAO), kuna watu milioni 38 duniani wanaofanya kazi ya kuvua au kufuga samaki na hivyo husaidia kukuza uchumi wa nchi zao.

Pamoja na wavuvi hao pia wapo watu wengine milioni 500 wanaojishughulisha na masuala ya uvuvi kupitia usafirishaji wa samaki na bidhaa za baharini na kuuza sokoni, madukani na hata mahotelini.

Kwa upande wa Tanzania, shughuli za uvuvi nazo zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa nchi hiyo, kutokana na ukweli kuwa Tanzania ni moja ya nchi za Afrika zilizobarikiwa kuwa na bahari, maziwa, mito na mabwawa yenye samaki na viumbe wa kila aina wanaoishi kwenye maji.

Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2014 jumla ya watanzania 202,654 hutegemea sekta ya uvuvi kama kitega uchumi chao ambapo Tanzania kuna jumla ya wavuvi 19, 223.

Kwa ujumla, takribani watanzania milioni nne wananufaika kwa namna moja au nyingine kupitia sekta hiyo ya uvuvi; hii ni kwa maana ya biashara, usafirishaji wa bidhaa hiyo na utengenezaji wa boti au ngalawa za uvuvi.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, mwaka 2013, uzalishaji wa samaki nchini ulikuwa ni jumla ya tani 367,854 na kiwango cha juu kabisa kuwahi kurikodiwa cha uzalishaji wa samaki kilikuwa ni mwaka 2005 ambapo kulivuliwa jumla ya tani 375,534.

Aidha, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/18, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba, alisema katika mwaka wa fedha 2016/2017, jumla ya tani 362,595 za samaki wenye thamani ya Sh trilioni 1.49 zilivunwa na wavuvi 203,529.

Wakati katika mwaka wa fedha wa 2015/16 tani 362,645.3 za samaki wenye thamani ya Sh trilioni 1.48 ndio waliovunwa. Hata hivyo, kutokana na kukithiri kwa shughuli za uvuvi usio endelevu, hasa uvuvi haramu katika maeneo mengi ikiwemo Tanga, kuna hatari kubwa ya biashara hiyo nchini kushuka.

Wanaojitosa katika uvuvi haramu ni wale wanaozingatia maslahi ya kipindi cha sasa pekee bila kujali kipindi na vizazi vijavyo kutokana na kuharibu kabisa mazingira na mazalia ya viumbe vya baharini wakiwemo samaki.

Uvuvi haramu unahusisha matumizi ya zana haramu za uvuvi zilizozuiliwa kisheria ambazo husababisha kuvuliwa kwa samaki wachanga na kuharibu mazalia baharini. Zana hizo ni pamoja na matumizi ya mabomu au baruti, nyavu aina ya kokoro, uvuvi kwa kutumia mikuki, matumizi ya mitando na sumu.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti hili mkoani Tanga, serikali imechukua hatua mbalimbali za kudhibiti uvuvi haramu Tanga, baada ya kuonekana kuwepo kwa shughuli zilizokithiri za uvuvi na uvuvi haramu na hivyo kuhatarisha viumbe baharini.

Katika mkoa huo, halmashauri za wilaya ambazo ni Mkinga, jiji la Tanga, Muheza na Pangani ndio zinazojishughulisha na uvuvi na wananchi wanaoishi katika wilaya hizo takribani asilimia 90 ni wavuvi na asilimia iliyobaki hujishughulisha na shughuli nyingine kama vile kilimo.

Hata hivyo, katika halmashauri hizo zote zilizo pembezoni mwa bahari shughuli yao kubwa ni uvuvi kwa asilimia 90 na shughuli nyingine kama vile kilimo cha mwani ni asilimia 10.

Pamoja na hayo mkoa huo, una ukanda mrefu wa mwambao wa pwani yenye kuwa na mandhari nzuri za kupendeza kama vile ghuba, matumbawe, ghuba za Kwale, Manza, Moa, Tanga pamoja na Mwambani.

Fukwe zipatikanazo mkoani Tanga ni pamoja na Kigombe, Pangani na Ushongo. Fukwe hizo zimefunikwa na kuzungukwa na aina mbalimbali za visiwa kadhaa kama vile Ulenge na Toten vinavyotoa fursa kadhaa za kiutalii na malazi.

Maeneo yenye kuwa na mandhari nzuri na mvuto katika kutembelea mkoani humo ni pamoja na mji wa kihistoria mjini Tanga, visiwa vya Toten, Ulenge, Yambe, Karange, Maziwe pamoja na Pangani iliyo karibu kabisa na mapango ya Amboni.

Maeneo mengine ni pamoja na magofu ya kale ya Tongoni na maji moto ya Gallanos. Hata hivyo, pamoja na uzuri wa mkoa huo katika maeneo ya Pwani, baadhi ya mandhari zinaanza kupotea vikiwemo visiwa kufukiwa na maji kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira ya baharini.

Kisiwa ambacho katika miaka ijayo kitapotea kabisa ni pamoja na kisiwa cha Maziwe ambacho kilikuwa ni makazi ya watu, kina miti na majani lakini sasa kisiwa hicho kimebaki eneo dogo tu la mchanga mtupu, ambalo kutokana na hali ya bahari wakati mwingine hufukiwa kabisa na kubaki eneo dogo tu.

Kwa mujibu wa Mshauri wa Uvuvi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tanga, Hassan Juma, mkoa wa Tanga takribani maeneo yote yanajishughulisha na uvuvi, lakini ni halmashauri nne tu ndio shughuli zake kubwa ni uvuvi.

Anasema mkoa huo una eneo la bahari lenye urefu wa kilometa 480 za mstari wa fukwe likiwa limesheheni miamba ya matumbawe 96 ambalo kwa upande wa eneo la uvuvi ni kuanzia urefu wa kilometa moja hadi saba.

“Kwa mujibu wa takwimu za sensa za mwaka jana, mkoa huo una wavuvi takribani 8,000 wanaotumia jumla ya vyombo vya uvuvi vinavyokadiriwa kufikia 3,500 vyenye uwezo wa kwenda umbali wa kilometa kuanzia mbili hadi 12 baharini na wachuuzi wakubwa wa samaki 12,000.

“Samaki wanaovuliwa kwa wingi mkoani hapa ni pamoja na changu wadogo, samaki wadogo mfano wa dagaa, jarife, papa wakubwa wenye urefu wa kuanzia nchi sita kwenda juu, jodari na pweza.

Hata hivyo, Juma anabainisha kuwa hali ya uvuvi haramu mkoani humo si nzuri na uvuvi unaotumika kwa sana ni wa baruti, kokoro, kuzamia, kutumia mkuki na sumu, hali inayoharibu mazalia na maeneo ya kujifichia viumbe wa bahari.

Anakiri kuwa kutokana na uvuvi huo haramu, ni ngumu kwa wavuvi wa mkoa huo kuvua katika maeneo ya karibu ya bahari wakafanikiwa na hivyo walazimika kutumia takribani saa saba mpaka 12 kuvua samaki kutokana na kupungua kwa samaki hao.

“Ili waweze kwenda kwenye maji marefu na kupata samaki wengi, ni lazima wawe na meli na boti za kisasa zinazotumia injini. Mwanzoni kulikuwa hakuna ulazima wa kwenda umbali mrefu kuvua samaki, lakini sasa hivi hali ni mbaya samaki katika maeneo ya jirani wamepungua sana,” anasema.

Anasema kutokana na jitihada za serikali katika kudhibiti uvuvi huo kupitia taasisi zake mbalimbali wakiwemo Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu. Akizungumza na gazeti hili, jijini Tanga hivi karibuni, Mhifadhi Mwandamizi katika Hifadhi ya Bahari ya Silikanti Tanga (TACMP), January Ndagala anasema uvuvi haramu usipodhibitiwa kuna hatari ya visiwa maarufu, samaki na viumbe muhimu wa baharini kutoweka katika miaka ijayo.

Anafafanua kuwa uvuvi wa kokoro ni ule unaohusisha nyavu zenye matundu madogo ambazo hutegwa na kubeba samaki, matumbawe na maficho ya samaki ambayo kwa mujibu wa mtaalamu huyo yana umuhimu mkubwa katika maisha ya viumbe hao wa baharini.

Pia anasema uvuvi wa baruti au mabomu ndio hatari zaidi kwani wenyewe huharibu kabisa mazingira ya chini ya bahari ambayo ni makazi, na matumbawe kiasi cha kusababisha samaki kushindwa kuzaliana. “Ifahamike kuwa kila kitu kilicho chini ya bahari kina umuhimu wake, kuanzia majani, miamba, matumbawe na mikoko.

Kama tulivyo sisi huku nchi kavu, hata baharini kuna viumbe mbalimbali wanaotegemeana sasa ukiharibu mazingira yao ya kawaida, ni wazi kuwa watakimbia au kutoweka kabisa,” anasisitiza.

Anasema kwa sasa kazi ya TACMP ni kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kulinda mazingira ya viumbe baharini, kulinda viumbe hao na makazi yao, kufanya utafiti na utalii na uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wake, Ofisa Mhifadhi Mwandamizi wa Hifadhi ya Bahari, kupitia Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu, Haji Mahingika, anasema uvuvi huo haramu unasababisha uharibifu mkubwa wa viumbe hai baharini kiasi cha kusababisha baadhi ya visiwa maarufu mkoani humo kumezwa na maji.

Anasema visiwa vingi ambavyo miaka takribani 1,000 iliyopita vilikuwa vikitumiwa na binadamu kwa shughuli za utalii, makazi na shughuli nyingine hata za kiuhalifu, kwa sasa vinaelekea kufukiwa kabisa na maji, akitolea mfano kisiwa cha Maziwe na cha Mpunguti.

Mahingika anaeleza kuwa mkoa wa Tanga ni moja ya mikoa yenye maeneo mazuri ya bahari yanayohitaji kutunzwa kupitia uvuvi endelevu. “Tunafanya kazi ya kuelimisha jamii juu ya madhara ya kutumia sumu, mabomu na nyavu za kokoro wakati wakivua, tunawaelezea faida za kiuchumi watakazopata kupitia uvuvi endelevu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Moa ambacho ni maarufu mkoani hapo kwa biashara ya samaki, Zarine Mohamed, kutokana na kukithiri kwa shughuli za uvuvi haramu kwa sasa hali ya samaki ni mbaya kwani wengi wanapatikana katika maji marefu yanayohitaji boti na meli za kisasa.

“Wengi wetu hapa tunavua kwa kutumia mitumbwi na ngawala ambazo hazina uwezo wa kwenda maji marefu kwani zinatumia mishipi inayoendeshwa kulingana na hali ya hewa. Uharibifu ni mkubwa sana kiasi kwamba maeneo ya karibu hakuna tena samaki,” anasema.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Doria katika kijiji chake, anakiri kuwa uvuvi haramu wa kutumia kokoro, baruti na mikuki umechangia kuharibu mazalia na mazingira ya baharini kiasi cha samaki kupungua kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ndumbini wilayani Mkinga, Sheha Haji, anasema pamoja na kwamba serikali imejitahidi kudhibiti uvuvi haramu mkoani Tanga kwa kuwa na vyombo mbalimbali vya udhibiti bado elimu inahitajika kwa wavuvi kutambua madhara ya uvuvi huo haramu.

“Kijiji cha Moa kimejitahidi sana kudhibiti uvuvi haramu, tatizo lipo katika vijiji vya Maboza na Petukiza kule ngalawa hazipungui 10 kwa siku zikiwa na kokoro zaidi ya 48 zikivua. Doria inafanyika lakini na wao pia wanavua kwa kuvizia, lengo lao ni kupata samaki wengi kwa wakati mmoja bila kujali uharibifu wanaoufanya,”anasema.

Wakati mkoa huo, ukijitahidi kuhakikisha, uvuvi unaofanywa mkoani Tanga ni endevu, katika bajeti yam waka wa fedha 2017/18, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, imepanga kuendelea kuhamasisha wavuvi kuwekeza katika ununuzi wa zana bora za uvuvi ili waweze kuvua kwenye maji ya kina kirefu katika Maziwa na Bahari.

Kwa mujibu wa Waziri Tizeba, idadi ya boti zenye injini imeongezeka kutoka 11,284 mwaka 2015/2016 hadi 14,136 mwaka 2016/2017 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 25.3. “Pia, Wizara kupitia Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu, imeweka jumla ya vifaa 36 vya kuvutia samaki ili kuvutia samaki wakusanyike mahali pamoja na hivyo kuwarahishia wavuvi kuwafikia kwa urahisi.