Mwarobaini wa kuingiza mifugo holela Mbeya waja

MKOA wa Mbeya ni moja ya mikoa iliyoitikia mwito wa Serikali nchini wa kupiga chapa mifugo iliyopo zaidi ya 3,000. Upigaji chapa mifugo ni agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambalo ni utekelezaji wa Sheria Namba 12 ya mwaka 2010 ya Usajili, Utambuzi na Ufuatiliaji wa Mifugo.

Sheria inasema upigaji chapa unasaidia udhibiti wa wizi wa mifugo, udhibiti wa magonjwa ya mlipuko, kuimarisha mbari za mifugo, hakikisho la usalama wa chakula, ustawi wa wanyama na kuwezesha biashara ya mifugo ndani na nje ya nchi.

Sheria nyingine iliyo na uhusiano na inayotekelezwa sasa kwa upigaji chapa mifugo ni ya Malisho na Rasilimali ya Vyakula vya Mifugo Namba13 ya mwaka 2010. Sheria hiyo inasisitiza Serikali za Vijiji kutenga maeneo ya malisho ya mifugo kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi ya vijiji Namba 5 ya mwaka 1999 na sheria ya matumizi bora ya Ardhi Namba 6 ya mwaka 2007.

Wilaya za Chunya na Mbarali ndizo zinazoongoza kwa kuwa na mifugo mingi zaidi kulinganisha na wilaya nyingine mkoani hapa na mifugo mingi huingizwa kinyemela na wafugaji katika wialaya hizo.

Hali hiyo husababisha migogoro baina ya wafugaji kwa wafugaji, wafugaji na wakulima na wafugaji na Mamlaka mbalimbali za kama vile Hifadhi ya Taifa ya Ruaha wilayani Mbarali na Misitu ya Nyuki wilayani Chunya.

Katika utekelezaji agizo la Waziri Mkuu, upigaji chapa mifugo katika wilaya hizi mbili umeanza kufanyika na kazi hii inaendelea katika maeneo mbalimbali mkoani Mbeya. Ng’ombe ndiyo inayoonekana kulengwa zaidi kutokana na ukweli kwamba ndio mara nyingi husababisha migogoro.

Kwa wilayani Chunya mifugo itakuwa na nembo ya T-CHU wakati wilayani Mbarali itakuwa na nembo T-MBA. Wilaya kama Rungwe inayoongoza kwa kuwa na ng’ombe chotara wa nyama na maziwa ambao hawachungwi watawekewa alama za heeeni sambamba na namba zake maalumu.

Rungwe inaongoza kwa uzalishaji mkubwa wa maziwa japo si rahisi kuona mifugo ikizagaa katika mapori yake wala vijijini. Upigaji chapa ulizinduliwa Julai 11 mwaka huu wilayani Chunya na Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, katika kijiji cha Soweto kata ya Kasanga.

Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya ya Chunya, Rehema Madusa, hadi kukamilika kwa hatua hiyo, ng’ombe 280,000 wa wafugaji 2,755 watakuwa wamepigwa chapa ya utambuzi.

Katika uzinduzi huo, Makalla aliwataka wafugaji wote kuhakikisha wanapeleka mifugo yao ili kupigwa chapa huku akisisitiza kuwa kwa yeyote atakayekiuka agizo hilo, mifugo yake haitatambuliwa na itabidi iondolewe wilayani humo.

Anawasihi pia wenyeviti wa vijiji na watendaji wa kata kuhakikisha hawapokei mifugo mipya ili kuiingiza katika utaratibu wa upigaji chapa kwa kuwa mifugo itakayohusika ni ile iliyopo katika orodha zilizokusanywa wakati wa sensa ya kubaini mifugo iliyopo.

Kwa upande wake, mkuu wa wilaya ya Chunya, Rehema Madusa anasema upigaji chapa ulitazamiwa kumalizika jana (Agosti 1) na kwamba kuanzia leo na kuendelea, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya itaanza kazi ya kukagua mifugo isiyo na chapa ya utambuzi wa kiwilaya.

Anaona hatua ya kupiga chapa mifugo kuwa mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya uingizwaji mifugo kiholela. “Ni kama ndoto inayotimia sasa. Tumeimba kwa muda mrefu, tumetafuta suluhu kwa muda mrefu. Sasa tutakuwa na uwezo mkubwa wa kufuatilia na kujua kinachoendelea kwa wafugaji wetu.

Lakini pia itasaidia upangaji wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyetu.” Madusa anasema Chunya ina vijiji 43 na kati ya hivyo, 13 pekee ndivyo vimepimwa na vina mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Kwa upande wa Mbarali, upigaji chapa ulianza Julai 14 baada ya kuzinduluwa na Makalla katika kijiji cha Azimio Mapula, kata ya Kongolo Mswiswi. Kwa mujibu wa Ofisa Mifugo wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali, Augustino Lawi, wilaya ina jumla ya wafugaji 7,049 na Mifugo iliyopo ni ng’ombe wa asili 193,434, chotara 1,555 na ng’ombe chotara wa nyama aina ya boran 2,250 na kufanya jumla ya ng’ombe wote kuwa wa 197, 239.

Mifugo mingine ni mbuzi 93,707, kondoo 38,491 na punda 4,486. Kwa Kata ya Kongolo Mswiswi pekee ulipofanyika uzinduzi, Lawi alisema kuna ng’ombe 2,631, mbuzi 1,171, kondoo 173 na punda 121.

Akasema katika kijiji cha Azimio Mapula pekee ambacho ndipo shughuli husika ilifanyika kuna ng’ombe 628, mbuzi 625, kondoo 133 na punda 95. Lawi anasema kwa sasa maeneo ya malisho yaliyopo katika Wilaya ya Mbarali ni hekta 154,000 na kwamba kati ya hizo, hekta 97,281 za malisho ziko katika maeneo ya vijijini.

Maeneo yaliyobakia yenye jumla ya hekta 294 ni za shamba la mbegu za malisho la Langwira linalomilikiwa na Serikali na hekta 43,725 zinamilikiwa na wawekezaji binafsi wa ranchi ndogo kama Ranchi ya Usangu ambayo imegawanywa katika ranchi ndogo 16 za watu binafsi na ranchi ya wafugaji wa mifugo ya asili ya Matebete yenye ukubwa wa hekta 12,700.

Inaaminika kwamba upigaji chapa huo utakuwa mwarubaini wa changamoto kubwa zaidi ambayo ni ongezeko la idadi ya mifugo ambalo halitokani tu na kuzaliana kwa mifugo, bali wafugaji wavamizi kutoka maeneo mengine nje ya wilaya wanaoamua kuhamishia mifugo yao katika wilaya hiyo, jambo linalochochea migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

Hali hiyo inaelezwa kusababisha pia uhaba wa malisho na maji hali ambayo inachangiwa pia na mabadiliko ya tabianchi. Wakati wa kiangazi kumekuwa kukiibuka mara kwa mara migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi kwa kugombea vyanzo vya maji.

Tatizo lingine linalotajwa ni mwamko mdogo wa wafugaji wa kutokuwa na mpango endelevu wa kupunguza idadi ya mifugo kwa kuvuna na kuuza mifugo yao ili eneo la malisho lililopo liweze kutosheleza mahitaji bila kuathiri mazingira.

Changamoto nyingine kwa wafugaji inayotajwa ni upungufu wa wataalamu wa mifugo ngazi ya vijiji pmoja na vitendea kazi kwa maofisa ugani wa mifugo vikiwemo vyombo vya usafiri na nyumba za kuishi.

Makalla anasema ni muhimu taarifa za mifugo iliyotambuliwa na kisha kupigwa chapa kuingizwa kwenye Mtandao ili kurahisisha ufuatiliaji wa mifugo mkoani hapa wakati wote. “Hapo ndipo nataka nione usomi wa watu waliosomea IT (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-Tehama).

Nataka taarifa ya kila mfugaji ionekane tena na picha yake iwekwe. Ili hata nikiwa pale ofisini nikitaka kujua taarifa za mifugo ya mfugaji Shija niweze kuzipata haraka. “Hii itasaidia hata pale tunapotaka kubadili taarifa baada ya mifugo ya mfugaji kuongezeka kwa kuzaliana, kuuziana, kulipana mahari wanapoozeshana au ikipungua.

Anawataka wafugaji kutoingiwa na hofu na hatua ya upigaji chapa mifugo kwani pia itaasaidia kudhibiti wizi wa mifugo kwa kuwa kila halmashauri ina nembo yake. “Tutakapomuona ng’ombe aliye na nembo ya Chunya hapa Mbarali tutauliza kaingiaje hapa na kama aliibwa tutajua. Kama kuna mfugaji kaingia kinyemela pia tutajua. Lengo hasa tunataka kila mmoja abakie pale alipotambuliwa na kutengewa eneo kwa ajili ya malisho ya mifugo yake,” anasema.