Ulevi, ushirikina vyachangia kesi za ubakaji Iringa

VITENDO vya ubakaji na udhalilishaji wa kinjisia, vimekuwa vikishika kasi kila siku, hali ambayo inasababisha wasiwasi na hali ya kutoaminiana miongoni mwa wanajamii.

Hivi karibuni nilitembelea Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa na miongoni mwa maeneo ambayo nilivutiwa nayo ni kutaka kufahamu aina gani ya mashauri yanayofunguliwa kwa wingi. Mahojiano maalumu na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Mkoa wa Iringa, David Ngunyale yanabainisha kuwa kesi za unyanyasi wa kijinsia hususani za ubakaji, zinaongoza kwa kufunguliwa kwa wingi katika Mahakama mkoani humo.

Takwimu za mwaka 2016 zinaonesha kuwa jumla ya kesi 62 zilifunguliwa na kuanzia Januari hadi Juni mwaka 2017 tayari kesi 36 zimeshafunguliwa. “Matukio ya ubakaji katika mkoa wa Iringa yanazidi kushika kasi, kwa miezi sita ndani ya mwaka huu tayari kesi 36 zimefunguliwa, hali hii inaonesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu kutakuwa na kesi nyingi za namna hii” anasema.

Anasema kutokana na uwingi wa kesi hizo, mahakama inazipa kipaumbele cha kuzisikiliza na kuzitolea maamuzi kwa haraka iwezekanavyo, ingawa juhudi hizo zinakwamishwa na jamii. “Kesi za namna hii zinakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na baadhi ya walalamikaji kula njama na washitakiwa na mashahidi kutotokea mahakamani, jambo ambalo linachangia baadhi ya kesi kushindwa kuendelea,” anasema.

Kwa mujibu wa sheria, endapo mtu atabainika kuwa alishiriki katika kitendo cha ubakaji pasipo shaka, Mahakama hutoa adhabu ya kifungo cha miaka 30, viboko sita na fidia kwa familia ya muathirika wa tukio hilo. Aidha; Hakimu huyo Mfawidhi amesifu ushirikiano uliopo kati ya Mahakama na wadau wake mkoani humo ikiwa ni pamoja na Polisi, wanasheria na idara ya ustawi wa jamii katika uendeshaji wa kesi hizo.

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi, Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Iringa, Deusdedit Kasindo anakiri kuwapo ukubwa wa tatizo la ubakaji na kubainisha viashiria kuwa ni ulevi wa dawa za kulevya, pombe za kienyeji, kutelekezwa kwa watototo na umasikini. “Imani za kishirikina pia zinachangia ongezeko la kesi za aina hii kwa sababu waganga wa kienyeji wamekuwa wakiwadanganya watu kushiriki vitendo hivyo, jambo ambalo linachangia ongezeko hilo,” anasema.

Takwimu zinaonesha kwa mwaka 2016, kesi 259 zilizoripotiwa kwenye vituo vya polisi mkoani humo kesi 239 ziliwahusu watoto, ambapo kati ya hizo kesi 203 zilikuwa za kubaka, kesi 11 za kujaribu kubaka na kesi 25 za kulawiti. Pia takwimu hizo zinaonesha kuwa kesi za kubakwa wanawake zilikuwa kesi 18 na kujaribu kubaka ni kesi 2. “Katika kesi ambazo zinaripotiwa polisi zinaonesha watoto wanaofanyiwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia hususani ubakaji wana kati ya miaka 2 hadi 10,” anasema.

Kasindo anasema kati ya kesi 259 zilizoripotiwa kwenye vituo vya polisi, kesi 163 zilifikishwa mahakamani huku watuhumiwa 41 walitiwa hatiani na kesi zingine zinaendelea kusikilizwa. Kasindo anasema mwaka huu hadi kufikia mwezi Mei, Jeshi la Polisi limepokea kesi 139 na kati ya hizo kesi 121 zinawahusu watoto. Kesi zilizofikishwa mahakamani kwa mwaka huu ni 105, watuhumiwa 12 wametiwa hatiani na 45 wameachiwa, wakati kesi 48 zinaendelea mahakamani, jambo ambalo linafanya mafanikio kuwa ni asilimia 10.

Kasindo alibainisha changamoto kadhaa, zinazokwamisha kesi hizo kukamilika kuwa ni umri mdogo wa waathirika unaosababisha washindwe kujieleza kwa ufasaha, mashitaka kuwahusisha watu wa familia na maelewano ya pande mbili yanayofanywa nje ya mahakama.

“Tumeweka mikakati ya kupambana na vitendo vya ubakaji kwa kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari, kufanya mikutano na kufanya semina kwa viongozi walio karibu na wananchi, tukishirikiana na asasi za kiraia, ustawi wa jamii, lengo ni kuongeza mwamko wa kushughulikia kwa haraka zaidi mashitaka ya aina hiyo” anasema Kasindo anatumia fursa hiyo kukemea vitendo hivyo vya ubakaji na kusisitiza kuwa vitendo hivyo ni kosa la jinai na dhambi kwa Mungu huku akisisitiza jamii kuachana na ulevi wa kupindukia na imani za kishirikina.

Akizungumzia juhudi za kudhibiti na kutokomeza vitendo hivyo, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Iringa, Ismail Mambo anasema: “Tunapozungumzia ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto, tunamaanisha vile vitendo ambavyo vinamuathiri mtoto katika ukuaji wake hasa kiakili, kimwili na kihisia. Vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto ni ubakaji, ulawiti pamoja na kutelekezwa na wazazi.

Watoto wengi wanafungiwa majumbani bila msaada wowote, wapo wanaotelekezwa na kukosa matunzo kwa sababu za mimba zisizotarajiwa, ulemavu wa watoto, mimba za utotoni.” Anasema katika kukabiliana na hali hiyo, halmashauri imeweka mikakati na baadhi ikiwamo ya kuanzisha kamati za mitaa za kuhudumia watoto waishio katika mazingira hatarishi, “Kamati zitakuwa na kazi ya kuibua vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto vinavyotokea na kuviripoti kwenye kamati ya ulinzi na usalama na baadaye kufikisha kesi hizo polisi.

“Hapo hatua mbalimbali huchukuliwa kati ya polisi na ustawi wa jamii ikiwemo kuhakikisha kwamba mtoto mwathirika anapata haki stahiki ikiwa ni pamoja na kupata matibabu, kusikilizwa na kupatiwa huduma na taratibu za kisheria katika ngazi ya Mahakama. Aidha, Mambo anafafanua zaidi kuwa kwa sasa uelewa wa jamii katika suala la malezi ya watoto umeongezeka, ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo jamii ilikuwa haitoi taarifa kutokana na woga.

Anasema mikakati mingine ni pamoja na kutoa elimu ya malezi katika ngazi ya jamii, kwa kuanzisha vikundi vinavyotoa elimu na kusimamia utekelezaji wake na kutoa mafunzo kwa wasaidizi wa jamii wawili kwa kila mtaa, ambapo mitaa yote 192 ya Manispaa ya Iringa imefikiwa na mafunzo hayo.

Mambo anasema mikakati mingine ni ufuatiliaji wa karibu wa wataalamu na wanachama wa kamati ya ulinzi na usalama ngazi ya halmashauri katika kamati za watoto waishio katika mazingira hatarishi ngazi za mitaa na kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya suala zima la ulinzi na usalama wa mtoto.

Katibu Mkuu wa Taasisi ya DHI, NUREYN- Islamic-Iringa, Sheikh Shams Elmi Obsiye anasema: “Ni kweli tatizo hili lipo, kama viongozi wa dini tunajitahidi kuhamasisha jamii kupitia madrasa za watoto kwa kutoa elimu ya viashiria vya ubakaji mfano kununuliwa pipi, kupakatwa au kuitwa mchumba.”

“Tunatoa elimu ili wananchi wajue vitendo hivyo ni kosa la jinai na havimpendezi Mwenyezi Mungu. Pia tunakemea vitendo vingine vya unyanyasaji wa kijinsia kama wanaume kuwapiga wake zao,” anasema na kuongeza kuwa kwa mwezi hupokea malalamiko zaidi ya 30.

Obsiye anapendekeza kutolewa mafunzo ya jinsi ya kushughulikia kesi za ubakaji na unyanyasaji mwingine wa kijinsia kwa viongozi wa dini na kusisitiza jamii kushiriki katika mapambano hayo na kutoa elimu. Vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa kinjisia, vimekuwa vikishika kasi kila uchwao, hali ambayo inapelekea wasiwasi na hali ya kutoaminiana miongoni mwa wanajamii.