Kuna cha kujifunza uchaguzi Kenya

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) imemtangaza Uhuru Kenyatta (55) kuwa mshindi katika uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo uliofanyika Agosti nane mwaka huu. Wakenya wamemchagua Kenyatta awaongoze kwa muhula wa pili, kwa mara ya kwanza alichaguliwa katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2013.

Kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi wa Kenya, Rais anapaswa kuapishwa siku 14 baada ya kutangazwa kuwa mshindi endapo hakuna pingamizi la kisheria kortini. Jambo la msingi kwa Watanzania ni mambo gani ambayo Tanzania inaweza kujifunza kutokana na uchaguzi huo, katika kuendeleza demokrasia nchini.

Kiongozi wa Chama cha ACTWazalendo, Kabwe Zitto anasema jambo kubwa ambalo Tanzania inaweza kujifunza ni uwazi katika mfumo wa uchaguzi, na utoaji matokeo kwa haraka. “Uwazi katika mfumo mzima wa uchaguzi. Matokeo kwa haraka na pia kuendesha uchaguzi kwa namna ambayo malalamiko yamekuwa kwenye fomu za matokeo tu.

Tanzania inalo la kujifunza.” Kuhusu upigaji kura kwa Wakenya waishio nje ya nchi na wafungwa, Zitto anasema: “Mimi naunga mkono Watanzania waliopo nje kupiga kura. Rwanda wamefanya na Kenya pia. Tunaweza kufanya. Hata wafungwa Zimbabwe wanafanya na sisi tunaweza.”

Kuhusu kushindwa kwa Raila Odinga kwa mara ya nne Zitto anasema: “Ni uchaguzi. Lazima pawepo na mshindi na mshindwa. Raila amefanya kazi kubwa sana ya kujenga demokrasia Kenya. Ameshindwa lakini siyo mtu wa kubeza.”

Zitto anasema siasa za Kenya ni za kikabila kwa pande zote na kwamba, jambo hilo madhara yake ni makubwa kwa kuwa umoja wa kitaifa unakuwa mashakani, hivyo nchini hiyo inapaswa kuacha siasa kwa misingi hiyo ya kibaguzi.

Kuhusu utamaduni ya wanasiasa wanaoshindwa kutokubali matokeo, Zitto anasema: “Kama mtu haridhiki na matokeo lazima ayakatae. Uchaguzi ukiwa huru na haki watu watakubali matokeo.”

Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana anasema, kutokana na yaliyofanyika kwenye Uchaguzi Mkuu Kenya, umefika wakati kwa Serikali ya Tanzania kuruhusu mgombea binafsi.

“Wakati mwingine wananchi watataka kumchagua mtu, lakini wanaamua kutomchagua kwa sababu ameteuliwa na chama fulani,” anasema. Dk Bana anasema Tanzania iangalie namna uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unavyoweza kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na ukafanyika siku moja ili kupunguza gharama.

“Tumeona Wakenya wameweza kuchagua makundi sita ya ngazi za uongozi kwa wakati mmoja chini ya IEBC jambo ambalo linaonesha hata Tanzania inaweza kufanya hivyo.”

Anasema, Tanzania pia inaweza kuiga kwa kuruhusu Watanzania wanaoishi nje ya nchi kupiga kura kumchagua Rais wa nchi sanjari na kuruhusu wafungwa wapige kura kwa kuwa nao ni Watanzania.

Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa, Profesa Mwesiga Baregu anasema Wakenya wamefanya uchaguzi vizuri ingawa kulikuwa na changamoto mbalimbali. Anasema changamoto za teknolojia na hasa suala la udukuzi linaweza kufanyiwa kazi na hata nchi nyingine ikiwemo Tanzania zinaweza kujifunza kuhusu jambo hilo.

“Hata sisi huku bila kusemea upande wowote jambo kubwa ni kuonesha kuwa matokeo ni ya kuaminiwa, na si tena kuwepo na matokeo ambayo yanakuwa na mashaka ndani yake,” Katika uchaguzi huo, mchuano mkali ulikuwa baina ya Kenyatta na mgombea wa Muungano wa Vyama vya Upinzani (NASA), Raila Odinga (72).

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na IEBC, Kenyatta ametangazwa mshindi kwa kupata kura 8,203,224 sawa na asilimia 54.27, akifuatiwa na Raila aliyepata kura 6,762,224, sawa na asilimia ya 44.74. Kwa kuzingatia matokeo hayo, kuna tofauti ya kura 1,403,095 baina ya Kenyatta na Odinga.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu umefanyika katika vituo 40,883. Wapigakura milioni 19.6 walijiandikisha. Rais Mteule Kenyatta ametoa mwito wa amani na umoja. Katika uchaguzi wa mwaka 2013 Kenyatta aliibuka mshindi kwa jumla ya kura 6,173,433 sawa na asilimia 50.07 ya kura milioni 12.3 zilizopigwa.

Uchaguzi huo ulishirikisha wagombea wanane wa kiti cha urais. Mwaka 2013 Odinga aligombea urais kwa mara ya tatu. Kwa mara ya kwanza Daniel Arap Moi alimshinda katika uchaguzi wa mwaka 1997 na 2007 Mwai Kibaki alimshinda. Mwaka 2013 Kenyatta alimshinda Odinga kwa kura 832,887.

Katika uchaguzi huo, Mgombea Mwenza wa Kenyatta William Ruto na pia katika uchaguzi wa mwaka huu alikuwa huyo huyo. Marais wengine waliowahi kuiongoza Kenya ni Jomo Kenyatta ambaye ni baba mzazi wa Uhuru, Daniel Arap Moi na Mwai Kibaki. Odinga ni mtoto wa Makamu wa Rais wa kwanza wa Kenya, Jaramogi Oginga Odinga.