UCSAF na ukombozi wa mama lishe vijijini

KWA muda mrefu, teknolojia ya mawasiliano ya simu za mkononi imekuwa ikijikita mijini na kuyaacha maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara, hasahasa vijijini kuwa ‘kisiwa’ na hivyo kuachwa nyuma kwa mengi.

Hii inatokana na ukweli kuwa maeneo hayo ni magumu kufikika, gharama za kuyafikishia mawasiliano haya ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) ni kubwa na miundombinu ni duni. Hilo linasababisha gharama za uendeshaji zikiwamo za kupeleka mafuta na kuendesha minara ya simu kuwa kubwa.

Lakini kwa kuwa mawasiliano ni uchumi, maeneo hayo kuendelea kubaki kama kisiwa kimawasiliano maana yake ni kwamba uwezo wa watu walioko maeneo hayo katika kuboresha maisha yao pia hubaki nyuma.

Kwa kuliona hilo kuwa kikwazo kwa maendeleo ya taifa, mwaka 2006 Serikali ilianzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unaofadhili ujenzi wa minara ya simu katika maeneo hayo na mengine yenye shida ya mawasiliano.

Mkurugenzi Mtendaji wa UCSAF, Peter Ulanga anasema, hadi sasa mfuko umejenga minara 520 ya simu na inaendelea kujenga mingine 120 kusaidia wananchi wa vijijini kwa mawasiliano katika shughuli zao za kijamii na kiuchumi.

Anasema: “Tunapokamilisha ujenzi wa mnara, tunaingia mkataba na kampuni ya simu za mkononi (TTCL, Vodacom, Airtel au Tigo) ili wautumie kutoa huduma za mawasiliano kwa Watanzania wenzetu.”

Hivi karibuni gazeti hili lilitembelea baadhi ya wilaya na mikoa na kubaini namna mpango huo wa Serikali kupitia UCSAF ulivyowanufaisha wananchi wa kada mbalimbali kiuchumi na kuyapa maisha yao mabadiliko chanya.

Mwandishi alishuhudia na kuzungumza na baadhi ya wanawake katika mikoa ya Tabora, Shinyanga na Kigoma hususani wanaouza chakula walioeleza namna minara ya UCSAF ilivyobadili maisha yao na kuwakomboa kiuchumi.

Wilayani Urambo katika Mkoa wa Tabora, Astara Bitatuka wa kijiji cha Ndorobo anayefanya biashara ya mgahawa (mama lishe) katika Kijiji cha Nsenda anasema, minara iliyowekwa kijiji hapo imewapa ukombozi na usalama wa kiuchumi tofauti na siku za nyuma.

“Kabla hatujapata hii minara nilikuwa natumia nguvu na muda mwingi wa biashara kuzunguka vijijini kutafuta mahitaji kama kuku, au kwenda kununua mahitaji mengine ya mgahawa kama maharage, mchele na mafuta. Ilinibidi nimtume mtu kwa kumlipa, au mwanafamilia mwingine aache kazi nyingine za nyumbani,” anasema Astara.

“Baada ya simu hizi kuja, nawapigia simu wafugaji hata wa vijiji vingine wananiletea tena kwa bei tuliokwishakubaliana. Isitoshe, wateja wengine wanapiga simu kuweka oda ya chakula. Kwa kweli hii minara imeleta ukombozi. Tunashukuru TTCL kwani nao wameleta TTCLPesa,” anasema.

Anasema kwa wastani matumizi ya simu baada ya UCSAF kuweka minara ya simu kijijini Imalamakoye, yamemwongezea wastani wa wateja watatu kwa siku sawa na nyongeza ya wateja 90 kwa mwezi na hivyo, kuimarisha biashara na kipato chake.

Kijijini Singita, Kata ya Usando, Jimbo la Solwa wilayani Shinyanga Vijijini, Margaret Mwenda, anasema minara iliyowekwa kuhudumia Kijiji cha Itilima ukiwamo wa TTCL, umeimarisha usalama wa pesa anazopata katika biashara yake ya mama lishe.

Anasema: “Pesa ninayopata katika hii biashara ninaitunza mwenyewe kwa sababu sina akaunti ya benki na hivyo naiweka kwenye simu yangu, inakuwa salama, hivyo ujio wa simu umeleta faida nyigine ya kutunza fedha zetu.”

Anapoulizwa kwanini hatumii akaunti za benki, Margaret anasema: “Ukienda benki unakuta foleni, mara ujaze fomu, mara uandike saini huku biashara umefunga au umeachia mtu mwingine na unajua biashara haipendi mambo ya kuachiana achiana.

Sasa wakati mwingine pia unahitaji kuweka au kutoa pesa zako benki, lakini kwa muda huo wamefunga sasa inakuwa shida, lakini kwa simu mambo ni mazuri sana.” Kuhusu faida za kutunzia pesa kwenye simu anazidi kufafanua: “Wakati mwingine unatoka benki hujui mbaya wako ni nani au nani anakufuatilia.

Unaweza hata kuporwa njiani, lakini kwenye simu iwe TigoPesa, haloPesa au TTCL– Pesa unakwenda pale kibandani wakati wowote; mtu hajui kuwa labda umeenda kununua vocha, unaweka au kuchukua pesa zako kwa dakika mbili au tatu, unarudi kwenye shughui zako.

Hii inatoa muda mwingi kufanya kazi kuliko kupanga foleni.” Mwanamke huyo mjasiriamali anasema kabla maeneo yao hayajapata mawasiliano ya simu, alilazimika kwenda kupeleka faida ya biashara yake na mapato mengine kwa wazazi wake katika kijiji cha Mwamala, mwendo wa takriban nusu saa ili wamtunzie.

“Ilikuwa inabidi niwapelekee nyumbani wanitunzie maana mwenyewe ninashindwa kujizuia kuzitumia hata kwa mambo ambayo siyo ya muhimu sana,” anasema Margaret. Mkoani Kigoma katika Wilaya ya Kasulu, Semeni Mussa Moshi wa Kijiji cha Kumnyika anasema uwepo wa minara ya simu vijijini umechochea watu kufanya miamala kwa kutuma na kupokea pesa kupitia simu zao, hali ambayo ni rahisi na salama zaidi.

“Nilipomaliza kidato cha nne mwaka 2011, niliingia katika kibarua cha kusomba maji kwa mafundi wanaofyatua matofali wakati wa kiangazi… kwa wiki nilikuwa napata shilingi 6,000 au 7,000. Nikaona maisha yangu hayana tumaini; yanazidi kudidimia,” anasema Semeni.

“Tulipowekewa minara ya simu na kuanza kupata mawasiliano, nikajiunga na uwakala wa M-Pesa na ule wa kusajili laini za simu na pote huko, ninapata kamisheni nzuri tu.”

Anasema, alianza na mtaji wa shiulingi 300,000, lakini sasa yupo vizuri na mambo yanakwenda sawa (anakataa kutaja mtaji wake kwa sasa) na hivyo, hatarajii kuacha shughuli hizo na badala yake, ana mpango wa kuongeza vituo maana imekuwa mkombozi katika maisha yake kiasi cha kumudu kufanya ukarabati wa nyumba ya familia yao, jambo analosema bila UCSAF, lisingewezekana.

Katika Kijiji cha Nsimbo wilayani Kaliua mkoani Tabora, Mariamu Paul anayefanya biashara ya mama lishe anasema anajuta kutokuwa na simu huku akiapa kuitafuta haraka. Lakini kwa upande wake, Zainabu Mstaafu, mchuuzi wa nafaka kijijini hapo yeye anasema simu yake inamsaidia kutafuta wakulima wenye mazao na kuwagiza wamletee.

“Wateja wangu wananipigia simu kuniuliza kama nipo waniletee mahindi na wengine wanataka kujua kwanza nitanunua kwa bei gani… wengine wananiambia nisiondoke niwasubiri wako njiani wananiletea mahindi.”

Kwa nyakati tofauti, wanawake hao wajasiriamali wanasema minara ya simu katika maeneo yao yasiyofikika kirahisi wala kuwa na mvuto wa biashara imechangia kuboresha maisha ya familia zao kwa kusomesha watoto, kuchangia mahitaji ya lazima kama chakula, mavazi na matibu.

Mbali na wanawake hao, Samwel Gaspar, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kilimahewa, ambaye pia ni mfanyabiashara katika genge la chakula kijijini Mahembe Kigoma, anaishukuru UCSAF akisema kwamba kupitia simu, anapata maombi ya chakula kati ya manne hadi matano kwa siku.

Anasema: “Simu zimekuwa mkombozi mkubwa. Wakulima na wafugaji wengi wanaitumia kuniita nikanunue maharage na kuku. Kabla ya hapo, nilikuwa natumia baiskeli kutafuta vitu hivyo sasa gharama ya kwenda huko ni kubwa; jua kali, baiskeli saa nyingine inaharibika, unahitaji kula, lakini sasa ukiweka shilingi 1,000 kwenye simu, unamaliza mambo yote.

Kwa kweli serikali (UCSAF) imetukumbuka na kutujali sana.” Kiongozi wa Timu ya Masoko wa Vodacom wilayani Kasulu, Deogratius Chubwa anasema uwepo wa minara ya UCSAF umeongeza fursa za ajira kupitia njia mbalimbali zikiwamo za uwakala wa miamala ya pesa na usajili wa laini.