Kanuni maduka ya fedha za kigeni zinavyobadilika

MWAKA 1951, kulikuwa na sheria ya kudhibiti fedha za kigeni ambapo serikali kupitia Benki Kuu ndiyo pekee iliyokuwa ikiruhusiwa kumiliki fedha za kigeni. Wakati huo wa ukoloni, mwananchi aliyekuwa anahitaji fedha za kigeni alilazimika kwenda benki kuu na kabla ya kupewa fedha hiyo alitakiwa kutoa sababu za msingi ndipo apewe.

Hata hivyo, baada ya uhuru, mwishoni mwa miaka ya 1980 serikali ilianza kurasimisha vitu mbalimbali ambapo sekta hiyo nayo ilirasimishwa hivyo wananchi wakapewa leseni ya kuendesha biashara ya fedha za kigeni. Serikali ilitunga sheria ya fedha za kigeni ya mwaka 1992 sheria ambayo inatumika mpaka sasa.

Sheria hiyo ilimpa gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mamlaka ya kuanzisha maduka ya kuuza na kununua fedha za kigeni na pia mamlaka ya kutunga kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo ya kusimamia maduka hayo.

Sheria hiyo iliruhusu pia mwananchi kumiliki fedha hizo na kufungua akaunti ya fedha hizo, jambo ambalo awali haikuwa hivyo. Ofisa Msimamizi wa Maduka ya Kuuza na Kununua Fedha za Kigeni wa BoT, Kanuti Mosha, akifafanua suala hili anasema mwaka 1999, Gavana alitengeneza kanuni za kusimamia maduka hayo, lakini kwa kuwa maduka hayakuwa mengi, hakukuwa na masharti magumu.

“Mtu ukiwa na Sh milioni tano au sita alikuwa anaweza kufungua duka, lakini baada ya muda uchumi umekua, teknolojia ikakua, na soko la fedha likakua na kuonekana kuna uhitaji wa kubadili kanuni hizi,” Mosha.

“Mwaka 2008 kanuni hizo zilibadilika na ni kwa sababu hizo hizo za kukua kwa uchumi, teknolojia na soko la fedha za kigeni,” anasema. Mosha anasema kanuni za zamani ziliruhusu mtu mmoja mmoja kumiliki duka la namna hiyo, jambo ambalo ilikuwa ni vigumu kwa serikali kuyasimamia maduka hayo na kupata taarifa zao za biashara.

“Moja ya mabadiliko haya tuliyataka maduka kuwa kampuni, kwa kuwa kampuni maana yake lazima utimize sheria za makampuni ambayo ni pamoja na kutakiwa kutengeneza mahesabu na kupeleka marejesho kila mwaka,” anasema Mosha.

Baada ya mabadiliko hayo ya kanuni, Mosha anasema maduka hayo yalianza kuweka kumbukumbu na mahesabu yao vizuri na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikaanza kupata kodi stahiki.

Baada ya miaka kupita na teknolojia kuzidi kukua, kanuni zilibadilishwa tena na kutungwa mpya za mwaka 2015. Mabadiliko hayo ni pamoja na serikali kutambulisha mfumo mpya wa ukusanyaji kodi kwa kupitia mashine za kodi za kielektroniki (EFD) ambapo maduka hayo pia yalitakiwa kutumia mfumo huo.

“Kila duka lilitakiwa kuwa na mfumo wa kompyuta na takwimu ziende BoT na pia TRA,” anasema Mosha. Mabadiliko hayo pia yalihusisha ongezeko la mitaji ambapo mmiliki wa duka la kubadilishia fedha alitakiwa kuwa na mtaji wa Sh milioni 100 na walipewa muda wa miaka miwili kufikia viwango hivyo.

Muda huo ulikuwa unaisha Juni 30 mwaka huu. “Wakati watu wanasubiri kufikia kigezo cha mtaji wa Sh milioni 100, serikali imefanya marekebisho tena kwenye kanuni na kubadilisha mitaji iliyokuwepo kwenye kanuni hiyo ya mwaka 2015. Mitaji sasa takuwa ni sh milioni 300,” anafafanua Mosha.

Anasema serikali ya awamu hii ilitoa kipindi cha miezi mitatu pekee maduka hayo yaongeze mtaji na kufikia milioni 300 na hiyo ni kwa mujibu wa tangazo lililotoka Juni 30 mwaka huu kwenye gazeti la serikali ambapo mwisho ni Septemba mosi mwaka huu.

Kilichosababisha mabadiliko hayo makubwa Mosha anasema ni pamoja na BoT kwa kushirikiana na vyombo vingine kufanya uchunguzi kwenye maduka hayo na kubaini maduka mengi yalikua yanaficha mitaji yao halisi.

“Kwa mfano ukiangalia vitabu vyao vya mahesabu, wengi walikuwa wanaonesha mitaji ambayo siyo halisi, maduka mengi yalikuwa yanaonesha kila mwaka yanapata hasara lakini hali halisi ilionekana siyo kweli,” anasema.

Anabainisha pia kuwa wenye maduka hayo walikuwa wakifanya biashara zao nje ya mfumo wa kawaida ambao BoT unautambua huku wengine wakifanya miamala ambayo siyo ya hapohapo.

Anachukua fedha za mtu kisha anamtafutia fedha za kigeni kitu ambacho ni kinyume cha taratibu. Anasema kwamba baadhi ya maduka pia yalikuwa hayatoi risiti kwa kila muamala, kwa mujibu wa mfumo uliopo na kwamba mtu anapotoa risiti muamala huo ndiyo ambao unaenda BoT.

“Fedha ambazo zilikuwa zinatokana na biashara ya bila kutoa risiti ndizo ambazo zilikuwa zikitumika kufadhili biashara haramu kama za dawa za kulevya na utakatishaji fedha,” anasema.

Ofisa Msimamizi huyo anasema matokeo ya uchunguzi uliofanywa yanaonesha kwamba maduka hayo yalikiuka utaratibu wa uendeshaji, ndiyo maana serikali ilibadili kanuni na kuongeza mtaji ikiamini kwamba mtaji halisi uliokuwa unafichwa sasa utaoneshwa na kupata faida ambayo watatoa mapato stahili serikalini.

Kwa mujibu wa Mosha, BoT ilitoa taratibu nyingine mpya na kuelekeza mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kusimamisha utoaji wa leseni kwa sasa mpaka itakapotangazwa baadaye. Lengo la hatua hiyo anasema ni kushughulika na kuwasaili wenye maduka waliopo kwanza kabla ya kuwasaili wapya.

Nchi nzima kuna maduka ya kubadilishia fedha za kigeni 297 ambayo yana leseni ya BoT huku matatu ndiyo yakiwa ya daraja B. Katika kipindi hicho cha miezi mitatu wenye maduka wanatakiwa kuomba leseni upya, na ikiwa mtu hataomba mpaka muda huo kupita maana yake ni kwamba hataruhusiwa kufanya biashara hiyo.

“Na maombi yake yatafikiriwa ikiwa yatakidhi matakwa mapya ya utoaji wa leseni ikiwa ni pamoja na mtaji mpya wa Sh milioni 300 kwa daraja A. Kuna daraja B ambalo wamiliki wake isyo zaidi ya watatu,” anasema Mosha.

Kwenye mtaji wa milioni 300 Mosha anafafanua kwamba theluthi tatu ambayo ni sawa na Sh milioni 200 inatakiwa iwe ni mtaji, yaani fedha taslimu na inayobaki iwe ni thamani ya vitendea kazi. Katika mabadiliko hayo, wale wenye maduka zaidi ya moja wanatakiwa wayaunganishe na kuwa duka moja huku mengine yakitakiwa kuombewa usajili wa kuwa matawi huko baadaye.

“Kwenye masharti ya matawi tutaangalia eneo ambalo unataka kufanya kazi na tutakwambia uongeze kulingana na mahitaji,” anasema. Anasema maduka yote katika muongozo huo mpya, yanatakiwa kuweka kamera za CCTV ambazo zitakuwa kwenye ofisi, chumba cha kuhudumia wateja na pia kwenye kaunta.

Anasema lengo la kamera hizo ni kuimarisha usalama kwani kumekuwa na matukio ya wizi katika maduka hayo na pia kutumika kuangalia mwenendo wa maduka hayo hususuani kama wateja wanapewa risiti kulingana na muamala unaofanyika.

Anasema BoT ilitoa pendekezo kwa wale ambao hawajatimiza vigezo kuungana zaidi ya duka moja ili kuweza kidhi kigezo cha mtaji. Kutokana na mabadiliko hayo kuwa ni ya muda mfupi, wenyemaduka wengi waliomba mkutano na BoT wakiomba kuongezewa muda ili waweze kutimiza vigezo vilivyowekwa.

Anasema BoT kwa upande wake ilijiridhisha kwamba hatua zilizochukuliwa ni stahiki na muda unatosha hivyo hakuna haja ya kuongeza hasa ikizingatiwa wenye maduka wengi walikurupuka katika siku za mwishoni.

Kwa upande wa Zanzibar, Mosha anasema wenye maduka wameomba kuongea na BoT wafikiriwe hasa ikizingatiwa hali ya uchumi kwa upande huo iko chini, hivyo hawataweza kutimiza vigezo husika, ombi ambalo anasema linafanyiwa kazi.

Lakini anasisitiza kwamba biashara hiyo inasimamiwa na sheria na taratibu na kwambe yule ambaye hatoweza kutimiza vigezo atakaa pembeni na kuangalia biashara nyingine. “Ni bora tukabaki na maduka 50 ambayo yanafuata taratibu, yanarekodi fedha zote zinazoingia na kutoka, na yanalipa kodi, kuliko kuwa na maduka 300 ambayo hayalipi kodi na fedha zinaenda kufadhili biashara haramu.”

Mosha anatoa onyo kwa watu ambao wanaendesha biashara za kuuza na kununua fedha za kigeni kwa njia za magendo kwamba serikali inaendeleza msako. Adhabu kwa atakayefikishwa mahakamani na kupatikana na hatia anasema ni pamoja na faini ya Sh milioni 4 au kifungo cha miaka 14 au vyote viwili.