Kilimo cha GMO nchini kuanza na mazao manne

KUTOKANA na mabadiliko ya tabianchi duniani kote, watafiti mbalimbali wa kilimo wamekuwa wakitafuta njia ambazo zitawezesha kupata mavuno kwa wingi kwa maana ya kuwa na uwezo wa kustahimili magonjwa na wadudu waharibifu.

Njia hizo pia zitawezesha kupata virutubisho kwa wingi kama kwenye mchele, muhogo na mtama wenye vitamin A nyingi pamoja na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuvumilia ukame, tindikali na hali ya chumvi.

Mabadiliko hayo ya tabianchi yamefanya wataalamu kuanza michakato ya kuendeleza mazao yaliyofanyiwa mabadiliko ya kijenetiki (GMO), ambayo yameleta mafanikio katika baadhi ya nchi ikiwamo Afrika Kusini kwenye kilimo cha mahindi na Burkina Faso kwenye zao la pamba.

Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia nchini (OFAB) kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Nicholus Nyange anasema, hapa nchini ilipendekezwa teknolojia ya uhandisi jeni ianze kwenye mazao manne.

Zao la kwanza ni mahindi yanayostahimili ukame na bungua ambayo yanafanyiwa utafiti katika Kituo cha Utafiti Makutupora mkoani Dodoma. Jaribio la kupanda mahindi hayo lilifanyika Oktoba 5, mwaka jana.

Ukaguzi wa jaribio hilo ulifanyika Novemba 22 mwaka jana, na uvunaji ulikuwa Februari 14 mwaka huu. Kwa sasa kinachosubiriwa ni kibali kutoka serikalini ili hatua nyingine ya utafiti huo iendelee.

Anasema zao pili ni muhogo ambalo limekuwa likishambuliwa na magonjwa ya batobato na michirizi ya kahawia. Hivi sasa kuna aina mbalimbali ya mbegu za muhogo zinaboreshwa kwa njia ya uhandisi jeni katika maabara ya Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mikocheni (MARI) kilichopo Dar es Salaam.

Utafiti wa muhogo hivi sasa unafanyika ndani ya maabara. Na aina ya mbegu za mihogo inayofanyiwa utafiti ni Rushura, Karatasi, Gago, Milundikachini, Marekani na Mwarusha ambayo imetoka katika mikoa ya Kagera, Tanga na Mwanza.

Nyange anasema zao lingine lililopendekezwa ni migomba yenye ukinzani dhidi ya ugonjwa wa mnyauko. Kwa sasa watafiti wanatumia miche ya migomba iliyosafishwa (tissue culture) ili kuwapatia wakulima mbegu safi.

Ugonjwa wa mnyauko ulishambulia zao la migomba katika Mkoa wa Kagera hali iliyowafanya wananchi kutafuta mazao mbadala ya mihogo na viazi vutamu. Na zao la nne lililopendekezwa ni pamba yenye ukinzani kwa wadudu waharibifu ambalo hapa nchini hulimwa na wakulima wadogo katika mikoa 15 na wilaya 46 za Tanzania. Zao la pamba kwa nchi ya Burkina Faso imefanya vizuri kwani wao walishaanza kutumia GMO.

Aidha, pamoja na kwamba Tanzania haijaanza kutumia mazao ya GMO, kwa kuwa yapo kwenye majaribio lakini tayari wananchi wanatumia bidhaa hizo kutoka nchi nyingine ambazo zipo sokoni.

Kwa mfano, chakula cha GMO katika soko la Tanzania ni corn flakes na pia nguo ambazo huvaliwa na watu wengi, kwa kuwa asilimia 80 ya pamba yote inayolimwa ulimwenguni ni ya GMO.

Mbali na nguo, pia mafuta ya pamba za GMO hayana protini hivyo hutumika kwa chakula na vipodozi, na nchi za Ulaya huagiza bidhaa za pamba hiyo kwa chakula cha binadamu na mifugo.

Mtafiti wa zao la pamba kutoka Kituo cha Utafiti Ukiliguru Mwanza, Stellah Chirimi anasema kutokana na mabadiliko ya tabianchi wametoa mafunzo mkoa wa Geita na Tabora ili wakulima waachane na kilimo cha mazoea na walime kisasa kwa kufuata maelekezo kutoka kwa maofisa kilimo, watafiti pamoja na wataalamu wa kilimo.

“Malengo ya elimu tuitoayo ni kuwafanya wakulima wa Kanda ya Ziwa wazalishe kwa zaidi ya asilimia 99, ili kuwe na malighafi ya kutosha kwenye viwanda vya ndani na nje ya nchi,” anasema.

Mkuu wa Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Peresi Magiri anasema Tanzania hivi sasa inazungumzia uchumi wa viwanda hivyo kila mtu anapaswa kushiriki katika kuinua uchumi wa viwanda. “Tunataka kuona tunaboresha uzalishaji wa mazao.

Tukiwasaidia wakulima wetu wakazalisha kisasa na kutumia mbegu zinazokinzana na magonjwa tutafika,” anasema. Anawataka wataalamu kupeleka mbegu bora za mihogo katika wilaya hiyo ili wazalishe mazao mazuri.

Mkuu wa Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, Anjelina Kwinga anasema wanahitaji msaada zaidi wa kisayansi katika kilimo ili waweze kuwasaidia wakulima ambao wamekata tamaa kutokana na mazao yao kushambuliwa na wadudu.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Hamim Gwiyama anaiomba serikali na wadau kushiriki kutafuta wawekezaji watakaojenga viwanda vya juisi na usindikaji dengu.

Mratibu wa OFAB, Philbert Nyinondi anasema lengo la mafunzo ni kuwajengea uwezo maofisa ugani ili wawasaidie wakulima kulima kilimo chenye tija na kuwaonesha mbinu za kibayoteknolojia zinavyoweza kusaidia kuongeza uzalishaji na kuondoa changamoto.

Anasema wakati serikali ikitekeleza kwa vitendo mpango wa kuifanya Tanzania ya viwanda, lazima maandalizi yafanyike kwa wakulima kuwawezesha kuchangamkia fursa hiyo kwa kuzalisha mazao hayo kwa tija ili kunufaika na mpango.

Katika kufikia uchumi wa viwanda ni muhimu Serikali ikachukua hatua mahsusi na za haraka kuhakikisha hatubaki nyuma katika karne hii ya sayansi na teknolojia pamoja na ugunduzi. Hivyo bayoteknolojia ina uwezo mkubwa wa kuchangia katika maendeleo ya nchi katika sekta za kilimo, afya, viwanda na mazingira.

Katika kilimo teknolojia ya uhandisi jeni ina uwezo wa kuongeza wingi na ubora wa mazao kwa kuwa wakulima duniani wanaopanda mazao ya GMO wamepata faida kubwa kiuchumi.