Wasichana hukumbwa na changamoto za masomo katika nchi hizi

HATIMAYE Umoja wa Mataifa umetoa ripoti inayotaja nchi 10 duniani ambapo wasichana hukumbwa na changamoto za kupata masomo. Katika ripoti hiyo nchi ya Sudan Kusini imetajwa kama mahala pabaya zaidi duniani katika masuala ya masomo kwa wasichana.

Mijadala kuhusu shule zilizo nchi tajiri uhusisha masuala tofauti, hasa ni masomo yapi yanayofaa kutiliwa maanani, nani anafaa kusaidiwa zaidi na ni kipi kinahitaji fedha zaidi. Lakini kwa familia zilizo katika nchi zinazoendelea, masuala kuhusu masomo yanaweza kuwa rahisi tu.

Je, kuna fursa yoyote ya kwenda shuleni? Takwimu kutoka Umoja wa Mataifa inadadisi kuwa “hakujawa na hatua zozote” katika muongo mmoja kutatua ukosefu wa shule katika maeneo yaliyo maskini zaidi duniani.

Ripoti zaidi ilichunguza ubora wa elimu, na Umoja wa Mataifa ukasema kuwa matokeo yalikuwa ni ya kushangaza, kukiwa na zaidi ya watoto milioni 600 walio shuleni lakini wanaopata masomo duni.

Nchini Niger, wanawake wanne kati ya watano wanasalia kutojua kusoma na kuandika. Kati ya nchi zote 10, wengi wa wale wanaokosa fursa za kusoma ni wasichana. Hizi ni nchi zilizo na migogoro, ambapo familia nyingi zinakumbwa na hali ya umaskini, afya duni, lishe duni na kufukuzwa makwao kutokana na vita na mizozo.

Wasichana wengi wadogo hufanya kazi badala ya kwenda shuleni. Na wengi huolewa wakiwa wadogo, na kuzima fursa yoyote ya kupata masomo. Takwimu hizo kutoka Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa wasichana wana uwezekano mara mbili zaidi wa kukosa masomo katika maeneo ya mizozo.

Ripoti kutoka nchini Chad zinasema migogoro ya mara kwa mara nchini humo imetatiza masomo ya mamilioni ya wanafunzi. Ripoti nchini Chad ilihusisha idadi ya wasichana wasiokuwa na nafasi katika shule za msingi, idadi ya wasichana wasiokuwa na nafasi katika shule za sekondari, idadi ya wasichana wanaohitimu kutoka shule za msingi na idadi ya wasichana wanaohitimu kutoka shule za sekondari.

Viwango vingine ilikuwa ni miaka ambayo wasichana huanza kwenda shule, idadi ya wanawake wasiojua kusoma na kuandika na idadi ya walimu ikilinganishwa na wanafunzi. Katika baadhi ya nchi kama Syria, hakukuwa na takwimu za kubainisha ili kuwekwa katika orodha.

Zifuatazo ni nchi 10 ambapo wasichana hupata changamoto za kusoma: Sudan Kusini: Zaidi ya robo tatu ya wasichana hawakufi ka shule ya msingi. Jamhuri ya Afrika ya Kati: Kuna mwalimu mmoja kwa wanafunzi 80 Niger: Asilimia 17 pekee ya wanawake kati ya miaka 15 na 24 wanaweza kusoma na kuandika.

Afghanistan: Kuna pengo kubwa la jinsia huku uwezekano wa wavulana kuwa shuleni kuliko wasichana ukiwa juu. Chad: Masuala ya kijamii na uchumi yanawazuia wasichana na wanawake kupata masomo. Mali: Asilimia 38 pekee ya wasichana huweza kuhitimu kutoka shule za msingi.

Guinea: Wakati wastani wanaotumia wanawake zaidi ya miaka 25 katika masomo ni chini ya mwaka mmoja. Burkina Faso: Asilimia 1 pekee ya wasichana humaliza masomo ya sekondari. Liberia: Takribani theluthi mbili ya wanafunzi waliotimiza umri wa kuenda shule za msingi hawaendi shuleni.

Ethiopia: Wasichana wawili kati ya watano wanaolewa kabla ya kufi kia umri wa miaka 18. Ukosefu wa walimu wa kutosha ni tatizo ambalo lilishuhudiwa kwenye nchi maskini. Mwaka jana, Umoja wa Mataifa ulisema kuwa walimu milioni 69 zaidi, wanastahili kuajiriwa duniani kufi kia mwaka wa 2030 ikiwa ahadi za kimataifa kuhusu masomo zitahitajika kutimizwa.