Pembejeo bora zinavyoweza kuchochea ukuzaji kilimo

KILIMO ni sekta inayotegemewa kiuchumi na Watanzania zaidi ya asilimia 75, kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa kitakwimu uliofanywa na mashirika tofauti ya ndani na kimataifa, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), kwa mujibu wa ripoti yake ya 2013, kilimo kinachangia asilimia 30 ya pato la ndani (GDP) na asilimia 64 ya pato linalotokana na mauzo nje ya nchi.

Kilimo ni sekta inatoa ajira mara 11 zaidi ya sekta nyingine za uzalishaji nchini, hivyo kuifanya kuwa na umuhimu wa pekee katika kukuza uchumi wa nchi na kustawisha maendeleo ya watu.

Ni kutokana na umuhimu huo, mwaka jana Baraza la Kilimo nchini (ACT) liliratibu utafiti uliojielekeza katika mifumo ya usimamizi kwa matumizi ya pembejeo za kilimo, mnyororo wa usambazaji na namna zinavyochochea uzalishaji kwa mkulima.

Utafiti huo uliofanywa na kampuni ya Match Maker Associates kwa niaba ya ACT, ulielekezwa katika mikoa yenye kanda zinazonufaika na mradi wa SAGCOT na Kaskazini mwa nchi.

Ofisa anayeshughulikia sera katika ACT, Laetitia William anasema utafiti huo ulifanyika kwenye wilaya tatu na kuzilenga pembejeo chache ambazo ni mbolea, mbegu na kemikali zinazotumika kwenye kilimo.

Wilaya hizo na mazao yaliyotumika katika utafiti huo kwenye mabano ni Mbozi na Babati (mahindi), Kilombero (mpunga), Babati (alizeti na maharage). Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Kilimo, mahitaji ya mbegu zilizoboreshwa nchini yanakadiriwa kuwa zaidi ya tani za ujazo 120,000 kwa mwaka wakati kiasi kinachosambazwa ni tani za ujazo 35,352 sawa na asilimia 59.

Hata hivyo, ripoti hiyo inaeleza kuwa matumizi ya mbegu hizo yapo kwa kiwango kidogo, ikikadiriwa kwamba asilimia 25 ya mazao yanayovunwa yanatokana na mbegu zilizoboreshwa wakati asilimia 75 ni kutoka kwenye mbegu za asili.

Hali hiyo inatokana na ukubwa wa bei inayotozwa kwa mbegu zilizoboreshwa, upatikanaji wake, miundombinu na mtandao duni katika usambazaji. Mtafiti John Alinanuswe kutoka Match Maker Associate Limited, anasema utafiti huo, pamoja na mambo mengine ulibaini kuwa kutokana na upatikanaji fedha usiokuwa wa uhakika kwa Taasisi ya Uthibitisho Rasmi Mbegu (TOSCI), wakati mwingine unasababisha kuchelewa kwa utekelezaji wa majukumu inayojipangia hususani kwenye ofisi zake zilizopo Arusha, Mwanza, Mtwara, Njombe na Morogoro.

Hali hiyo, kwa mujibu wa taarifa ya utafiti, imechangia pia sehemu ya ziara za ukaguzi wa TOSCI kukasimiwa kwa maofisa wa serikali ngazi ya wilaya. Alinanuswe anasema licha ya Kamati ya Taifa ya Mbegu (NSC) kuitisha mkutano wa wadau wa mbegu mara moja kwa mwaka, lengo likiwa ni kujadili masuala yanayohusiana na sekta hiyo, mahudhurio si ya kuridhisha kutokana na ushiriki kuwa suala la hiari.

Hata hivyo, ripoti hiyo inakosoa kwamba vikao hivyo vinaitishwa na kufanyika kitaifa wakati katika ngazi ya wilaya ufanisi wake ni mdogo na mara nyingi havifanyiki kutokana na sababu tofauti ikiwamo taasisi za wadau wa pembejeo za kilimo kutohudhuria.

Aidha, taarifa ya kitengo cha zana za kilimo katika Wizara ya Kilimo, inaonesha kuwa mahitaji ya mbolea yaliongezeka kutoka mita za ujazo 485,000 kwa msimu wa 2011/2011 kufikia 885,019 mwaka 2015/2016.

Mtafiti Alinanuswe anasema utafiti uliofanywa umebaini kuwa ubadilishanaji taarifa kati ya mamlaka zinazosimamia sekta ya kilimo nchini dhidi ya wadau wanaoshirikiana nao ni mdogo. “Katika majadiliano na mamlaka tofauti za usimamizi wa kilimo, hatukupata ushahidi wa kumbukumbu za pamoja za wadau wanaojihusisha na uingizaji na biashara ya pembejeo za kilimo,” anasema.

Hata hivyo, mwakilishi wa Tosci, Mtafiti Mwandamizi Doroth Ole Meiludi anasema hali hiyo imeboreshwa na kwamba miongoni mwa mamlaka hizo na hususani taasisi hiyo ya uthibitisho wa mbegu ina kumbukumbu hizo zinazosaidia kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Lakini Alinanuswe anasema ukosefu wa kumbukumbu unasababisha ugumu katika kuisimamia sekta ya kilimo, kuwatambua wanaoshiriki vitendo viovu dhidi ya pembejeo na kuwachukulia hatua zinazostahili.

Anasema matokeo hayo yanaonesha kuwa mamlaka za usimamizi zinakabiliwa na upungufu wa rasilimali watu na fedha, akizitaja kuwa ni nyenzo muhimu zinazochochea ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wakati.

Kuhusu mnyororo wa usambazaji pembejeo nchini, matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwapo kiwango duni cha uratibu wa pamoja wa shughuli za taasisi zinazoundwa na kampuni za uingizaji na biashara ya pembejeo.

Kampuni hizo zipo huru kujiunga na taasisi tofauti zilizoundwa ambazo ni pamoja na Chama cha Wafanyabiashara ya Mbegu (Tasta) na Chama cha Mawakala wa Mbegu (Tanada).

Alinanuswe anasema taasisi hizo zimebainika kupitia utafiti huo hazina uratibu wa pamoja na hakuna mfumo wa kuwezesha zikidhi sera na kanuni za mfumo wa usambazaji pembejeo nchini na kwamba hazijajiunda kusaidia shughuli za wasambazaji pembejeo kuwa na ufanisi.

Mtafiti huyo anasema stadi za utawala wa biashara kwa washiriki wengi wa pembejeo za kilimo hazipo kwa kiwango cha kuibua uwazi na ufanisi katika mfumo wa utoaji huduma husika.

Alinanuswe anasema ongezeko la matumizi sahihi ya pembejeo linaweza kuchangia kuongezeka uzalishaji na faida kwa wakulima. Utafiti unabaini kuwa sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwamo ufinyu wa masoko, ubovu wa miundombinu, ukosefu wa taarifa sahihi, fedha na bima, hali inayoweza kufifisha ufanisi kwa wakulima, ikiwa hazitapatiwa ufumbuzi.

Wakati huo huo utafiti umebaini kiwango cha uwapo wa pembejeo bandia za kilimo kushuka kwa mwaka jana ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2012. Anasema watoa taarifa katika utafiti huo walieleza kuwa mbolea, mbegu na viuatilifu haziwaathiri kwa kiwango kinacholingana kama ilivyokuwa awali, akitoa mfano kada chache kama za watumishi katika halmashauri za wilaya na wakulima pekee, walizungumza uwapo wa mbolea bandia.

Akasema kada hizo pamoja wafanyakazi wa kampuni za mbegu walieleza kuwa takribani asilimia 20 ya mbegu zilizopo kwenye soko zina ubora hafifu unaoziweka katika kundi la pembejeo bandia.

Waliohojiwa katika utafiti huo, wamekaririwa wakieleza kuwa hali ya pembejeo bandia ni mbaya zaidi kwa upande wa viuatilifu. MAPENDEKEZO Utafiti huo unapendekeza, pamoja na mambo mengine, kuwapo mapitio yenye lengo la kuboresha mamlaka za usimamizi katika sekta ya kilimo, kuboresha uratibu miongoni mwa mamlaka hizo ili zifanye kazi zikilenga kuboresha huduma kwa mkulima na kumpunguzia gharama za uzalishaji.

Mapendekezo mengine ni kutangaza kwenye gazeti la serikali majina ya wakaguzi wa mbegu, mbolea na viuatilifu katika ngazi za wilaya na kuwajengea uwezo ili watimize wajibu wao kwa ufanisi.

Pia kufanikisha upatikanaji wa taarifa zinazohitajika katika kusajili, biashara na kuingiza pembejeo za kilimo. Kuongeza kiasi cha faini kwa wahusika wa pembejeo bandia na fidia kwa waathirika wa vitendo hivyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Janeth Bitegeko anasema mkutano wa kujadili matokeo ya utafiti huo ni jukwaa muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho kasi ya utendaji kazi wa serikali ni kubwa, hivyo kuwapo uwezekano wa upungufu kadhaa kufanyiwa kazi tangu kufanyika kwa utafiti huo.

Bitegeko anasema kilimo ni biashara inayochangia maendeleo ya nchi, ustawi na uboreshaji huduma za jamii kutokana na fedha zinazopatikana kupitia kodi mbalimbali zinazotozwa kwenye sekta hiyo.

Ni kutokana na hali hiyo, Bitegeko anasema baraza limejikita katika kujenga uwezo wa wakulima na wadau wengine wa kilimo kuhusiana na mnyororo wa thamani ya mazao hususani katika kulima, kuvuna, kuuza na masoko.