Kusuasua mipango ya kuhimili ukame na umasikini Chamwino

WAKULIMA wa vijiji vya Chamwino, Buigiri, Chinangali II na Mwegamile, wilayani Chamwino katika Mkoa wa Dodoma, wanakabiliwa na ukosefu wa chakula na kipato ambao umechochewa na ukame na mvua zisizotabirika, zilizosababisha washindwe kuzalisha mazao shambani.

Licha ya kuwapo mipango na mikakati kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa ya kilimo kinachohimili na kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi, wakulima hawa wanakabiliwa na umasikini ambao chanzo ni mazao yao kukauka kutokana na ukame.

Mpango mkakati wa miaka mitano (2012-2017) wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino katika eneo la kilimo, unasisitiza halmashauri kufanya kilimo cha umwagiliaji huku ikielezwa kwamba, Wilaya ya Chamwino inafaa kwa kilimo hicho.

Mpango mkakati huu unaainisha kuwa jamii ya wakazi wa Chamwino inayotegemea kilimo na ufugaji haijanufaika ipasavyo na kilimo kwa sababu ya utegemezi wa kilimo kinachotegemea mvua. Kwa mujibu wa mpango mkakati huo, kati ya hekta 563,920 zinazofaa kwa kilimo, hekta 246,821 sawa na asilimia 44, ndizo zinatumika kwa uzalishaji wa mazao.

Asilimia zilizobaki, ardhi inayofaa kwa kilimo inabaki bila kulimwa. Wilaya hii yenye kilometa za mraba 8,056, kulingana na sensa ya makazi na watu ya mwaka 2012, ina idadi ya watu 330,543.

Asilimia 90 ya wakazi wanategemea kilimo na ufugaji. Sehemu ya mpango mkakati huo wa wilaya ya Chamwino inaweka bayana kuwa utegemezi wa kilimo cha mvua umefanya sekta ya kilimo kushindwa kuchangia uchumi wa wilaya ya Chamwino na watu wake kwa maana ya kuwa na kipato, ajira na kuhakikisha usalama wa chakula.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chamwino, Athumani Masasi anakiri kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi; kwa maana ya ukame na mvua zisizotabirika, zinajionesha wazi kwa wakulima. Anasema katika msimu wa mwaka 2016/17, zimezalishwa tani 82,569 za chakula wakati mahitaji halisi ya wilaya kwa mwaka ni tani 87,518.

Hivyo upungufu ni tani 4,949 za mazao ya chakula. Katika mahojiano na wakulima 40 kwenye vijiji vya Chamwino, Chinangali II, Buigiri na Mwegamile, asilimia 90 majibu yao yanadhihirisha kutotekelezwa kwa mbinu za kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabia nchi.

Wakulima hao kwa nyakati tofauti, wanaeleza kuwa hawatumii mbegu bora zenye ukinzani dhidi ya ukame zinazouzwa madukani. Badala yake, wamekuwa wakitumia mbegu wanazozalisha wenyewe mashambani. Sababu zinazotolewa ni pamoja na ukosefu wa fedha za kununua mbegu hizo.

Kwa mujibu wa Mpanduka, kilo ya uwele huuzwa Sh 2,000; mtama mweupe Sh 5,000 na kunde ni Sh 2,000. “Ni vigumu kwa mkulima wa kawaida kumudu kununua mbegu za kutosheleza mashamba yote,” anasema Jeremiah Mpanduka ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwegamile. Kilio kingine cha wakulima ni kukosa maelekezo ya karibu ya wataalamu juu ya mbinu za kilimo na ufugaji bora.

“Kama ni ushauri wa wataalamu, huwa tunaupata katika mkutano mkuu wa kijiji au ikitokea ziara za viongozi kama vile mkuu wa wilaya, ...ukimhitaji (ofisa ugani) ni mpaka umuite na umtafutie usafiri,” anasema mkazi wa kijiji cha Buigiri, Newston Goi. Kwa mujibu wa sheria ndogo za kilimo, wajibu wa ofisa ugani ni pamoja na kutoa programu ya kilimo ya mwaka kulingana na hali ya hewa.

Programu itazingatia aina ya mazao kwa msimu, aina ya mbegu, namna na wakati wa kupanda, namna na wakati gani wa kuvuna na kuhifadhi mazao baada ya kuvunwa. Wakati wowote wa saa za kazi, ofisa ugani ataweza kuingia kwenye eneo la kilimo kwa madhumuni ya kusimamia utekelezaji. Atapanga ratiba ya kutembelea mashamba ya wakazi kujionea kama wanatekeleza wajibu wa kulima na kutunza mashamba.

Maofisa kilimo wa vijiji na kata wanasema wamekuwa wakifanya kazi kwa kutimiza wajibu kulingana na majukumu yao yaliyoainishwa. Ofisa Mifugo wa Kata ya Buigiri, Stephano Adeline anatoa mfano kuwa mwaka jana kila kata ilitakiwa kuandaa shamba la kuzalisha mbegu za muhogo kwa lengo la kuzisambaza kwa wakulima. “Baada ya kupata mbegu hizo kutoka halmashauri, tulitengeneza shamba lakini mbegu zilikauka kutokana na ukame.

Bila mvua au mbinu nyingine za upatikanaji maji, ni vigumu kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi,” anasema Adeline. Majukumu mengine ambayo maofisa hawa wa vijiji na kata wanasema wamekuwa wakitekeleza, ni kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wakulima kama vile, kupanda mazao yanayohimili ukame na ya muda mfupi.

“Sisi tunafanya wajibu wetu kulingana na uwezo wetu na rasilimali zilizopo... kwa mfano, inapokuja suala la uchimbaji visima vikubwa kwa ajili ya kufanya umwagiliaji na si kutegemea mvua, sisi tunaitegemea halmashauri,” anasema Ofisa Mifugo wa Kata ya Chamwino, David Msimbe.

Msimbe anafafanua: “Sisi kama kuna vitu ambavyo vinatuhusu, lazima tushirikishe wilaya. Mfano kama ni shamba darasa, hapo unazungumzia fedha. Kwa mfano, ukizungumzia namna bora ya kupanda malisho, lazima halmashauri itenge maeneo ya malisho. Sisi ni wadogo.

Wakati mwingine wananchi wanatubebesha mizigo mikubwa ambayo hatuwezi.” “Tunapowatembelea, kama ng’ombe anaumwa, unamshauri, atafute dawa. Mimi kazi yangu ninakuwa nimemaliza,” anasema Msimbe.

Katika maelezo ya wataalamu hawa katika ngazi ya vijiji na kata, wanaweka wazi kwamba hawafahamu vizuri mipango na miongozo iliyoandaliwa kwa ajili ya kutekeleza kilimo kinachohimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ofisa Mifugo huyo wa Chamwino, Msimbe anaweka bayana akisema: “Mimi ninachokiona, mabadiliko ya tabianchi nayaelewa kwa sababu nimesoma. Lakini mpango mkakati wa kitaifa au wa kiwilaya, kwetu sisi tunakuwa hatufahamu vizuri. Hatujui wilaya imejipangaje. Tunatumia uzoefu tu wa kule chuoni ni namna gani tuwahudumie wakulima na wafugaji.”

Ofisa Kilimo wa Wilaya, Godfrey Mnyamale, anakiri kuwa maofisa hao hawajajengewa maarifa ya kutosha juu ya mikakati ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi. “Wataalamu wanahitaji kujengewa uwezo zaidi juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima, bajeti ya halmashauri haitoshelezi kuwezesha mipango ya kukabiliana na tabianchi,” anasema.

Bila kutaja fedha ambazo halmashauri imepewa, Mnyamale anafafanua: “Bajeti ya serikali inatengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi iliyoibuliwa na wananchi ingawa upatikanaji wa fedha za maendeleo kwa mwaka 2015/16 -2016/17 haukuwa mzuri hivyo baadhi ya shughuli kutotekelezeka.”

Ufinyu wa bajeti unaathiri pia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano (2012-2017) wa halmashauri ambao pamoja na masuala mengine, unataja kilimo cha umwagiliaji kuwa kinafaa kutekelezwa katika Wilaya ya Chamwino. Matokeo yake, kati ya vijiji 78 vya wilaya hii, skimu za umwagiliaji zilizopo ni Chinangali II (ekari 300) Huzi (ekari 200), Buigiri(ekari 100) Dabalo (ekari 120) na Chalinze (ekari 296).

Wakati huo huo hata vijiji ambavyo skimu hizo zinafanya kazi, si wakulima wote wanaonufaika. Kwa mfano, skimu ya Buigiri ambayo ilianza mwaka 1957, inanufaisha wakulima 139 sawa asilimia 4.5 ya wakulima 3,084 waliopo katika Kata ya Buigiri.

Kwa mujibu wa Ofisa Kilimo wa Kata ya Buigiri, Adeline, idadi ya wakulima walio ndani ya skimu wenye miundombinu ya umwagiliaji ni 97 na walio nje ya skimu wanaotumia pampu za kusukuma maji ni 42. Skimu hii inayoratibiwa na Umoja wa Watumia Maji Buigiri (UWAMABU), ilianza kutumika kwa umwagiliaji wa mifereji iliyoboreshwa mwaka 2009/2010.

Awali ilikuwa na ekari 30 tu zilizokuwa zinatu mika na sasa imepanuliwa na kufikia ekari 100 ambazo bado hazikidhi mahitaji. “Kama kijiji kizima (wakulima) tungeweza kuingia kwenye hii skimu, kijiji kingekuwa na neema…wala usingesikia habari za watu wanaotegemea kuuza kuni ili wapate fedha za kununua chakula. Ungeona watu wakiuza mboga za majani na mahindi,” anasema Yohana Masima, mkazi wa Kijiji cha Buigiri.

Masima ambaye ana shamba la nusu ekari nje ya skimu ambako analima pilipili, mahindi na chainizi, anafafanua, “Mimi siko ndani ya skimu.Ila nimekuwa nikitumia maji yanayotiririka ...yananisaidia sana.

Japo tunalia njaa, lakini siyo kama wenzetu ambao hawapati maji hata kidogo,” anasema. Akielezea nafasi ya halmashauri katika utekelezaji wa kilimo cha umwagiliaji, Ofisa Kilimo wa Wilaya, Godfrey Mnyamale anasema wilaya ina eneo linalofaa kwa umwagiliaji lenye hekta 9,191 lakini zinazotumika kwa umwagiliaji ni hekta 1,656.

“Ukosefu wa fedha za kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji hasa mabwawa, visima na nishati ya kusukuma maji ndiyo sababu kubwa ya kutosambaza au kujenga skimu kila kijiji,” anasema Mnyamale.

Mkurugenzi wa halmashauri, Masasi anasema wanaimarisha skimu zilizopo na wakati huo huo wanajenga nyingine nne za umwagiliaji .Masasi anataja skimu hizo zinazojengwa na ekari zake kwenye mabano katika vijiji vya Suli ( 100), Fufu ( 100), Chiboli ( 100), Mvumi Makulu ( 140) na usanifu wa bwawa la umwagiliaji la Membe ekari 4,000.

Mkuu wa Idara ya Mazingira katika iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi , Shakwaanande Natai anasema wao kama serikali kuu, wanao wajibu wa kuweka mkazo na nguvu ya kuhakikisha miongozo na mikakati inayoandaliwa kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi, inafika kwenye halmashauri hadi kwa wakulima.

“Familia ya kilimo ielimishwe ifafahamu sera, miongozo na mikakati iliyowekwa inasema nini? Inataka nini? Mbinu mbalimbali zilizo kwenye miongozo zikoje? Je, tunaweza tukazijaribu? Ili wakulima waichukue na waweke kwenye vitendo,” anasema Natai.

Mkuu huyu wa idara ya mazingira anasema miongozo imeandaliwa lakini wao kama serikali kuu hawajapata fedha za kutosha kuisambaza kama inavyotakiwa ili wakulima wote waelewe athari za mabadiliko ya tabia na mbinu za kuhimili.

Hata hivyo mkuu huyu wa idara anasisitiza halmashauri na wataalamu kutumia utaalamu wao kuwafundisha wakulima mbinu mbalimbali kama vile uvunaji maji ya mvua zinaponyesha na kuyahifadhi vizuri.

Kwa ujumla, Ofisa Mipango wa Wilaya ya Chamwino, Paschal Masatu anakiri kuwa mipango iliyopo, kama ingetekelezwa kwa kiwango kikubwa, umasikini unaotokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ungepungua kama si kukoma.

“Lakini kikwazo kikubwa ni rasilimali za utekelezaji,” anasema Masatu na kuomba kipaumbele cha serikali katika kukabili mabadiliko ya tabia nchi kiwe kwenye sekta ya kilimo na mifugo . Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, asilimia 80 ya watu waishio vijijini, wanategemea kilimo kuendesha maisha yao.