Hukumu ya Lulu: Yapo mengi ya kujifunza

HUKUMU ya Elizabeth Michael ‘Lulu’ kwenda Jela miaka miwili sawa na kumaliza msiba wa marehemu Steven Kanumba, hii ina maana amezikwa tena kifikra, kwa mujibu wa mama yake mzazi Flora Mtegoa.

Haki imetendeka hukumu imetolewa ni muda mwingine wa kuangalia yale ambayo yalitokea ili iwe funzo kwetu tuliobaki uraiani na bado tumepewa nafasi ya kuishi. Mapema wiki hii, Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam ilimhukumu jela miaka miwili Lulu baada ya kumkuta na hatia kwa kumuua Kanumba, Aprili 2012.

Hili liwe funzo kwa Wanatasnia zote mbili kwa muziki wa Bongofleva na Filamu, liwe funzo kwa Wazazi pia liwe funzo kwa Serikali na kila binaadamu kwakuwa siku na saa yoyote huenda likamtokea mwingine sababu hata wao hawakutarajia.

Wasanii liwe funzo kubwa kwao, ukizingatia Lulu na Kanumba wote walikuwa wasanii wa tasnia ya filamu. Wasanii wajifunze sanaa sio chombo cha kuendeshwa kwa rushwa ya ngono, kwaajili ya kumsaidia mtu afikie malengo yake, wawe na msimamo wamsaidie mtu kama wanaweza kama hawawezi wamwache aende kutafuta rizki kwingine.

Lakini sio kutumia sanaa kumlaghai mtu kwa kumwaminisha kwamba utamtoa katika sanaa yake, kumbe ulikuwa na lengo la kumtumia kwa kuchukulia kigezo cha shida zake na umri wake.

Najua wasanii wengi watakataa kwamba hawana mahusiano na wasanii wachanga, ambao wanatamani kuigiza huku umri wao ukichini ya miaka 18 tena wengine wakiwa shuleni.

Najua watakataa kwamba wao wanamashabiki wengi wanawake, lakini kundi kubwa la mashabiki hao ni wanafunzi wa Sekondari na shule za msingi ambao wengi wanandoto za kuwa na umaarufu mkubwa kama wa Wema Sepetu, Jackline Wolper au Kajala Masanja.

Wajifunze kwa mfumo wa kesi ya Lulu ulivyokuwa ukienda, ingekuwaje kama Kanumba asingekufa? Leo ingekuwa aibu ya mwaka kwa kutembea na mtoto wa miaka 16. Na pengine katika kukwepa hilo ndio maana uhusiano wa waili hao ulikuwa wa siri, hakuna aliyefahamu mpaka baada ya tukio la kifo cha Kanumba, ndipo siri ilipofichuka kwamba wawili hao walikuwa wapenzi.

Watu wa haki zote tungewasikia, huenda hukumu ya Lulu ingekuwa yake, kwa kesi ya kubaka ambapo tunajua kabisa ni miaka mingapi angetumikia jela. Hivyo hukumu ya Lulu na kifo cha Kanumba iwe somo kwa wasanii wengine, kwakuwa makosa kama hilo linaweza kutokea kwa mwingine kwakuwa maisha hayana mfumo maalumu wa kuelekea.

Unaweza usipatwe na umauti kama ilivyokuwa kwa Kanumba, lakini ukadhalilika kwa kuingia jela miaka 30 kwa kujihusisha kwenye uhusiano wa kimapenzi na mtoto aliye chini ya umri wa miaka 18.

Hata hivyo hatutaacha kumkumbuka Kanumba, kwakuwa msaada wake wa kuinua tasnia ya filamu ni mkubwa, ingawa kifo chake kimezua maswali mengi na mafunzo yasiyokuwa na mwisho.

Lakini pia kilichomkuta Lulu, iwe funzo kwa wazazi na walezi wenye watoto aina yake, wawe wapo kwenye filamu, muziki au wanafunzi. Mtoto anabaki kuwa mtoto na mzazi ama mlezi wake lazima azingatie misingi ya kumlea mtoto, ukuaji wa Lulu sababu ya umaarufu wake haikuwa siri ya alichokuwa akikifanya, kwani mara kwa mara alikuwa akipamba kurasa za magazeti ya udaku, mara kalewa chakari harusini, mara kakutwa kwenye kumbi za burudani.

Mtoto wa chini ya umri wa miaka 18 anafuata nini kwenye kumbi za starehe? Mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18 anaendaje harusini peke yake na kulewa?. Lawama hizi pia ziende kwa wasanii wenzake wakubwa wakati huo ambao walikuwa wakienda nae kwenye harusi na kumuacha analewa, huku wakifahamu fika kwamba licha ya kuigiza nae, lakini huyo ni mtoto bado.

Miaka Fulani uongozi wa ukumbi wa Bilicanas uliwahi kumtoa nje Lulu, kwa madai ya kuingia klabu za usiku akiwa na umri chini ya miaka 18. Na siku chache baadae alifanya sherehe kuadhimisha siku ya kuzaliwa akidai ametimiza umri wa miaka 18, lakini kabla ya hapo aliwahi kutamba kumiliki hati ya kusafiria ya mtu mzima na ana uwezo wa kusafiri popote, lakini hakuna yeyote aliyezungumza juu ya hilo si wazazi wake waka wasanii wenzie waliomzidi umri ambao wakati huo wengi walikuwa na umri sawa na mama zake, dada zake, baba zake ama kaka zake.

Suala la kutokuwa na umri wa miaka 18, lilikuja kufichuka baada ya kifo cha Kanumba, ndipo ilipobainika kuwa alidanganya umri ili iwe rahisi kwake kufanya mambo ya kikubwa kama kwenda kwenye kumbi za burudani na mambo mengine.

“Nilikuwa kila nikienda klabu nazuiwa mlangoni, naambiwa mimi mdogo… nikafikiria nikaona ngoja nifanya ‘birthday’ kisha nitangaze nimefikisha miaka 18, lakini lengo lilikuwa nisiwekewe tena vizuizi kwenda klabu,” alisema Lulu kwenye moja ya mahojiano yake na vyombo vya habari miaka ya nyuma.

Wazazi wake walikuwa wapi wakati mtoto wao anatanagaza hadharani kuwa na miaka 18 tena kwa lengo ovu, kwanini wasingemzuia? Mzazi anayemlea mtoto wake kwa maadili ni lazima angejiuliza sababu za mtoto tena binti kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa ushahidi wake Mahakamani, siku ya kifo cha Kanumba, Lulu alikuwa anaenda ‘kujirusha’ na rafiki zake, mama yake alimruhusu vipi? Mtoto wa chini ya miaka 18 anatokaje usiku na marafiki na mzazi roho iwe tuli.

Wazazi wengi katika sanaa ya filamu na muziki, wamekuwa hawaulizi mali ambazo watoto wamekuwa wakizipata, hata kudadisi ingawa magazeti yanakuwa yanaandika ukweli. Wazazi wamekuwa kimya kwa kuamini kwamba wanakula matunda ya watoto wao, hivyo linapotokea tatizo ndipo wanaposema mwanetu alikuwa akibakwa.

Ni bora kuziba ufa hata kwa matope na miti, ili ukianguka uanguke wakati umeshahamia nyumba nyingine kuliko kuuacha kwa kusema kwa maneno ukuta usianguke mpaka nihame. Lakini pia kuna la kujifunza kwa Serikali yetu kupitia wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na michezo, kupitia kitengo chake cha Baraza la Sanaa Tanzania.

Magazeti yamekuwa yakiandika habari nyingi za wasanii kuhusiana na matendo yao ya kutoka usiku, kudanganya miaka na matukio ambayo yapo chini ya umri wao. Kwa mfano kupitia mitandao ya kijamii, baba mzazi wa mwanamitindo wa video maarufu kama Tunda, amekuwa akilalamikia baadhi ya msanii kumharibu mtoto wake.

Mzee yule aliongea mengi na magazeti mengi yaliandika kwamba mwanaye bado mwananfunzi, ila wanamuziki wanamtumia katika video zao na kumharibia maisha yake ya baadaye.

Niliwahi kumsikia mwigizaji mwingine Hanifa Daud Maarufu kama Jenifa wa Kanumba, naye miongoni mwa watu waliowahi kulalamika kwamba kuna unyanyasaji wa kijinsia katika tasnia ya filamu.

Lakini sijasikia kitengo chochote cha Serikali kinachohusiana na sanaa ambacho kikaivalia njuga habari hiyo, hata kwa kuhoji umri wa binti huyo. Labda kuweka wazi kwa baadhi ya vitu kama hivi kusaidia kesi kama hii ikitokea watu kupata majibu ya haraka, mepesi na kila mtu akapata haki stahiki kwa mujibu wa sheria.

Lakini wakisema wakae kimya basi kila msanii atakuwa akimchukua mtoto akimfundisha sanaa, akiwa mkubwa anakula matunda yake mwenyewe kwa kumfanya mpenzi wake, hapo ndipo watu watakapoacha kuwapeleka watoto wao kufanya sanaa.

Kisha tutaendelea kulalamika kwamba sanaa ya Tanzania haikuwi, ndio kwanza inakufa, mara filamu za nje zinaua filamu kumbe sisi wenyewe tunaendesha filamu ili kufanya mambo yetu.

Sina lengo la kushambulia upande wowote katika makala haya, bali nataka wadau wa sanaa, wazazi na watoto kujifunza kupitia hukumu ya Lulu. Leo Lulu amehukumiwa akiwa mtu mzima, akitoka gerezani atakuwa na maisha yake na baadae atakuwa na familia, lazima ahakikishe njia alizopita yeye watoto wake hawapiti, ajifunze malezi mazuri ya watoto wake kupitia makosa waliyofanya wazazi wake kwake mpaka leo kumkuta yaliyomkuta. Lala kwa amani Kanumba.