Afrika Mashariki na sera za kudhibiti matumizi ya tumbaku

ZAIDI ya watu bilioni moja ulimwenguni wanavuta tumbaku na takriban watu milioni sita hufariki dunia kila mwaka kutokana na madhara yatokanayo na tumbaku. Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Zaidi ya vifo milioni tano kati ya hivyo ni matokeo ya uvutaji wa moja kwa moja wakati zaidi ya vifo 600,000 ni vya watu wasiovuta ambao huathirika na moshi wa tumbaku. WHO kwa kubaini kuwa tumbaku ni janga la kimataifa, lilitunga Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Tumbaku (FCTC).

Madhumuni yake ni kulinda kizazi cha sasa na kijacho dhidi ya majanya kiafya, kijamii, kiuchumi na kimazingira, yatokanayo na matumizi ya tumbaku na moshi wake. Mpaka sasa nchi 180 zimeridhia mkataba huu. Nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki, zimeridhia mkataba huo ukifuatiwa na utengenezaji wa sheria na kanuni dhidi ya matumizi ya tumbaku na mazao yake.

Kenya ndiyo nchi ya kwanza katika ukanda kuanzisha sheria mwaka 2007 iliyokuja na kanuni za udhibiti wa tumbaku kwa lengo la kulinda afya ya jamii. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa nchini humo mwaka juzi, takwimu zinaonesha watu milioni 2.5 sawa na asilimia 13, wanatumia tumbaku. Asilimia 10.1 ya hao, wanatumia mazao ya tumbaku kama vile sigara, kiko, shisha na asilimia ya waliobaki, wanatumia tumbaku isiyotoa moshi.

Ingawa sheria imeanza kufanya kazi tangu mwaka 2007, manufaa yaliyotarajiwa hayajatimia ipasavyo kutokana na kuchelewa kwa utekelezaji wa kanuni zake. Baada ya kampuni za tumbaku kuona kuwa kanuni hizi ni tishio kwa biashara na mtiririko wa pato, zilianza kupambana kwa kufungua shauri mahakamani dhidi ya kanuni.

Februari mwaka huu, Mahakama ya Rufaa ya Kenya ilitoa uamuzi ambao ulitupilia mbali madai ya kampuni ya British American Tobacco (BAT) ikisema kanuni hizo ni kwa maslahi ya afya ya umma. Awali, kampuni hiyo ilizuia utekelezaji wa kanuni za udhibiti wa tumbaku za mwaka 2014 kuanza kutekelezwa Juni 2015 kwa kufungua shauri Mahakama Kuu.

Machi mwaka jana, Mahakama Kuu ilitoa uamuzi uliotupa madai na kampuni ikakata rufaa. Nchi nyingine mwanachama wa jumuiya iliyoridhia mkataba ni Rwanda ambayo pia ilianzisha sheria ya udhibiti wa tumbaku mwaka 2013. Sheria hiyo ilichapishwa kwenye Gazeti la Serikali Aprili 8, 2013 huku pamoja na kanuni zikitoa mwongozo, kuzuia na pia kudhibiti matumizi ya tumbaku.

Mathalani, kupitia sheria husika, watu walio chini ya umri wa miaka 18 wanakatazwa kushika tumbaku na bidhaa zake. Kanuni zinasisitiza kutaarifu, kuelimisha na kuwasiliana na jamii kuhusu athari za kiafya, mazingira, uchumi na kijamii. Kwa upande wa Uganda, Sheria ya Udhibiti wa Tumbaku ilianzishwa mwaka juzi. Pamoja na masuala mengine, sheria hii ambayo imeanza kutumika Mei 2015, inakataza uvutaji sigara katika maeneo ya umma.

Miongoni mwa vifungu katika sheria hiyo ni pamoja na vinavyozuia matangazo ya kunadi tumbaku na bidhaa zake pamoja na kuruhusu udhamini kama inavyoelezwa katika kifungu cha 2(b-c) cha sheria hiyo. Hata hivyo, kama ilivyotokea Kenya, pia kwa Uganda, kampuni ya BAT-Uganda ilifungua shauri ikitaka zuio la utekelezaji wa kanuni za sheria hiyo.

Kwa upande wa Tanzania, serikali iliridhia mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Tumbaku Aprili mwaka 2007. Sheria iliyopo ni ile ya Usimamizi wa Bidhaa za Tumbaku, Sura ya 121 ya mwaka 2003 ambayo pamoja na mambo mengine, inapiga marufuku matumizi ya bidhaa zote za tumbaku kwenye maeneo ya umma.

Hata hivyo Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania (TTCF) kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wake, Lutgard Kagaruki kinasema wakati nchi za Afrika Mashariki zina sheria madhubuti ya kukidhi matumizi ya tumbaku zinazoendana na matakwa ya mkataba, kwa upande wa Tanzania haijakidhi hilo.

Kinasema uzalishaji wa tumbaku unaongezeka wakati Kenya na Uganda kilimo hicho kikishuka na kujikita katika kulima mazao mbadala. Akihimiza serikali kujizatiti katika udhibiti wa matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, Kagaruki ananukuu kaulimbiu ya mwaka huu ya WHO ya Siku ya Kutotumia Tumbaku Duniani inayosema tumbaku ni tishio la maendeleo.

Kama ambavyo baadhi ya nchi za Afrika Mashariki zimejielekeza katika kulima mazao mbadala wa tumbaku, TTCF kinasisitiza kuwa kilimo cha tumbaku katika hali ya kawaida kinaweza kudhaniwa kuwa na faida lakini athari za zao hili ni kubwa kiuchumi kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla.

Kagaruki anatoa mfano wa Malawi kuwa ni nchi inayoongoza kwenye kilimo cha tumbaku katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara lakini pato lake la taifa ni la chini sana. Anasema robo tatu ya nchi hiyo ni jangwa, kutokana na ukataji miti kwa ajili ya kukaushia tumbaku.

Chama hicho kinazungumzia athari za kiafya za tumbaku kwa kunukuu utafiti uliofanyika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ya jijini Dar es Salaam unaoonesha kuwa matibabu ya saratani hulisababishia taifa hasara ya zaidi ya Sh bilioni 89 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Huduma za Kinga ya Saratani katika Hospitali ya Taifa ya Ocean Road, Dk Chrispin, takribani saratani zote zinahusishwa na tumbaku; Lakini zaidi ni saratani zinazoathiri maeneo ya mfumo wa chakula ambao unaanzia kwenye kinywa ukihusisha ulimi, mdomo, njia za hewa, koo na tumbo.

Aidha utafiti uliofanyika hospitali ya Taifa Muhimbili mwaka 2014 ulionesha kuwa, gharama za matibabu ya magonjwa ya moyo yanayohusishwa na matumizi ya tumbaku, yaligharimu zaidi ya Sh bilioni 400 kwa mwaka. Lengo la wanaharakati wa kudhibiti tumbaku duniani ni kuiona tumbaku inapotea kwenye ajenda za kimataifa ifikapo mwaka 2030.

“Tunawaomba viongozi wetu waone na kukubali kuwa tumbaku ni janga la kitaifa na halina faida kwa mkulima wala kwa taifa, bali inafaidisha kampuni zinazohusika,” anasema Kagaruki. Shauku ya wanaharakati wanaopinga tumbaku ni kuona nchi zote zinashiriki mapambano dhidi ya tumbaku kuepuka madhara yake kiafya, kiuchumi, kijamii na kimazingira.

Matumizi ya tumbaku katika Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla yanatajwa kuwa yatapungua (kama si kukoma) endapo watu wataelimika zaidi na kufahamu madhara yake kwa mapana.

Wakati huo huo kutungwa sheria madhubuti za kudhibiti zinazoendana na matakwa ya mkataba wa WHO, ni hatua nyingine ambayo TTCF na wanaharakati wengine wanasema italeta udhibiti wa kutosha wa matumizi ya tumbaku na bidhaa zake siyo tu katika ukanda, bali Afrika nzima.

WHO linasisitiza kuwa sera bora za kudhibiti matumizi ya tumbaku zina manufaa makubwa kiuchumi na kijamii. Sera hizo ni pamoja na kuongeza ushuru kwenye bidhaa za tumbaku na udhibiti wa matumizi na hivyo mapato kutumika katika shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.

Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa (UM) mwaka huu, Mshauri wa Masuala ya tumbaku, ofisi ya WHO kanda ya Afrika, Dk Ahmed Ouma alitaja Rwanda, Kenya, Chad na Mauritius kuwa ni nchi ambazo zimejumuisha sera za udhibiti kwenye bajeti na wakulima wa tumbaku wanahamasishwa kilimo mbadala.

Akiwasilisha ripoti ya WHO ya mwaka huu kuhusu janga la tumbaku, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus anasema kwa kufanya kazi pamoja, nchi zinaweza kuzuia vifo vya mamilioni ya watu ambao wanafariki dunia kwa sababu ya magonjwa yanayotokana na matumizi ya tumbaku. Anasema pia zitaokoa mabilioni ya dola kila mwaka yanayotumika kusaka huduma za afya na kudumaza nguvu kazi.